Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ikiwa ni pamoja na kuzifanyia maboresho baadhi ya sheria za usimamizi wa biashara ili kuongeza ufanisi kwa sekta binafsi katika uzalishaji.
Dkt. Stergomena ametoa kauli hiyo jijini Lisbon wakati akifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililoloandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ureno na Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Ureno na kuishirikisha Jumuiya yaWafanyabiashara wa Ureno.
Dkt.Tax amesema dhamira kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara hususan kwa kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi.
Amesema tayari Serikali imefanya majadiliano ya mara kwa mara na sekta biafsi ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Amesema katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini masuala mbalimbali yanaboreshwa zikiwemo huduma, sheria, miundombinu pamoja na kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi ambayo ni muhimu katika kuchangia uchumi wa nchini.
“Tupo hapa leo ili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji. Tanzania inaendelea kuhamasisha uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji.
“Katika maboresho hayo ni pamoja na Serikali kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuiwezesha sekta hii kuwa na
ufanisi na kuchangia uchumi ipasavyo” amesema Dkt. Tax.
Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama barabara, bandari, reli, viwanja vya ndege na upatikanaji wa maji na umeme ili kuwawezesha wawekezaji kutopata changamoto zozote pale wanapokuja nchini kuwekeza.
“Serikali imefanya jitihada za makusudi za kuhakikisha miundombinu yote ya msingi kama maji, umeme, barabara, reli,usafiri wa anga na mawasiliano ya simu vinapatikana kwa ngazi tofauti tofauti.
Kupitia maboresho haya ni imani yetu wawekezeji watapata ujasiri wa kuwekeza Tanzania na si mahali pengine popote”, amesisitiza Dkt. Tax.
Amesema masuala mengine yanayohamasisha uwekezaji, biashara na utalii nchini ni pamoja na ushiriki wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Filamu ya kutangaza Utalii nchini ya The Royal Tour, Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi ambayo imekuwa chachu katika kuwajengea ujasiri wawekezaji nchini pamoja na ushiriki wa Tanzania kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa ya biashara na uwekezaji kama Maonesho ya Biashara ya Dubai ya mwaka 2020. Vyote hivi vimeipaisha zaidi Tanzania duniani na kuchangia ongezeko la watalii na wawekezaji nchini.
Dkt.Tax alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji na wananchi wa Ureno kwa ujumla kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii huku akiwahamasisha kuangalia Filamu ya Utalii ya Royal Tour ambayo ameilezea kuwa ni ya aina yake kwani mhusika mkuu katika Filamu hiyo ni Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Waziri anayeshughulikia Biashara na Uwekezaji wa Ureno,Bernardo Ivo Cruz amepongeza ziara ya Mhe. Dkt. Tax nchini humo akisema imekuja wakati mwafaka ambao wakati dunia ikiendelea kushuhudia changamoto mbalimbali za kiuchumi, Tanzania na Ureno zinaangalia namna ya kushirikiana katika biashara na uwekezaji ili kujikwamua kiuchumi.
“Tanzania ni mshirika wetu muhimu katika biashara na uwekezaji na tupo tayari kuimarisha ushirikiano huu. Nakupongeza Mhe. Waziri kwa kufanya ziara katika kipindi hiki na tunaahidi kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo Kilimobiashara, Uchumi wa Bluu, Miundombinu na Sekta zingine za
uwekezaji” amesema Cruz.
Pia ameongeza kusema nchi yake inao Mpango wa miaka sita wa ushirikiano katika biashara na uwekezaji kuanzia mwaka 2021-2027 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na mpango huo.
Akiwasilisha mada kuhusu Fursa za Uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa hilo,Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),Bw. Revocatus Rasheli amewahamasisha wawekezaji na wafanyabiasha kutoka Ureno
kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini huku akisema tayari anayo mkononi miradi 100 chini ya Sekta ya Umma na miradi 36 chini ya Sekta Binafsi ambayo ipo tayari na kwamba ni kiasi cha wawekezaji hao kuchagua na kuwekeza.
Aliongeza kusema Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji imetenga ardhi yenye ukubwa wa Hekta milioni 1.6 kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo ambapo tayari Hekta 6,000 zipo mkoani Morogoro kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.