Tulipoandika namna bora na taratibu maalum za kufuata unapotaka kununua ardhi, tulisema pia kuwa taratibu za ununuzi wa ardhi huwa zinatofautiana kutegemeana na  mazingira ya kila ardhi.

Tukasema unaponunua ardhi kwa msimamizi wa mirathi ni tofauti na unaponunua kwa mmiliki mwenyewe. Unaponunua ardhi ya familia ni tofauti na unaponunua ardhi isiyo ya familia.

Vilevile, unaponunua ardhi ya kijiji ni tofauti na unaponunua ardhi isiyo ya kijiji. Taratibu hutofautiana na hasa tofauti ipo katika nyaraka ambazo zinatakiwa kuambatanishwa ikiwa kama ithibati ya ununuzi.

Hata uandishi wa mkataba wa manunuzi pia nao huwa na tofauti katika hili.

 

1. Ardhi ya kijiji kwa uwekezaji

Wako watu wamekuwa wakinunua ardhi hasa huko vijijini, lakini baadaye wamekuwa wakijikuta katika migogoro mikubwa na wenyeji. Mwamko wa kununua maeneo kama Bagamoyo, Kisarawe, Chanika, Dondwe na maeneo mengine umekuwa mkubwa sana.

Hata hivyo, mwamko unavyoongezeka ndivyo na migogoro inavyoongezeka. Kubwa katika migogoro hii ni hatua ya wanunuzi kutokufuata utaratibu wa ununuzi aidha kwa kujua, kutokujua au kupotoshwa.

Wakati mwingine ni uelewa mdogo miongoni mwa wenyeji, lakini zaidi ni hili la kutofuata utaratibu. Mara zote huwa tunasema ni bora zaidi mgogoro unapotokea halafu ukukute ulifuata taratibu wakati wa ununuzi.

Bila shaka hautakuwa na athari kubwa kwako, lakini ni mbaya zaidi ukitokea halafu ukukute kuna taratibu hukufuata kwa bahati mbaya au bila kujua, huwa unakuwa katika hatari ya kupoteza.

Unapokwenda kununua ardhi ya kijiji kwa sababu yoyote ile hasa uwekezaji, upo utaratibu maalum wa kufuata nitakaoeleza.

 

2.  Ardhi ya kijiji ni nini?

Ardhi ya kijiji ni ile ardhi iliyopo katika mipaka ya kijiji fulani iliyoainishwa na mamlaka za wilaya husika, huku ikiwa na hati ya usajili wa kijiji. Ardhi hii hulindwa kwa taratibu za kimila za eneo husika ikiwa ni pamoja na Sheria namba 4 ya 1999.

 

3. Utaratibu wa kununua ardhi ya kijiji kisheria

(a) Maombi maalum huandaliwa na kuwasilishwa kwa mtendaji wa kijiji ambaye hupatikana katika kila kijiji.

(b) Maombi huandaliwa katika fomu maalum ambazo hupatikana katika kila ofisi za kijiji. Si maombi ambayo huandaliwa kama barua za kawaida za maombi.

(c) Ikiwa mwombaji ni mtu mmoja, basi atasaini sehemu maalum na ikiwa ni maombi kwa niaba ya  familiia basi watu wawili kutoka ile familia watasaini na ikiwa ni ardhi kwa ajili ya kikundi pia wawakilishi wasiopungua wawili kutoka kile kikundi watasaini kwa niaba ya wengine.

(d) Kama mwombaji ni chama cha ushirika au kampuni, basi inatakiwa kuwapo wadhamini wawili kwa ajili ya shirika au kampuni hiyo. Wanaweza kuwa zaidi ya wawili, lakini wasipungue.

(e) Kama anayeomba ardhi si mwenyeji wa eneo husika basi atatakiwa kuwa na wadhamini wasiopungua watano ambao ni wenyeji wa eneo hilo. Sharti ni kuwa kati ya hao wadhamini wasiwepo ndugu wa mwombaji.

(f) Mwombaji atatakiwa kuambatanisha katika maombi yake tamko linaloonesha ardhi nyingine anayoimiliki Tanzania nje na hiyo anayoomba.

(g) Ikiwa ardhi inaombwa kwa ajili ya makazi basi mwombaji atatakiwa kuambatanisha tamko linaloonesha kuwa ataanza ujenzi wa makazi hayo ndani ya miezi mitatu tangu siku ya kuidhinishiwa ardhi. 

(h) Ikiwa mauzo ni heka 50 au kuendelea, ni lazima yaidhinishwe na mkutano mkuu wa kijiji.

(i) Baada ya kukamilisha taratibu hizo, halmashauri ya kijiji itakaa vikao na ndani ya siku 90 itatakiwa kutoa majibu.

Kamwe usikubali kuuziwa ardhi ya kijiji na viongozi wa kijiji bila kufuata utaratibu huu. Hii hasa ni kwa wawekezaji wanaochukua maeneo makubwa kwa shughuli za kiuchumi.

 

Kuhusu sheria  za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea Sheria Yakub Blog.