Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga (TAKUKURU), imefanikiwa kudhibiti wagonjwa hewa 313 wa VVU kwenye mfumo wa usajili wa wagonjwa hao wilayani Muheza.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 2,2022 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga Zainabu Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitoa taarifa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2022.
Amesema TAKAKUKURU kupitia vyanzo vya siri ilibaini kuwa watoa huduma za afya wanaohusika na kusajiliwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi,wamekuwa wakifanya udanganyifu kwa kuwaingiza majina hewa ili kuonesha takwimu za wanaoishi na VVU kuonekana zipo juu kwa maslahi yao binafsi.
Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga amesema katika ufuatiliaji wa mkoa ulibaini kuwa wahudumu wa afya wanaohusika na zoezi la kuwasajili na kuwafuatilia wagonjwa wanaoishi na VVU wamekuwa wakilipwa posho ya gharama ya usafiri ka mawasiliano kiasi cha sh. 20,000 kwa siku kila wanapotoka kwenda kukutembelea wagonjwa hao.
Amesema kwamba fedha hizo hulipwa na Shirika la Afya la Amref kwa kazi ya kufuatilia kila mgonjwa kwa lengo la kuhakikisha hali yake kiafya inaimarika kwa maana ya kutumia dawa kwa wakati na huduma nyingine zinazostahili.
Aidha amesema fedha hizo kulipwa moja kwa moja kwa mhudumu husika kupitia namba yake ya simu ya mkononi na ndiyo sababu inavyopelekea watumishi wasio waadilifu kuweka takwimu hewa kwa lengo la kujiongezea posho.
Ameeleza katika ufuatiliaji uliofanywa na TAKUKURU kwa baadhi ya Zahanati ilibainika kuwa ni kweli kuna wagonjwa ambao siyo halisi kwa maana ya upatikanaji wake na hivyo kufanya udhibiti kwa kuchukua hatua.
Amesema kwamba hatua walizoanza kuchukua ni kufikisha kikao cha pamoja kati yao na ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya na watendaji wake wote wanaohusika na kuwahudumia watu wanaoishi na VVU pamoja na Amref.
”Katika kikao TAKUKURU iliwasilisha yaliyobainika katika ukaguzi wa kutembelea jumla ya zahanati 7 kati ya 16 zilizopo katika Wilaya ya Muheza na kubaini tatizo hilo” amesema.
Hata hivyo amesema kwamba katika kikao kazi hicho ilimuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza kufanya uhakiki wa takwimu za wagonjwa wote wanaoishi na VVU na kutoa taarifa ya uhakiki.
Amesema baada ya agizo hilo ilibainika kuwepo kwa jumla ya wagonjwa hewa 313 ambapo idadi hiyo iliondolewa kwenye mfumo.
Pia amesema wahusika katika usajili wa wagonjwa hao hewa wamepewa barua za kujitoleza kwa kitendo cha usajili wagonjwa hewa huku Wizara ya Afua ikitoa maelekezo ya kufanyika uhakiki kwa wateja wanaotumia dawa ambao sio halisi.
Hata hivyo taasisi hiyo inaendelea kuwasihi watumishi wote wa Umma kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni,taratibu,sheria na kiongozi iliyopo katika utekelezaji wa majukumu yao.