Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi zimesaini hati mbili za makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (The 5th Joint-Permanent Commission for Cooperation – JPCC) kati ya nchi hizo mbili uliofikia tamati jana tarehe 28 Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam.
Hati hizo za makubaliano zilizosainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) na Mhe. Titus Mvalo Waziri wa Sheria wa nchini Malawi zinahusu ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi la Malawi na Jeshi la Polisi la Tanzania, na ushirikiano baina ya Taasisi za Uhamiaji za pande zote mbili.
Akizungumza muda mfupi baada ya kusaini hati hizo, Waziri Ndumbaro na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo, ambaye pia alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ameeleza kuwa Mkutano huo umewezesha pande hizo mbili kukubaliana katika masuala mbalimbali ya msingi huku msisitizo mkubwa ukielekezwa katika sekta ya Biashara, Uwekezaji, Ulinzi na Usalama, Miundombinu, Masuala ya Mambo ya Nje na Kijamii
“Katika Mkutano huu wa Tano wa JPCC pamoja na masuala mengine nchi zetu mbili zimekubaliana kuongeza kasi ya kutatua changamoto zinazokabili sekta binafsi ili kuwezesha na kurahisisha biashara, vilevile tumekubalia kutumia fursa ya uwepo wa Ziwa Nyasa katika kurahisisha uendeshaji wa shuguli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu kwa maendeleo ya wananchi wetu” alisema Dkt. Ndumbaro.
Waziri Mdumbaro aliongeza kutaja fursa na faida mbalimbali zilizotokana na Mkutano huo ikiwemo, nia na dhamira ya Nchi ya Malawi ya kutumia barabara ya Mtwara hadi Bandari Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma katika kusafirisha bidhaa na huduma kwenda nchini humo. Fursa nyingine ni nia ya Malawi kushirikiana na Tanzania katika suala la elimu na mfunzo kupitia Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaa, ambapo alieleza kuwa hati ya makubaliano kuhusiana na suala hilo inatarajiwa kusainiwa siku za usoni.
Dkt. Ndumbaro aliendelea kufanunua kuwa licha ushirikiano na uhusiano mzuri wa Kidiplomasia uliopo baina ya pande hizo mbili, Malawi imeonesha nia ya kutumia Bandari ya Mtwara na Mbamba Bay kutokana na ukweli kuwa njia hiyo ni fupi zaidi ikilinganishwa na njia zote wanazozitumia hivi sasa kutoka Bandari mbalimbali kuingiza bidhaa nchini humo.
Mbali na kuzungumzia fursa za kiuchumi Dkt. Ndumbaro, alitoa rai kwa Serikali ya Jamhuri ya Malawi kuendelea kuthamini lugha ya Kiswahili sambamba na kuhimiza matumizi ya lugha hiyo nchini humo. Vilevile aligusia umuhimu wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi kuendelea kufundisha somo la Kiswahili katika ngazi mbalimbali za elimu nchini humo.
Kwa upande wake Mhe. Titus Mvalo, Waziri wa Sheria wa Malawi na Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi ambaye pia alikuwa anamwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo amebainisha kuwa, masuala yote katika Mkutano huo yamehafikiwa katika wakati sahihi ambapo Viongozi Wakuu wa Serikali za pande zote mbili wanania ya dhati kuona ushirikiano wa Tanzania na Malawi unaleta tija ya kiuchumi kwa wananchi wa pande zote mbili.
Waziri Mvalo aliendelea kuelezea namna Serikali ya Malawi inaweka jitihada katika kukuza lugha ya Kiswahili nchini humo ikiwemo kuongeza somo la kiswahili kwenye mtaala wa elimu nchini humo.
“Moja ya sifa kubwa ya lugha ya Kiswahili ni ile ya kutokuwa na mizizi ya ukabila, siyo rahisi hata hapa nchini Tanzania kusikia kabila moja wapo miongoni mwa makabila zaidi ya 120 yaliyopo likijinasibu kuwa lugha ya kiswahili ya kwake. Tunajivunia lugha hii hadhimu ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha ya asili ya Afrika inayounganisha watu wengi barani hapa” alisema Waziri Mvalo
Akihitimisha hotuba yake ya kufunga Mkutano wa Tano wa JPCC Waziri Mvalo ametoa rai kwa sekta zote kuhakisha wanakutana mara kwa mara ili kufuatilia utekelezaji wa masuala yote yaliyohafikiwa katika Mkutano huo.
Mkutano wa Tano wa JPCC ambao umehitimishwa katika ngazi ya Mawaziri umefanyika kwa kipindi cha siku tatu kuanzia terehe 26 – 28 Oktoba 2022. Mbali na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kwa upande wa Tanzania Mkutano pia ulihudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa. Wengine waliohudhuria ni Watendaji kutoka Wizara, Idara, na Taasisi mbalimbali za Serikali.