Serikali imesema mtazamo wa nchi ni kuhakikisha ugonjwa wa Ebola uliopo nchi jirani ya Uganda hauingii nchini Tanzania.
Kauli hiyo imebainishwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu wakati akiwa ziarani mkoani Kagera kuangalia utayari wa mkoa huo kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Prof. Nagu amesema ili kufikia azma ya Serikali katika kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu ni lazima elimu itolewe ya kutosha kwa jamii kwa njia mbalimbali ikiwemo matangazo katika radio za kijamii na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Aidha amewataka Maafisa Afya katika mkoa huo kuwakumbusha wananchi usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa kunawa kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono ili kuwa salama na magonjwa ya mlipuko kama Ebola na magonjwa mengine.
Vile vile, Prof.Nagu amesema pamoja na ulinzi na usalama katika mipaka ya nchi Serikali inajukumu la kujenga uelewa kwa wananchi juu ya ugonjwa huu na dalili zake ili mtu akiwa na dalili hizo aweze kwenda kituo cha kutolea huduma za afya kwa wakati.
Katika hatua nyingine Prof. Nagu amewapongeza na kuwatia moyo watumishi wanaofanya kazi katika mipaka ya Uganda na Tanzania kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhakikisha Tanzania inabaki salama kwa ugonjwa wa Ebola kutoingia nchini.
Pia katika ziara hiyo Prof. Nagu amekagua kituo cha afya Kabyaile kilichopo wilayani Missenyi kilichotengwa kuhudumia wahisiwa wa ugonjwa wa ebola endapo watagundulika kuwa na dalili ya ugonjwa huo.
Katika kituo hicho, ameshuhudia na kukagua Maabara jongezi ya Kisasa iliyosimikwa na Serikali yenye uwezo wa kupima Virusi mbalimbali vya magonjwa ya milipuko ikiwemo Virusi vya Ebola .
Sambamba na hilo amewapongeza kwa Kazi nzuri wataalam wa Maabara ya Taifa kwa kushirikiana na wataalam wa Maabara mkoani Kagera kwa namna walivyojipanga kusimamia upimaji na ubora wa huduma hiyo kipindi chote cha tishio la ugonjwa huu.