kingunge-ngombale-mwiru-2-1Mwanasiasa wa siku nyingi, Kingunge Ngombale-Mwiru, amekiacha “utupu” Chama Cha Mapinduzi (CCM), akidai kimegeuka misingi yake ya kuanzishwa kwake na kwa sasa kinaendeshwa kinyume cha Katiba na taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi nyumbani kwake, Kijitonyama Dar es Salaam, Kingunge anasema ameamua kujitoa kwenye chama hicho kwa sababu, “(CCM) imechoka na kwamba haina tena pumzi” ya kuitoa Tanzania ilipo sasa kwenda mbele.

“CCM imeishiwa na pumzi ya kuongoza. Inafika mahala pumzi inakwisha. Huwezi kuendelea mbele na ukitaka kuendelea wananchi watabaki palepale walipo,” amesema mwanasiasa huyo mkongwe ambaye anajitoa CCM baada ya kuwa mwanachama kwa miaka 61.

Akizungumza taratibu na kuchagua maneno ya kutamka, Kingunge anasema wananchi wa Tanzania kwa sasa wanakabiliwa na changamoto za uchumi, ajira, umaskini ambazo zinaweza kuondolewa na uchumi bora na imara.

Anasema kwamba ndani ya CCM kumejaa ukiritimba na ulevi mkubwa wa madaraka kiasi kwamba imefika hatua ya kubadili vionjo vyake vya salamu bila kujali demokrasia iliyoiasisi.

Na kutokana na uongozi wa sasa wa CCM, kuamua kukibinafsisha chama hicho na kufanya yale wanayotaka wao kwa maslahi ambayo Mzee Kingunge amedai hana hakika ni kwa maslahi ya nani na mambo yanayofanyika ni ya ajabu, ameamua kujitoa.

“Vijana wanatumika kujaribu kudhalilisha watu. Watu wazima. Mavuvuzela wanaajiriwa kuwatukana watu. Mimi nasema, sikubaliani, hicho si chama ambacho tulishirikiana kukijenga. Hiki ni chama kingine,” anasema Kingunge. Kutokana na hilo, Kingunge akasema: “Kwa hivyo mimi kuanzia leo (Jumapili) naachana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa sababu siwezi kuhimili chama kinachoendeshwa bila kuheshimu Katiba kwa sababu Katiba ndiyo inayotuunganisha wote.

“…Nasema kuanzia sasa. Mimi najitoa kwenye Chama Cha Mapinduzi. Najua uamuzi wangu utawasumbua baadhi ya ndugu zangu, rafiki zangu, makada wenzangu, wazee wenzangu ambao wengine tunawasiliana mara kwa mara, hata vijana. Wengi lakini, ni uamuzi ambao lazima niufanye kwa sababu vinginevyo nitajisaliti mwenyewe.

“Nimehusika katika kuweka misingi ya chama chetu, nikaamini ndiyo misingi sawasawa niliyojihakikishia ndani ya chama chetu, lakini sasa demokrasia ndani ya chama inapigwa mateke, halafu wakuu wanakwenda kutangaza kwenye majukwaa na kusema mambo yote yalikwenda sawa, tuliwapa kulea chama na kulea Katiba. Nawaachia Chama Cha Mapinduzi.”

Mbali ya kujitoa, Kingunge alitangaza kutotaka kujiunga na chama chochote kwa kuwa amekuwa mwanaharakati tangu TANU na sasa CCM kwa pamoja miaka 61.

Anaonesha masikitiko akisema, “Nidhamu ya chama ni kuheshimu Katiba na wenzako, sikusudii kujiunga na chama. Mimi ni raia, raia huru wa Tanzania. Nina haki zangu za kisiasa na kijamii.”

Katika kutoa maoni yake, Kingunge amesema ataendelea kutoa misimamo kuhusu Tanzania katika hali ya sasa na kwamba kila itakapobidi atatoa msimamo wake. “Hali ya sasa ina makundi mawili. Kundi moja linasema kidumu chama tawala, maana yake hakuna mabadiliko na kundi jingine linasema tunataka mabadiliko katika nchi yetu.

“Sasa sitaki kusema kundi lipi kubwa, lakini nasema hali iko hivyo. Lakini kwa jinsi ninavyotazama, vijana wanataka mabadiliko, walio wengi ukiacha kakundi ka UVCCM, lakini walio wengi wanataka mabadiliko.

“Najua akinamama walio wengi wanataka mabadiliko. Najua wafanyakazi wanataka mabadiliko,” anasema Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, alimuunga mkono Lowassa. “Nilipoulizwa mara kwa mara, nilisema nitamuunga mkono yule ambaye ziko dalili zote ambazo wananchi wanasema yule anafaa. Nilisema pia kule Arusha. “Maana Mwalimu Nyerere alisema katika harakati za kutafuta mgombea urais, ulizeni wananchi wanasema nini na sikilizeni wananchi wanasema nini.

“Alisema msikae kwenye maofisi mkadhani mnatafuta katibu kata. Lazima awe anakubalika ndani ya CCM na nje ya CCM. Nimerudia kusema, katika hili suala la mabadiliko, mimi niko upande wa mabadiliko.

“Mabadiliko yanahitajika sasa. Vijana, akinamama, wafanyakazi, wakulima na wavuvi, wazee wanataka mabadiliko. Hata kuungana Bara na Visiwani ni mabadiliko,” anasema.

“Kule kuungana ni mabadiliko. Mwaka 1967 kuua TANU na kuua ASP kuunda CCM ni mabadiliko. Tumekuwa na mabadiliko na tumekuwa na mfumo wa chama kimoja. Kwenye Halmashauri Kuu kilichofanyika Dodoma Februari 1992 ni kuingia vyama vingi,” anasema.

Kingunge anasema kwamba mchakato wa kuwapata wagombea watano, ambao Kamati Kuu ingependekeza ili kupata watu ulikuwa na matatizo ya kimsingi.

“Maelekezo ya Katiba hayakufuatwa, Kamati Kuu ndiyo ambayo inawafikiria wagombea wote baada ya kuwasikiliza wagombea wote na wajumbe wa Kamati Kuu kupata nafasi ya kuwahoji na baada ya hapo kutoa uamuzi wa watu watano,” anasema.

Anasema kwamba jambo hilo halikufanyika, majina ya watu watano yalichomolewa kutoka Kamati ya Maadili, ambacho ni kitengo kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu na wagombea wale 38 hawakufika kwenye Kamati Kuu.

“Mchakato wenyewe ni batili. Na leo hii ni vizuri ieleweke, suala hili la watu kugombea urais si jipya. Tulilianza mwaka 1995. Na utaratibu uliofuata kwa mujibu wa Katiba na kanuni ni kwamba baada vya kurejesha fomu zao wale wagombea 16 wakati ule, kikao cha Kamati Kuu kilianza kazi, sekretarieti ilikabidhi orodha yao kwenye Kamati Kuu.

“Wakaitwa mmoja mmoja na kujieleza kwanini wanataka kugombea urais? Wagombea 16 walifika kwenye Kamati Kuu na miongoni mwao ni Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, vilevile Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa,” anasema.