Septemba 2, mwaka huu maiti ya  Aylan Kurdi,  mtoto wa Kisiria wa miaka mitatu, iliokotwa katika ufukwe wa bahari ya Mediterania. Alizama pamoja na ndugu yake Galip wa miaka mitano na mama yao wakati wakijaribu kuvuka kutoka Uturuki kuelekea Ugiriki.

Picha na habari za mtoto huyo zilienea kwa haraka katika vyombo vya habari na mtandao kote duniani. Waliokuwa wamesahau au wanajaribu kusahau wakalazimika kukumbuka kuwa kuna tatizo kubwa la wakimbizi kutoka Syria na kwengineko wanaojaribu kuokoa maisha yao kwa kuingia Ulaya.

Kwani baada ya mashambulizi ya Syria yaliyodumu zaidi ya miaka minne, mamilioni ya wananchi wake wamegeuka wakimbizi ndani na nje ya nchi yao. Idadi hii haijawahi kuonekana duniani tangu vita kuu ya pili.

Picha za mtoto Aylan zilienezwa katika mtandao na mtoto huyo akazungumzwa sana katika vyombo vya habari.  Lakini ni wachache walielezwa kuwa kabla ya kufa kwa mtoto huyo wakimbizi 71 walikufa kwa kukosa hewa wakiwa wamefungiwa katika lori lililokuwa linawasafirisha hadi Austria. Habari hii haikupewa uzito.

Pia tangu mwanzo wa mwaka 2014 tayari wakimbizi zaidi ya 5,000 wamepoteza maisha yao wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kutoka Libya kuelekea Italia. 

Zaidi ya Wasiria milioni nne wamekimbilia nchi za jirani, wakiishi katika kambi nchini Ururuki, Lebanon, Jordan, Iraq na Misri.  Wengine milioni nne wameyaacha makazi yao na wamebaki ndani ya nchi. Hii ni Syria ilivyo leo, nchi ndogo yenye wakazi  milioni 17, nchi ambayo kwa karne nyingi imekuwa ikiwapokea wakimbizi kutoka nje. 

Bila shaka nchi za Kiarabu zimefurika na zinashindwa kuwahudumia idadi kubwa ya wakimbizi. Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi (UNHCR) nalo limeelemewa. Halina chakula cha kutosha kuwalisha. Kila mkimbizi anapewa chakula cha nusu dola kwa siku, lakini wengi wanakosa hata hicho kiduchu. 

Matokeo yake wako tayari kufa wakivuka bahari kuelekea Ulaya. Kifo cha mtoto Aylan kwa hiyo ni moja kati ya maelfu waliopoteza maisha yao wakivuka kutoka Uturuki au kutoka Libya.

Kwa mujibu wa UNHCR, inakisiwa kuwa takriban wakimbizi 366,400 wamevuka bahari ya Mediteranea na kuingia Ulaya. Kati yao 2,800 wamepoteza maisha yao. Waliobaki wameingia nchini Ugiriki na wamekuwa wakitembea kwa miguu zaidi ya kilometa 110 kupitia Macedonia, Serbia, Hungary hadi Austria. Wengi wao ni wanawake na watoto.

Wakiingia Austria wenyeji wanawapokea kwa kuwapa chakula na maji. Hali yao huwa afueni wanapowasili Austria. Hata hivyo wengi wao lengo lao ni kuelekea Ujerumani ambako kuna ndugu na jamaa zao. 

Licha ya Wasiria, idadi kubwa ya wakimbizi wamekuwa wakiingia Ulaya kutoka nchi za Kiarabu,  Afrika na Asia. Wanavuka bahari kutoka Libya au Uturuki hadi Ugiriki na Italia. Kutoka huko wanaelekea nchi za Ulaya magharibi kwa kupitia nchi za Ulaya mashariki.

Kuna wanaotoa hoja kuwa hawa si wakimbizi bali ni wahamiaji wa kiuchumi, ni watu wanaotaka kuzihama nchi zao ili kutafuta maisha bora. Eti ni vizuri warejeshwe walikotoka kwa sababu hawana sifa za kuwa wakimbizi. 

Kisheria mkimbizi ni yule ambaye anaondoka nchini mwake ili kuepukana na kukamatwa, kuteswa au kuuawa kwa sababu za kisiasa, kidini au kikabila. Tofauti na yule anayekimbia ili kuepukana na maisha magumu au umasikini.

Sasa katika hali ya kivita kama ile ya Syria au Iraq au Libya au Afghanistan ni vigumu kuanza kumchunguza kila mmoja katika halaiki ya watu wanaokimbia. Inatosha kusema kuwa yule anayekimbia kwa sababu ya vita si tofauti ya yule anayesakwa kwa sababu ya dini au kabila lake.

Si wote wanaoelewa hivyo. Ndio maana kuna watu kama Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ambaye ametumia neno la kejeli kama ‘kundi la nzige’ (swarms) ili kuwaelezea maelfu ya wakimbizi wanaojaribu kuingia Ulaya. Naye Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper anasema wengi kati yao ni magaidi wa Al Qaeda au ISIS (Daesh).

Hata hivyo, Ujerumani imesema iko tayari kuwapokea jumla ya wakimbizi wapatao 800,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu. Pia itawapokea milioni moja mwaka 2016 na 2017 Hii ni nchi ya peke katika Umoja wa Ulaya (EU) ambayo imetenga dola Bilioni 6.68 kuwagharamia wakimbizi hao. 

Nchi mbili katika bara la Ulaya zinapaswa zipongezwe kwa ukarimu wao, nazo ni Ujerumani na Sweden. Katika mtandao tunaona wananchi wakijitokeza kuwakaribisha wakimbizi. Kamati za maandalizi zimeundwa ili kuwapokea wanapowasili.

Nchi nyingine ambazo zimeahidi kuwapokea wakimbizi ni Austria, Norway, Finland na Iceland. Denmark imekataa katukatu. Uingereza na Ufaransa zilikataa, lakini zikakubali kupokea wachache. Uingereza imetangaza kuwachukua wakimbizi 10,000 wakati Ufaransa itawapokea 24,000 “katika kipindi cha miaka miwili ijayo”. Canada imesema itawachukua 10,000 katika muda huohuo, lakini baada ya kuwachunguza. 

Rais wa Umoja wa Ulaya (EU), Jean-Claude Juncker amesema nchi nyingi za Ulaya zimekataa kushiriki katika mpango wa kuwapokea wakimbizi. Amesema umoja huu wa nchi 28 umekosa umoja. Alizikumbusha nchi hizo kuwa wakati mmoja katika historia ni Ulaya ndiyo iliyotoa wakimbizi wengi zaidi ya Syria leo.

Juncker amesema haya baada ya polisi kuwashambulia wakimbizi 25,000 katika kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos. Wakimbizi hao walifikia kutoka Uturuki wakiwa njiani kuelekea Ulaya magharibi. Hasira zilipanda baada ya wakimbizi hao kusubiri zaidi ya wiki mbili bila ya kupata usafiri kama walivyoahidiwa.

Pia nchini Hungary serikali ya mrengo wa kulia ilitoa amri kwa majeshi kujenga uzio wa chuma mpakani ili kuzuia wakimbizi wasiingie. Serikali ikayakamata magari yaliyokuwa yakiwasafirisha wakimbizi kutoka Hungary na kuwaingiza Austria. Hata hivyo serikali haikufanikiwa, kwani wanaharakati wakatangaza katika mtandao na wakafanikiwa kukusanya magari zaidi ya 200 na wakawavusha wakimbizi kutoka mpaka wa Hungary.

Kati ya wanaharakati hao ni Erzsebet Szabo kutoka Austria. Yeye alisema amesaidia kuwavusha wakimbizi kama 380. Alipoulizwa kama haogopi kukamatwa na polisi alijibu “Hata kama watanikamata mateso nitakayopata hayafanani na yale wanayoyapata hawa wakimbizi.”

Kwa upande wa pili kuna kikundi cha kikaburu nchini  Uingereza (UKIP) ambacho kimetamka kuwa nchi hiyo haipaswi kuwapokea Wasiria walio Waislamu, bali iwachukue wale walio Wakristo tu. Hawa wanataka kuwagawa wakimbizi kwa msingi wa dini zao. Labda baada ya hapo watawabagua kwa madhehebu yao – hawa ni Waprotestanti na hawa Wakatoliki.  

Pia katika kambi za wakimbizi nchini Ujerumani kumekuwepo na mashambulizi zaidi ya 340 tangu mapema mwaka huu. Haya ni mashambulizi yaliyoripotiwa polisi na yalifanywa na makundi ya wabaguzi wanaopinga wageni kwa misingi ya ukabila na rangi.

Mashambulizi haya ni pamoja na matusi na kashfa za mdomo na za kuandika, kuchomwa moto kambi na kuwapiga wakimbizi binafsi. Wakimbizi 38 wameshambuliwa mwaka huu na 28 mwaka jana. Polisi imeripoti kuwa nyumba moja walimokuwa wakiishi wakimbizi ilichomwa moto mjini Rottenburg am Neckar. Watu watano walijeruhiwa kutokana na moto. Wawili waliumia baada ya kuruka kutoka ghorofani. Nyumba hiyo haikaliki tena.

Tunapozungumzia wakimbizi kutoka Syria ni vizuri tukajiuliza chanzo chake ni nini. 

Marekani na wenzake wa NATO wamekuwa wakiishambulia Syria kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad, sawa na walivyofanya huko Libya ambako walimuua Kanali Gaddafy. Baada ya kuuawa kwa Gaddafy hali imezidi kuwa mbaya, pamoja na nchi kutekwa na majeshi ya mujahidina ambao sasa wamekuwa maadui wakubwa wa magharibi. 

Lakini watawala wa NATO hawataki kujiuliza suali la msingi: je baada ya kumuondoa Assad ndio iweje? Hao vibaraka wa magharibi waliopewa fedha na silaha hawaonekani. Hivi sasa sehemu kubwa ya nchi inadhibitiwa na mujahidina waliosimamisha Khilafa (ISIS au Daesh), nao wamekuwa wakiwachinja raia wa magharibi. Je hawa watayeyuka hewani baada ya kuondoshwa kwa Assad? Matokeo yake ni kusababisha Libya ya pili.

Vyombo vya habari vinapozungumzia hili wimbi la wakimbizi vinakuwa vyepesi kuwalaumu hawa Daesh au kumlaumu Assad kuwa ndio chanzo. Hatusikii Marekani ikilaumiwa kwa mashambulizi yake ya kijeshi yaliyochochea balaa hili. 

Wametumia kisingizio cha kupigana na udikteta wa Assad kwa ajili ya maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi. Huu ni mkakati wa mataifa ya magharibi uliokuwepo kwa muda mrefu  

Tangu kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti (USSR) mwaka 1991mataifa haya yaliamua kutumia nguvu za kijeshi ili kueneza himaya zao katika Ulaya mashariki, nchi za Kiarabu, bara la  Afrika na kwengineko. 

Wameshambulia Afghanistan wakidai wanapigana na ugaidi kisha wakaishambulia Iraq kwa udanganyifu kuwa Saddam alikuwa na silaha za maangamizi. Matokeo yake ni kuangamiza jamii na kuwaua maelfu na maelfu ya wananchi, wakiwemo watoto na wanawake. Leo wanajifanya eti wanaomboleza kifo cha mtoto Ailan Kurdi.

Wakaishambulia Libya na kumuua kikatili Muammar Gaddafi. Nchi za magharibi zilishangilia wakati hata maiti ya Gaddafi ilipodhalilishwa. Leo Libya imesambaratika na matokeo yake ni maelfu ya wakimbizi. Imekuwa ni njia ya wakimbizi kutoka  Afrika na kwengineko kusafiri hadi Ulaya, wengi wao wakizama na kufa baharini.

Halafu wakaishambulia Syria ili kumpindua Assad. Mamilioni ya dola na silaha zikaingia nchini ili kuchochea vita. Matokeo yake ni kuzuka kwa majeshi ya ISIS na mamilioni ya wananchi wakikimbilia nchi za jirani.

Yote haya ni uhalifu wa sharia ya kimataifa. Waliosababisha madhambi haya walitakiwa wafikishwe katika mahakama ya kimataifa. Hawa ni kina Bush, Cheney, Rumsfeld na Blair ambao leo wanatamba ulimwenguni wakati watawala wa Kiafrika kama Charles Taylor (Liberia), Laurent Gbagbo (Côte d’Ivoire)  na Hissène Habré (Chad) ndio wanaokamatwa na kufikishwa mahakamani.

 

+1 613 6992933 

[email protected]