Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuripoti kwa umakini na usahihi habari mbalimbali hasa zinazohusu uchaguzi ili kuipa jamii kile ambacho inachostahili.
Ili kuviwezesha vyombo hivyo vya habari kufanya kazi yake ipasavyo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na BBC Media Action liliandaa warsha kwa lengo la kuwawezesha wana habari hao kutoka vyombo mbalimbali vya habari kuweza kujifunza namna ya kuripoti habari hizo kwa usahihi.
Vivyo hivyo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) chini ya Uratibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilifanya warsha ya siku mbili iliyokuwa na lengo la kuwawezesha waandishi wa habari kujifunza kwa kina namna ya kuripoti kwa usahihi habari za uchaguzi.
Mwezeshaji wa warsha ya MCT iliyofanyia jijini Dar es Salaam, Kiondo Mshana anasema waandishi wa habari wana wajibu wa kuepuka kupokea rushwa hasa wakati wa kampeni, vitisho, upendeleo wa kuripoti habari za vyama fulani na kuelemea vingine bali wana wajibu wa kuripoti habari za uchaguzi kwa kuzingatia usawa bila kubagua vyama.
“Wakati wa kampeni waandishi wa habari wana wajibu wa kutopendelea vyama vya siasa kwa kuegemea kuripoti habari za chama fulani na kuacha wagombea wengine wakishindwa kuripotiwa habari zao,” anasema Kiondo Mshana na kuongeza wakati wa kampeni wagombea wanatakiwa kuwa huru kunadi sera zao pamoja na kuendesha mikutano yao bila kuingiliwa.
“Naona uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na wa miaka mingine, uchaguzi wa safari hii naona watu wameamka vilivyo hivyo tutarajie kuona mengi wakati wa uchaguzi wa mwaka huu,” anasema Mshana.
Naye Mwezeshaji mwingine wa warsha hiyo ya MCT, Atilio Tagalile anasema waandishi wa habari wana wajibu wa kusoma Sheria ya Uchaguzi na kuielewa kabla ya kuiripoti kwa umma kwani ikiwa watairipoti kabla ya kuisoma ipasavyo wanaweza kuongeza au kupunguza makali.
Mambo ya kuzingatia
Kwa mujibu wa Tagalile, wanahabari wanapaswa kufuatilia kwa karibu kura zilizohesabiwa vituoni kuanzia mwanzo wa upigaji kura hadi siku matokeo yanapotangazwa kama njia ya kuiwezesha jamii kupata habari zauchaguzi kwa usahihi na kwa wakati.
Pia wanatakiwa kuzijua sheria za uchaguzi, pia waepuke ushabiki kutoa hitimisho wakati wa kuripoti habari hizo hasa wanapogundua chama fulani kimeshinda. Mengine ya kuzingatia ni kuepuka kuandika habari za uchochezi.
Kwa mujibu wa Ripoti iliyoandaliwa na MCT kuhusu namna ya kuripoti habari za uchaguzi iliyotolewa Machi, mwaka huu, vyombo vya habari vina wajibu pia wa kulinda taaluma yao kwa kuepuka kupokea zawadi mbalimbali kama vile fedha, kutumiwa tiketi, kulipiwa ada ili kuripoti habari kutoka kwa wagombea au watu wanaowawezesha kupata fedha hizo.
Kuhusu matangazo; wana habari wana wajibu pia wa kuepuka kutangaza kwa ushabiki kwenye vyombo vyao habari kuhusu wagombea kwa kuelemea upande mmoja kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara katika jamii.
Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda, ambaye alikuwa mtoa mada katika warsha ya wanahabari kuhusu kuripoti habari za uchaguzi iliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani, anasema anauona uchaguzi wa mwaka huu kuwa na changamoto nyingi kuliko chaguzi nyingine zilizopita.
“Viashiria vya hali hiyo vimejitokeza hivi karibuni hivyo sisi kama wanahabari tuna wajibu wa kujua cha kufanya hasa tunaporipoti habari hizo za uchaguzi na kikubwa tunachotakiwa kufanya ni kuzingatia maadili na miiko ya taaluma yetu vya Uandishi wa habari.
“Tutakuwa watu wa ajabu tukiripoti habari za uchaguzi bila kujua idadi ya wagombea, kilichotokea katika chaguzi zilizopita nakadhalika. Cha msingi tunachopaswa kuzingatia ni kuepuka ushabiki bali kunatakiwa kuripoti kwa usahihi habari za uchaguzi,”anaeleza Kibanda,
Kibanda ambaye pia ni Mhariti Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) anasisistiza kwamba vitendo vya ushabiki visipewe nafasi wakati wa kutipoti habari za uchaguzi pia wana habari wana wajibu wa kuwa makini wakati wa kufanya kazi zao ili kuepuka kutekwa au kufanyiwa vitu vingine vibaya.
Naye Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Jamhuri Media Limited, ambayo ni wachapishaji wa gazeti la JAMHURI, Deodatus Balile, anasema vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa ujumbe wake kwa usahihi kwa jamii na si vinginevyo.
Balile ambaye alikuwa miongoni mwa watoa mada wakati wa warsha hiyo, anasema taaluma ya uandishi wa habari ni moja kati ya taaluma nyeti nchini na kwa msingi huo ina wajibu wa kuepuka kuandika habari za uchaguzi kwa ushabiki.
Ametoa rai kwa wana habari kuepuka kupokea zawadi, kuwalinda watoa habari hasa wanaoapatia habari nyeti zinazoweza kuhatarisha.
Naye, Frank Sanga ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la MWANANCHI, anasema vyombo vya habari vina wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha, kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote inaporipoti habari za uchaguzi.
“Tuna wajibu pia wa kuhakikisha tunaripoti issues kwani sio kila kinachoongelewa ni habari, pia tuepuke kupendelea baadhi ya vyama na kuviacha vingine vikikosa kuandikwa bali tuandike habari zetu za uchaguzi kwa usawa,” anasema Sanga.
Vivyo hivyo, Sanga anatoa rai kwa wana habari kuandika habari zinazohusu tuhuma mbalimbali za wagombea kwa kutoegemea upande mmoja. “Ikiwa tunapata habari za tuhuma tusiandike bila ku balance upande unaotuhumiwa,”anasema Sanga.
Anawaasa wana habari kuepuka kutembea peke yao bali wjumuike na wenzao ili endapo litatokea tatizo iwe rahisi kujulikana na kusaidiwa kwa urahisi.
[email protected] au 0785 438 478.