Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ametangaza matokeo ya sensa ya wanyamapori iliyofanyika mwaka huu ambapo Tanzania inatajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya nyati Barani Barani Afrika kwa kuwa na jumla ya nyati 191,805.
Akitangaza matokeo hayo jana Jijini Arusha, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana alisema nyati hao wengi wanapatikana katika mifumo ikolojia ya Serengeti (69,075) Nyerere-Selous-Mikumi (66,546) Katavi-Rukwa (35,273) pamoja na Ruaha-Rungwa ( 20,911).
Amesema lengo la Sensa hiyo ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitatu katika mfumo Ikolojia wa Katavi – Rukwa na Ruaha-Rungwa ni kujua uwepo, idadi, mtawanyiko pamoja na viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori nchini Tanzania.
Akizungumzia kuhusu idadi hiyo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema imeendelea kuongezeka hasa katika maeneo ya ndani ya hifadhi ambapo nyati hao wameongezeko kwa asilimia 64 toka mwaka 2018.
Alifafanua kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto za mifugo katika mifumo ya Ikolojia nyati wameongezeka na hii ni kiashiria kizuri cha udhibiti wa mifugo kwenye maeneo yaliohifadhiwa.
Akizungumzia matokeo ya sensa katika mfumo wa ikolojia wa Katavi Rukwa, Waziri Dkt. Pindi Chana amesema idadi ya tembo imeendelea kuimarika na viashiria vya ujangili wa tembo vimeendelea kupungua ukilinganisha na sensa ya mwaka 2018.
Amefafanua kuwa mamo mwaka 2021, uwiano wa mizoga mipya ya tembo ilikuwa asilimia 3 wakati mwaka 2018 ilikuwa asilimia 12.
Katika hatua nyingine, Balozi Dkt. Pindi Chana alisema katika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha- Rungwa idadi ya wanyamapori adimu kama korongo na palahala imeendelea kuongezeka. Korongo wameongezeka mara mbili toka korongo 1,436 mwaka 2018 hadi 3,127 kwa sensa ya mwaka 2021.
Zoezi hili liliwezeshwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori (Wildlife Conservation Society – WCS) na kuratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).