Na Robert Hokororo,JamhuriMedia

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama ameonesha kutoridhishwa na usimamizi wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula unaotekelezwa katika Halmashauri ya Nzega mkoani Tabora.

Pia ameshangazwa na namna utekelezaji wa mradi huo unavyosuasua pamoja na kuwa tayari fedha zimeshatolewa na Serikali kwa Halmashauri za wilaya zinazotekeleza miradi hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama (kulia) akikagua ujenzi wa ghala la kusaga nafaka linalojengwa kupitia Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo
yenye Ukame nchini (LDFS) lakini mkandarasi ameshindwa kutimiza masharti ya makaba, alipofanya ziara ya kukagua mradi huo wilayani Nzega mkoani Tabora humo.

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo Ukame nchini (LDFS) wilayani Nzega mkoani Tabora.

Ameshangazwa na namna wilaya inavyotekeleza miradi ya Serikali kwa ubaguzi kwa kutoipatia kipaumbele miradi ya mazingira kama inavyofanya kwa miradi mingine katika wilaya hiyo.

“Matumizi ya fedha katika mradi huu hayaridhishi hata kidogo, kwa mwaka 2022/23 Nzega mmetengewa shilingi bilioni 2.3 na kati ya hizo milioni 467.6 zipo kwenye akaunti bado hazijatumika na mpaka Desemba zinatakiwa ziwe zimetumika hali hii hairidhishi hata kidogo,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akizungumza na viongozi kutoka Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo yenye Ukame nchini (LDFS).

Akiwa ziarani katika Wilaya ya Nzega baada ya kukuta mradi wa ujenzi wa ghala kwa ajili ya kukoboa mpunga unasuasua aliutaka uongozi wa Halmashauri kujitathmini kuhusu utendaji wake na kutoa siku saba wa kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa kazi hiyo.

Katika eneo hilo la ujenzi mkandarasi huyo anatajwa kutofanya kazi yake inavyotakiwa ambapo mpaka sasa amechimba msingi pekee wakati Mkataba wake wa mwezi mmoja ulianza tarehe 1 Oktoba, 2022 na unategemea kukamilika 30 Oktoba, 2022.

“Haiwezekani katika miezi miwili ya mkataba mkandarasi ana siku 23 hajafanya kazi yoyote lakini halmashauri iko kimya, mkurugenzi yuko kimya, mratibu wa mradi wa wilaya yuko kimya hamchukui hatua,” amesema.

Kutokana na hali hiyo ameelekeza kusitishwa kwa mkataba dhidi ya mkandarasi huyo kwani ameshindwa kutekeleza majukumu yake na kuusimamia mkataba wake na halmashauri.

Ameitaka menejimenti ya halmashauri pamoja kujitathmini katika nafasi zao na kumuondoa mara moja mratibu wa mradi wa wilaya kwakuwa ameshindwa kusimamia mradi huo.

Aidha, katika hatua nyingine alimtaka Mkurugenzi wa halmashauri kumchukulia hatua Afisa Manunuzi kwa kufanya mchakato wa kununua mashine ya kukoboa mpunga kupitia mradi huo ambayo inadaiwa kutokidhi viwango na kutoendana na bei halisi.

Naibu Katibu Mkuu Mkama alisema mashine hiyo inaoekana imetajwa kununuliwa kwa sh.milioni 50 tofauti na viwango na kuelekeza Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani wa Serikali ishirikishwe na kupewa kazi ya kuikagua kujua kama nakidhi viwango.

Kwa upande Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega Bw. Evance Chambo amesema amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itasimamia kikamilifu utekelezaji.

Amesema atamuelekeza mratibu wa mradi wa wilaya awe anatoa taarifa za utekelezaji kila wiki ili kuhakikisha unatekelezwa kama ulivyopanga kuepuka changamoto kama hizo.

Mtambo wa kuchimba visima virefu ukiendelea na kazi katika kijiji cha Bulende ambako katika Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama alipofanya ziara ya kukagua shughuli hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo yenye Ukame nchini (LDFS) lakini mkandarasi ameshindwa kutimiza masharti ya makaba, alipofanya ziara ya kukagua mradi huo wilayani Nzega mkoani Tabora humo.

Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo ametembelea miradi mingine ikiwemo uchimbaji wa visima virefu vya maji katika kijiji cha Bulende na Bulambukana mradi wa ufugaji nyuki katika kijiji cha Lyamalangwa ambapo amepongeza wanakikundi hao kuonesha hamasa katika ufugaji.

Dkt. Mkama na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais amefanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa LDFS katika wilaya za Magu (Mwanza), Nzega (Tabora) na Mkalama (Singida) ambapo ametoa maelekezo baada ya kukutana na changamoto mbalimbali.