Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa, amesema hana muda wa kuwajibu wale wote wanaomsakama, lakini amejipambanua kuwa anataka kuwatumikia Watanzania kuanzia mwezi huu.
Lowassa amesema kwa malengo hayo ya kutaka kuwatumikia Watanzania ambao kwa zaidi ya miaka 50 ya Uhuru na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wameshuhudia nchi inakabiliwa na matatizo ya kimsingi ikiwamo rushwa na ufisadi.
Miongoni mwa watu wanaomsakama Lowassa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, anayeelezwa kushika wadhifa huo kwa kazi maalum ya ‘kumtukana’ mgombea huyo wa Chadema tangu alipokuwa mwanachama wa chama tawala.
Amesema kwamba amekuwa akisakamwa yeye pamoja na uongozi mzima wa vyama vinavyounda Ukawa, lakini anachokiona yeye kutoka kwa wapinzani wake, “Wanapoteza muda mwingi bure. Nasema wanapoteza muda.”
Akizungumza jioni ya Jumamosi iliyopita mara baada ya mkutano wake huko Pemba visiwani Zanzibar, Lowassa anasema kwamba kwa namna Ukawa ilivyopanga, “CCM hawatuwezi. Kama nilivyosema wanapoteza muda.”
Anasema kuwa ameshikilia msimamo wa kuboresha elimu, mfumo wa afya na miuondombinu duni, umaskini, ukiukwaji wa haki, vitu ambavyo vimekuwa ni sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania.
Lowassa anawania nafasi hiyo kupitia Chadema inayoungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambavyo ni National League for Democracy (NLD), Chama cha Wananchi (CUF) na The National Convention for Construction and Reform-Mageuzi maarufu kwa jina la NCCR-Mageuzi.
Lowassa anasema kuwa ilani ambayo imechapishwa kwenye gazeti hili imelenga kumkomboa kila mwananchi kutokana na hali kandamizi ya utawala wa CCM, kuondoa umaskini, kuleta maendeleo na kusimamia haki na usawa.
Ukawa imekuwa ikishutumiwa kununuliwa na Lowassa ambaye wapinzani wake walianza kwa kumnanga kuwa anakodi watu kwenda kwenye mikutano yake na kwa sasa wanadai kuwa ni mgonjwa ambaye hawezi kuongoza.
“Niko fiti. Naomba uwaulize hao wanaonisema vibaya kama nanunua watu. Ina maana kila siku nanunua? Sina muda wa kujibizana nao. Watanzania wana kiu ya mambo mengi. Waache kupiga kelele eti watatushughulikia na kwamba hatuna uwezo, sisi tunasema majibu ni Oktoba 25, siku zote nasema huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono,” anasema Lowassa.
Lowassa amewatoa hofu wananchi kwamba Ukawa wakichukua nchi kutakuwa na vurugu, “Labda vurugu walete wao CCM. Sisi tunataka kuwatumikia Watanzania ambao wamechoka kunyanyasika. Hawawezi kufanya chochote,” anasema.
Lowassa anasema kutokana na idadi kubwa ya watu wengine wanaohamasika kwenye mikutano yake, ataunda Serikali rafiki kwa maskini hasa waendesha bodaboda, Mama Ntilie na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga.
Lowassa amesisitiza kuunda serikali rafiki na kwamba mtendaji yeyote atakayeteuliwa hana budi kufanya kazi kwa muda mrefu, ili kuhakikisha uchumi unakuwa na maendeleo yanapatikana kwa haraka.
Mbali ya Lowassa, mwingine aliyezungumza na Gazeti la JAMHURI juzi, ni Frederick Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu mwenye rekodi ya aina yake ya kuitumikia nchi kwa miaka 10 mfululizo.
Sumaye anasema wananchi wameivumilia CCM vya kutosha, hivyo inatosha iondoke madarakani na kwamba hakuna cha kuzuia Lowassa kuingia madarakani 2015.
Anasema kwamba CCM iliahidi mengi kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na “Maisha bora kwa kila Mtanzania”, ahadi ambayo kwa mujibu wa Sumaye, haijakamilishwa na uongozi unaotarajiwa kuondoka madarakani.
“Ninachoweza kusema ni kwamba bado Watanzania wako nyuma kimaendeleo. Wanachotakiwa kwa sasa ni kuiondoa CCM madarakani. Watanzania wafanye hivyo hasa mwaka huu,” anasema.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, ambaye kwa sasa anawania nafasi hiyo, anasema: “Katika siasa kuna mambo mengi. Safari hii Watanzania wanakwenda kufungua ukurasa mpya wa maisha yao.”
Jussa, ambaye kitaaluma ni msomi wa sheria, anasema kwa jinsi anavyoona, CCM ya Mwalimu Nyerere imepotea na waliobaki kwa sasa ni kila mmoja kuangalia maslahi yake.
“Muda wa CCM kuondoka madarakani umetimia. Wakati wake umefika,” anasema Jussa na kuongeza kuwa CCM kwa sasa inafanya hila zote za kuwarubuni Ukawa, lakini itakuwa ngumu kufanikiwa.
Hatua ya Ukawa kusakamwa ilichukua sura mpya wiki iliyopita ambako uongozi wa NCCR-Mageuzi umemsimamisha wadhifa Makamu Mwenyekiti wake, Leticia Masore, kwa madai ya kukiuka taratibu sambamba na kushirikiana na CCM kukihujumu chama hicho.
Kadhalika, anadaiwa kushirikiana na baadhi ya makamishna wa chama hicho kupanga njama za kutaka kupindua uongozi wa NCCR-Mageuzi chini ya Mwenyekiti, Mhandisi James Mbatia.
Juhudi za gazeti hili kumpata Masore zimegonga mwamba. Mbatia anasema, “Vita ni kubwa mno maana CCM wamepania kabisa kusambaratisha Ukawa.”
Katika mahojiano yaliyofanyika juzi, Mbatia anasema kwamba mkakati wa CCM wa kurubuni viongozi wa NCCR-Mageuzi na Ukawa kwa ujumla ni mkubwa, kwani uliwahi kumgusa baada ya kutakiwa ajitoe Ukawa kama ilivyowatokea kwa viongozi wengine wa umoja huo.
Viongozi waliojiondoa Ukawa ni pamoja na Mwenyekiti wa CUF wa zamani, Profesa Ibrahim Lipumba, na Dk. Willibroad Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema.
“Hata kwangu wamekuja sana. Ningependa fedha ningejitoa, lakini nataka kuwakomboa Watanzania wenzangu,” anasema Mbatia na kuongeza: “Hawatuwezi kwa sababu upinzani kwa sasa hasa Ukawa tuna nia ya dhati ya kuwatumikia Watanzania. Zimebaki kama wiki tatu, Watanzania waamue nini cha kufanya.”
Mbatia anasema kwamba uamuzi wa kumsimamisha Masore umefuata taratibu, kwani unatokana na kikao cha viongozi wakuu kilichofanyika Septemba 22, mwaka huu kusubiri kikao cha kamati ya nidhamu.
Anasema kwamba Ukawa ina bahati ya kuwa na vijana ambao wako vizuri kwenye mawasiliano na namna watu wanavyokutana kati ya viongozi wa NCCR-Mageuzi na wengine wanaopanga njama mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwazuru viongozi akiwamo yeye Mbatia.
“Tulipata taarifa za kiintelijensia. Kwa kifupi tuko vema kupata taarifa. Mheshimiwa Masore anajua na hata kama atajibu… atajibu tu kwa sababu ya kubisha, lakini tunajua kila kitu kutoka katika vikao vyao,” anasema.
Tayari NCCR-Mageuzi imeshatoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Kawe na kufungua jalada namba KW/RB/9600/2015 ili kuchunguza madai hayo ikiwa ni pamoja na kumtishia maisha Mbatia na Lowassa, mgombea urais wa Ukawa.
Hivi karibuni, Masore akiwa na Mosena Nyambabe, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, na viongozi wengine walijitokeza hadharani kutoa tamko la kupinga mwenendo wa Ukawa, wakisema Chadema imehodhi ushirikiano wa vyama hivyo.
Hata hivyo, imekuja kubainika kuwa Nyambabe alikuwa akipeleleza namna wanavyofanya kazi kabla ya kutoa taarifa kwa akina Mbatia ambao wamekaa na kuamua kupangua uongozi huo.