Watanzania mwaka huu wa 2015, ukweli wameuanza kwa shauku kubwa ya kutaka kupata viongozi wapya watakaowaongoza katika miaka mitano ijayo, na kuweka mustakabali wa maisha ya watu na maendeleo ya nchi.
Shauku hiyo inatarajiwa kuwafikisha kwenye mshindo mkuu utakaowapatia viongozi bora katika ngazi ya kata, jimbo na Taifa. Mshindo huo ni Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kujenga historia mpya ya maendeleo ya Watanzania chini ya nadharia ya mabadiliko.
Tayari hivi sasa hekaheka na shamrashamra zimezagaa katika kila eneo la makazi ya watu; huku vijana wake kwa waume wakirandaranda na kaulimbiu za vyama vyao vya siasa, wakati wazee wakitafakari namna watakavyochukuana na wimbi hilo la vijana la mabadiliko.
Kwangu msimulizi wa fasihi hii sina shida na vishindo hivyo vya vijana au wazee wala wagombea wanaotaka kuwa viongozi wa Taifa letu. Shida na hofu yangu ni matamko yatolewayo na baadhi ya wagombea, wapambe, wanachama na mashabiki wa vyama vya siasa mbele ya kadamnasi ya wananchi watakaopiga kura kuwachagua hao viongozi.
Tangu filimbi ilipopulizwa kuanzisha kampeni kwa wagombea kunadi ilani na sera za vyama vyao, matamko mbalimbali yametolewa kwa wananchi na makundi hayo. Naamini bila ya mashaka matamko hayo yamepokewa katika hisia tofauti.
Ya kuwaaminisha watu ya kuwa hakuna kilichofanyika tangu nchi hii kupata uhuru mwaka 1961. Ya kuwaaminisha katika sanduku la kura kuna wizi na hakuna haki itakayopatikana. Na mwisho kuwahamasisha vijana kufanya vurugu wao wasiposhinda uchaguzi.
Matamko kama hayo yanakolezwa na baadhi ya wagombea wanapotamka “Hakuna wa kunizuia; Ikulu ni yangu; sina msamiati wa kushindwa; ni kushinda tu…” na kadhalika. Binafsi napata shida kuendelea kunukuu matamko kama hayo yenye dalili ya kuvunja amani iliyopo. Falsafa na saikolojia niliyofunzwa yanitia vigingi kunukuu na kutamka zaidi.
Nashangazwa ninaposikia matamko hayo yakitoka vinywani mwa wagombea na wapambe katika kutafuta ridhaa ya kuongoza nchi yetu. Zaidi ya mshangao ni haohao tena wanapotamka wanaenzi falsafa za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ikiwamo ya mabadiliko. Je, Baba wa Taifa aliwahi kutuhamasisha viashiria vya kuvunja amani ya nchi yetu wakati na baada ya uchaguzi endapo upande mmoja umeshindwa?
Je, Mwalimu aliwahi kutuaminisha hakuna haki katika sanduku la kura na tujiandae kufanya vurugu? Je, Mwalimu aliwahi kututamkia kuwa katika uchaguzi hakuna msamiati wa kushindwa isipokuwa upo msamiati wa kushinda tu? Kwa matamko kama hayo ndiyo kumuenzi Mwalimu?
Ninapowasikiliza wagombea wote wanapokuwa majukwaani, kila mmoja anamgusa Mwalimu Nyerere katika falsafa na njia zake za uongozi alizopita. Kila mmoja anasema atapambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini. Ni nani huyo?
Anapotamka kutoa elimu bure, iwe kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu au kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Ni nani huyo? Mimi na hao wagombea na wapambe na wengine ni wahusika na mashahidi wa elimu bure. Ni nani huyo?
Tulikotoka (1960-1980) mtu kuwa na motokaa ni anasa au utajiri. Leo (1990-2015) mtu kuwa na motokaa si anasa wala utajiri. Ni uwezo. Watu wengi sasa wana uwezo wa kuwa na pikipiki, motokaa hata nyumba. Hii maana yake Watanzania wanaendelea. Kwa hiyo, yapo yaliyofanyika tangu nchi kupata uhuru.
Nakiri kusema Serikali ya Awamu ya Kwanza ilionesha kuwapo kwa tabaka tatu za maisha ya Watanzania. Na uwiano wake katika kipato cha mtu. Tabaka la watu wa hali ya chini, la watu wa hali ya kati na tabaka la watu wa hali ya juu. Leo tabaka la watu wa hali ya kati halipo. Tabaka la watu wa hali ya chini ni mashaka ukilinganisha na tabaka la watu wa juu. Hapa pana mushkeli. Umetoka wapi?
Hayo pia ni mabadiliko. Je, ni mabadiliko tuyatakayo? Ni dhahiri shahiri hapana. Wagombea na wapambe hamna budi kutumia hekima na busara kuchunga ndimi zenu mnapotoa matamko, kwani kauli hizo za leo kesho ni umbo kwa jamii.
Kama viongozi waasisi wa Taifa hili wangelikuwa wanatoa matamko ya kuwaaminisha Watanzania na hasa vijana wa jana; leo ni wazee kufanya matendo ya kuvunja amani Tanzania ya leo isingekuwa hivi. Tutambue amani inaundwa si kweli amani inashuka kama mvua au ipo kiasili. Amani inatokana na ukweli, haki, upendo na umoja.
Wagombea na wapambe hayo mnayotamka mtambue wasikilizaji tunaamini yanatoka moyoni mwenu. Na kama yanatoka moyoni au rohoni ni hatari kwa Taifa letu. Msituaminishe eti yanatoka vinywani mwenu tu, hapana. Kwa sababu kiongozi bora lazima awe muadilifu; akiwa ni kweli na mtenda haki.
Wanachama na mashabiki wa vyama vya siasa muelewe kuwa uanachama na ushabiki wenu katika siasa ni maisha, ni uhai, ni usalama. Tofauti na uanachama na ushabiki katika vyama vya michezo. Michezo ni furaha, ni burudani. Siasa ni maisha. Maisha hayaonjwi kama mchuzi wala hayajaribiwi kama nguo mwilini.
Tufananishe na kulinganisha embe na parachichi ni matunda yana utamu na ladha gani. Tusifananishe na tusilinganishe samaki (kitoweo) na mboga ya majani kama ya kunde kutafuta tamu na ladha. Huo siyo ulinganishaji wa haki na usawa wa mboga ni kubananga tu.
Vijana ni Taifa la leo na kesho, sikilizeni matamko na muyatafakari kwa kina na kuyapima kwa adabu katika mizania iliyo sawa. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni na mbayuwayu ni ndege. Akili kichwani mwako.