Na Mwandishi wetu,JamhuriMedia,Babati
Taasisi EBN ambayo inamiliki Kitalu Cha uwindaji katika eneo la jumuiya ya uhifadhi wa Wanyamapori ya Burunge ,imechimbwa bwawa ili kusaidia wanyamapori kupata maji.
Uamuzi huo umefikiwa kutokana na Ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi umeanza kusababisha vifo kwa wanyamapori katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge(WMA) wilaya ya Babati mkoa wa Manyara.
Burunge WMA ipo kati kati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Manyara na inaundwa na vijiji 10 ikiwa nva ukubwa wa kilomita za mraba 283
Licha ya wanyamapori kuanza kufa pia kumeongezeka matukio ya ujangili na migogoro baina ya wananchi na wanyamapori kutokana na wanyamapori hao kuanza kuingia maeneo ya vijiji kusaka maji na malisho.
Meneja Uhusiano wa EBN, Charles Sylvester amesema wameamua kuchimba mabwawa na kutoa maji kwa Wanyamapori ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani maji yamepungua sambamba na malisho.
“Hivi Sasa eneo letu kuna idadi kubwa ya Wanyamapori tofauti na miaka ya nyuma kabla ya kupewa Kitalu hiki ambapo pia Sasa Wanyamapori wamekuwa rafiki na watu na kuwezesha utalii wa picha na Makundi makubwa ya wanyamapori yamerejea katika Kitalu”amesema.
Amesema wameimarisha pia doria za kupambana na ujangili na uvamizi ndani ya hifadhi kwa kushirikiana na Mamlaka ya usimamizi Wanyamapori ( TAWA),askari wa Burunge WMA, Maafisa wanyamapori na askari wa hifadhi za Taifa ( TANAPA).
“Tunatumia zaidi ya milioni 400 kwa mwaka kukabiliana na ujangili na hasa kipindi hiki Cha Ukame ambapo wanyamapori wanasogea vijijini”amesema Katibu wa Burunge WMA,Benson Mwaise.
“Katika siku za karibuni wameanza kufa kutokana na kukosa maji na kuzama kwenye tope kutokana na ukame.
“Hali ni mbaya sana ya Ukame kutokana na mabadiliko ya tabia nchi tumeanza kupata kesi za wanyama kufa , wengine kuzama kwenye tope wakitafuta maji na wengine kuingia vijijini”amesema.
Mwaise amesema,wanyamapori katika vijiji 10 ambavyo vinaunda jumuiya hiyo ya uhifadhi ambayo ipo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara,wameanza kuingiza mitaani kwenye nyumba za watu kunyang’anyana maji na watoto.
Alisema wanaomba Usaidizi wa wadau kukabiliana na changamoto ikiwepo kuchimba Maji.
Mwenyekiti mstaafu wa Serikali ya Kijiji cha Vilima vitatu,Erasto Belela alisema athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa lakini Mahusiano mazuri baina ya vijiji na mwekezaji EBN imesaidia kupunguza athari.
“Uzalishaji chakula umepungua sana lakini kupitia Utalii walau vijana zaidi 120 wameajiriwa kwa mwekezaji ,tumesaidia kujengewa shule ,kupata maji na kupata mgao wa fedha za maendeleo”alisema.
Amesema kama sio wawekezaji hao hali ya maisha katika vijiji 10 vinavyounda WMA ya Burunge ingekuwa ngumu kiuchumi.