Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Songea

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma limeazimia kumuita mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kanali Laban Thomas kwenye kikao cha dharula ili wamueleze kero nne zinazoisumbua jamii ikiwemo ya wafugaji ambao inadaiwa kuna baadhi ya watumishi wasio waaminifu kugeuza mitaji kutoka kwa wafugaji.

Wakichangia kamati ya huduma za uchumi kwenye Baraza hilo walisema kuwa swala la mifugo wilayani humo limekuwa kero kubwa sana licha ya Mkurugenzi kuunda kikosi kazi kwaajiri ya kufanya operesheni ya kuwafukuza wafugaji hao lakini bado hali imekuwa mbaya na idadi ya mifugo inazidi kuongezeka Jambo ambalo linaleta kero kwa wakulima na kutishia uwepo wa njaa.

Walisema kuwa wakulima walayani humo wamekosa msaada licha ya kutoa malalamiko yao serikalini juu ya uhalibifu unaofanywa na wafugaji lakini pia kunawanyama waalibifu kama Tembo nao huvamia mashamba na kufanya uharibifu mkubwa hivyo wameamua kikao hicho kigeuke kamati na maazimio waliyoyatoa wanamuhitaji mkuu wa Mkoa ili akawasikilize kero zao.

Kwa upande mwingine wameitaka Serikali kuiondoa Wilaya ya Tunduru kwenye mfumo wa kuuza zao la mbaazi kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi ya mazao ghalani kama ilivyo fanyika katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kwani hakuna faida wanayopata.

Hayo yalisemwa jana na madiwani hao katika kikao ha kawaida cha Robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Crasta ya walimu wa tarafa ya mlingoti Wilayani humo na kwamba maombi hayo wameyatoa kufutia uwepo wa mkanganyiko wakati wa uuzaji wa zao hilo ambao umekuwa ukijitokeza katika ya Serikali na Wakulima wa zao hilo.

Kufutia hali hiyo madiwani hao wamemtaka Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kanali Laban Thomas kufika na kufanya mazungumzo nao ili waweze kumwelezea vikwazo mbalimbali ambavyo vimekuwa vikipelekea wakulima wengi kutorosha mazao yao na kwenda kuuza Mkoani Mtwara ambapo hakuna huo mfumo.

Wakiongea kwa uchungu kwa niaba ya Madiwani wa kata ya Matemanga Hamis Kaesa, Diwani wa kata ya Namakambale amesema miongoni mwa vitu vitakavyo kiadhibu chama cha mapinduzi katika uchaguzi mkuu wamwaka 2025 ni pamoja na Serikali kuendelea kulazimisha zao la Mbaazi kuendelea kuuzwa kupitia mfumo huo.

Naye Diwani viti maalum Matemanga Stawa Omari amesema kuna kero nyingi ambazo zinawakabili wananchi na wao ndio wawakilishi wa wananchi hivyo RC aitwe ili aje kuelezwa kero hizo na wapate ufumbuzi kwani zimekuwa zikijadiliwa mara kwa mara bila kupata ufumbuzi.

“Tunamuhitaji Rc Ruvuma aje tumwambie maazimio ya baraza letu kuhusu zao la mbaazi , zinatoroshwa na wakulima kutokana na kuto uhitaji mfumo,Halmashauri haipati chochote lakini kuna watu wanalazimisha mfumo huo uendelee kwa maslahi ya nani? “alisisitiza Diwani wa kata ya Mbesa Daniel Mlanda .

Akizungumzia malalamiko hayo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Chiza Marando amesema kuwa ombi hilo wamelichukuwa na kwamba mwakilishi kutoka ofisi ya RAS Joel Mbewa amesikia na atalifikisha sehemu husika.

Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM), Wilaya ya Tunduru Abdalah Mtila pamoja na mambo mengine aliwataka viongozi kuacha kupuuza kero za wananchi na kwamba kwa kufanya hivyo wanashiriki kukididimiza chama cha mapinduzi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

“vitu vinavyo zungumzwa zungumzwa na wananchi visidharauliwe na viongozi eti ni vidogo “ hilo ni bomu ambalo litakiua chama cha mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025” amesistiza Mtila.

Akifunga mkutano huo mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Haillu Mussa amesema,Madiwani wapo tayari Mkuu wa mkoa aitwe na mkurugenzi aandae kikao ambacho hakina posho iliwaje wajadili kero nne ambazo zinasumbua jamii ikiwemo ya uuzaji wa mbaazi kwenye mfumo wa stakabadhi gharani.

Alisema kuwa Halmashauri yake itasimamia maelekezo yote yaliyotolewa kutoka kwa Viongozi na madiwani katika mikao hicho ikiwa ni pamoja na kuongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupanua wigo wa utoaji huduma kwa jamii.

Mwisho.