Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati nchini na kwamba hakuna mradi wowote utakaokwama.
Amesema hayo leo Oktoba 16, 2022 wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Daraja la Magufuli (Kigongo-Busisi) ambao umefikia asilimia 53.66 na Reli ya Kisasa (SGR) wakati wa ziara ya kikazi mkoani Mwanza.
“Wale wenye mashaka kuhusu miradi hii, niwahakikishie hakuna mradi utakaokwama, miradi yote iliyoanzishwa na Serikali yenu ya Chama cha Mapinduzi itakuwa endelevu na itakamilika, miradi hii yote inalenga kuwanufaisha Watanzania na Rais Samia anaiendeleza miradi yote.”
Amesema kuwa ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati, Serikali imeendelea kuhakikisha hakuna mkandarasi yoyote atakayecheleweshewa malipo pindi anapotoa hati ya madai.
Aidha,Majaliwa amewataka wakazi wanaoishi maeneo yanayozunguka miradi hiyo watumie fursa hiyo kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowaletea maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za kulala wageni.
Aidha,Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha anaimarisha ulinzi katika maeneo yote yanayotekelezwa miradi ili kuzuia vitendo vya wizi wa vifaa mbalimbali ikiwemo saruji na nondo.
Aliongeza kuwa Watanzania waliopata ajira kwenye miradi hiyo wahakikishe wanakuwa mahiri kwenye maeneo wanayofanya kazi. “Kama wewe unakunja nondo hakikisha unakuwa mahiri kwenye eneo hilo, kama wewe unaendesha mitambo hakikisha unakuwa mahiri, tunataka muwe mafundi mahiri kwenye kila eneo ili tunapoanza miradi mingine tuwe na wataalamu wakutosha.”
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa Ujenzi wa Daraja la Magufuli Abdulkarim Majuto amesema daraja hilo lenye urefu wa kilimota 3.2 litagharimu shilingi bilioni 716.333 na mpaka sasa limetoa ajira 885 kwa Watanzania.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Amina Lumuli amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa kipande cha Mwanza-Isaka ambacho kitaghrarimu shilingi trilioni 3.12 umefikia asilimia 14 hadi sasa. “Kipande hiki kitakuwa na stesheni 10 na kimeshazalisha ajira kwa Watanzania 5,400 na hadi kitakapokamilika kitatoa ajira 11,000.”