Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuwezesha upatikanaji wa wataalam, dawa, vitendanishi na vifaa tiba.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Oktoba 26, 2022 baada ya kushuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Ushirikiano baina ya Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) na Serikali ya Jimbo la Chungcheongbuck nchini Korea kusini.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, ambalo pia lilihudhuriwa na Gavana wa jimbo la Chungcheongbuck, Mheshimiwa Majaliwa amesema “Tukio hili la utiaji saini wa makubaliano haya ni ishara kwamba sasa tunakwenda kuimarika kwenye sekta ya dawa, mkataba huu kwetu ni muhimu kwa kuwa tunahitaji kujiimarisha katika eneo la upatikanaji wa dawa na tafiti.”
Sehemu ya makubaliano katika mkataba huo ni kujadili na kuendeleza mahusiano ya kibiashara katika nyanja za masoko ya bidhaa zinazozalishwa na Makampuni ya dawa katika jimbo hilo.
Maeneo mengine ni kubadilishana watumishi, semina za pamoja za wataalamu wao katika nyanja mbalimbali, kubadilishana na kupeana taarifa za uwekezaji kwenye sekta ya dawa, msaada wa kitaalamu na wataalam.
Mheshimiwa Majaliwa alimueleza Gavana huyo kuwa, kutokana na mpango wa Serikali wa kuendelea kuimarisha eneo la utoaji huduma za afya, Serikali ya Tanzania inawakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kuwezesha upatikanaji rahisi wa dawa na vifaa tiba.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa MSD, Tukai Mavere amesema kuwa mkataba huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uwezo wa MSD katika utoaji wa huduma na kupata utaalam wa kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo. “Tanzania tumeendelea kuagiza dawa na vifaa tiba kutoka hapa Korea Kusini”.
“Korea ina sifa kubwa ya ubora wa bidhaa na teknolojia, MSD tupo kwenye mabadiliko na tutayaelekeza katika teknolojia, uzalishaji na kuagiza bidhaa bora na kwa bei nzuri, tayari tunabidhaa zaidi ya 57 kutoka Korea Kusini.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea kituo cha KBio Health ambacho kinajishughulisha na utengenezaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba kilichopo katika mji wa Chungbuk, Korea Kusini.
Pia,Majaliwa alitembelea eneo jipya la mji wa Serikali, lililopo Sejong nchini Korea Kusini.