Watoto sita wa familia moja ya Kampala wamepata maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, wamesema maafisa katika mji mkuu Kampala.
Kwa wiki nne madaktari wamekuwa wakitoa wito wa hatua kali za kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi mjini Kampala.
Virusi vya Ebola vinaweza kusambaa haraka katika maeneo yanayokaliwa na watu wengi na aina hii ya Ebola- inayoitwa Ebola ya Sudan – haina chanjo.
Mapema mwezi huu wilaya ambazo zimeathirika zaidi na mlipuko, Mubende na Kassanda ziliwekwa katika karantini.
Watoto hao sita ndugu wa familia moja walipata maambukizi baada ya ndugu yao aliyetoka katika moja ya wilaya zilizoathiriwa zaidi kuja kuishi nao, na baadaye kufariki, wamethibitisha maafisa wa afya.
Tangu mlipuko ulipoanza Septemba, wizara ya afya ya Uganda imerekodi visa 109 na vifo 30. Kufikia Jumatatu, vifo 15 kati ya hivyo vilitokea mjini Kampala.
Baadhi wanahofia kuwa Rais Yoweri Museveni alichelewa kushughulikia hatua za tahathari za mapema zilizotolewa na wahudumu wa afya kuhusu virusi hivyo vya homa inayosababisha kuvuja kwa damu.
Waziri wa Afya Jane Ruth Aceng alisema anahofu kubwa kuhusu kusambaa kwa virusi katika maeneo ya mijini, ambako kuna idadi kubwa ya watu.
Watoto hao ndugu sita waliopatikana na Ebola katika mji mkuu hawajatajwa majina yao wala umri wao haujafichuliwa, ili kulinda utambulisho wao.Lakini tunafahamu kuwa shule wanakosoma watoto hawa bado haijafungwa.
Dkt. Aceng amesema wahudumu wa afya sita ambao walipata maambukizi baada ya kuwatibu wagonjwa pia ni miongoni mwa wale waliofariki hivi karibuni.