KikweteMengi yameandikwa na kusemwa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 nchini Tanzania, lakini kuna dalili za wazi kuwa huenda Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikatoka madarakani baada ya kuendesha Serikali kwa zaidi ya miongo mitano, yaani nusu karne.

Ilidhaniwa kuwa uzoefu huo wa muda mrefu madarakani ungekisaidia Chama hicho kufanya tathmini ya ufanisi wa utekelezaji wa sera zake mara kwa mara, lakini hilo halikufanyika. Matokeo yake Chama kimebweteka, na kujiaminisha kuwa kitashinda tu kila uchaguzi.

Kikatengeneza mazingira ya ulaji wa uhakika kwa wanasiasa badala ya wataalamu, matokeo yake wakajipenyeza, tena kwa pesa, hadaa na hila, viongozi walafi badala ya wale wenye uchungu, maono na uwezo wa kuwahudumia wananchi na kuinua uchumi wa nchi. Viongozi wanajijali wenyewe badala ya kuwajali wananchi.

 

Maswali mengi yasiyokuwa na majibu na wananchi wanalalamika

Yaliyofuata sasa ndiyo haya: Wananchi wanakata tamaa, uchumi wa nchi unadorora na shilingi inaporomoka kila kukicha. Huduma za afya, elimu na kujiendeleza kiuchumi kwa wananchi, hafifu. Yote haya yanatokea wakati nchi ina ardhi nzuri, maji mengi, imejaliwa madini ya aina aina, rasilimali nyingi na watu wenye ari ya kujiletea maendeleo.

Hivyo, tatizo wananchi wamekosa uongozi thabiti. Haishangazi basi hivi sasa, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, mwana-CCM akipita na sare zake katika maeneo fulani fulani anazomewa, tena na wale watu wa hali ya chini, au “wanyonge” ambao CCM imekuwa ikijinasibu kuwa ndiyo inayowatetea.

CCM imekubali Polisi wawakamate watu au, sijui kwa kuvunja sheria gani. Mkuu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova, alipotangaza amri hiyo, hakufafanua. Wanyonge hao ndio wanaojiuliza, kulikoni?

Wana maswali mengi, miongoni mwao: Mbona yale Maisha Bora, tuliyoahidiwa na Serikali hii ya Awamu ya Nne hatuyaoni tena? Mbona umasikini unazidi kutuzingira huku wakulima wanakopwa mazao yao, viwanda vimefungwa, vimefilisiwa au vimebinaifsishwa na kusababisha vijana wetu waliosoma vizuri kukosa ajira, tunauza mazao ghafi kwa bei ya kutupa badala ya kuuza yaliyoongezewa thamani viwandani yenye bei nzuri; mbona tukienda zahanati na hospitali, tunakosa dawa na tunaambiwa tukanunue kwa bei ghali kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi yaliyojengwa nje tu ya hospitali hizo?

Mbona tunachangia madawati, lakini shule nyingi watoto wetu wanakalia mawe au wanakaa chini, huku magogo na mbao vinasafirishwa nje kwa magendo ya wakubwa, walimu hawatoshi, waliopo hawana motisha, nyumba hawana, vyoo vya shule hakuna, maabara mpaka leo hazijakamilishwa na elimu inashuka? Mbona Serikali inasema uchumi wa nchi unakua kwa kasi, lakini hali ya wananchi inadidima ila tunaona tu kuwa Mheshimiwa Rais anapewa tuzo mbalimbali na sifa?

Hakuna majibu yanayotolewa ya maswali hayo na kuwaridhisha wananchi. Ukichambua, utaona malalamiko hayo ndiyo mambo ya msingi ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa Uhuru mwaka 1961 aliyataja kuwa ni Maadui Watatu ambao lazima wapigwe vita ili tuendelee: Umasikini, Ujinga na Maradhi!

 

Trilioni zinazopelekwa Halmashauri, zinakwenda wapi? Wanasiasa wananufaika, Wataalamu wanalalamika!

 Kwa hiyo mazingira yaliyojengwa na CCM ni kuwa kuna kinyang’anyiro kikubwa cha watu kukimbilia kwenye uongozi wa kisiasa kwa ajili ya ulaji wa uhakika. Kwa mfano, ukishinda kuwa Diwani, basi una hakika kuwa utapata urahisi wa kuendesha rushwa za viwanja, kuanzisha kampuni kupata zabuni za kutoa huduma mbalimbali kwenye Halmshauri ili kula fedha lukuki za maendeleo ambazo Serikali Kuu inatenga kwa kila Halmashauri kila mwaka (Mwaka huu wa 2015/2016 Serikali imetenga Sh trilioni 4.67 kwenda Halmashauri 133 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo, huduma za kiuchumi na kijamii, kutoka Sh bilioni 780 mwaka 2005/2006!); utakula rushwa ya uhakika kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wanaotaka huduma mbalimbali; utajimegea ardhi na mashamba ilimradi maisha yako yatabadilika ghafla na kuwa mazuri, kwa gharama za kuwasahau kabisa wananchi waliokupigia kura.

Ukipata nafasi ya kuwa Mbunge, basi utajiweka vizuri zaidi ili uwe Naibu Waziri au Waziri na hivyo “kuukata” na una hakika ya rushwa nono nono zaidi, kufunga mikataba ya kiwizi na wawekezaji, kupata nafasi ya kuanzisha biashara kubwa kubwa kama za usafirishaji na uchukuzi kwa malori. Hata kama hukuteuliwa kuwa Waziri au Naibu Waziri, basi Bunge kwanza litakupa mkopo wa gari la kifahari lenye thamani siyo chini ya Sh milioni 200; utapata mshahara na marupurupu mazuri, pamoja na posho ya vikao ambayo siyo chini ya Sh 200,000 kila siku; utapata posho za semina zinazofanyika mara kwa mara kila wikiendi, wakati wa vikao vya Bunge; unaweza kuzungukazunguka na Kamati za Bunge na kula posho nono nchi nzima, eti kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali; unaweza kubahatika kuwa kwenye bodi fulani ya shirika la umma au taasisi fulani na ukala posho; una hakika, kwa bahati mbaya ukipata mafua makali, utagharimiwa na Serikali hii hii isiyokuwa na dawa hospitalini, kwenda Afrika Kusini, India, Uingereza, Ujerumani au Marekani kwa matibabu ya uhakika kwa gharama kubwa; utapata Fedha za Maendeleo ya Jimbo na ukimaliza kipindi chako, hata kama hukurudi tena bungeni, utalipwa “mafao” manono, kiasi cha mamilioni ya fedha!

Wakati yote haya yanatendeka, watumishi wataalamu: Walimu, Madaktari na watoa huduma Sekta ya Afya; Mafundi Mchundo na Wahandisi; Mahakimu, Askari Polisi na Wanasheria (angalau hawa katika kundi la watoa haki wana nafasi kubwa ya kujineemesha kwa rushwa, kutokana na wananchi kuogopa kusweka jela!), wanalia njaa. Katika mfumo mzuri, watu ambao walikuwa wapate kipato kizuri ni wataalamu na mambo yangekwenda vizuri, na siyo wanasiasa!

“Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN) ni ulaji tu. Zipo idara za kufuatilia Ikulu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Hazina ila havifanyi kazi.

Tatizo kubwa ni kwamba wakati madhila yote haya yanatendeka, hakuna hatua za maana zinazochukuliwa wala angalau kukemea. Hatua iliwahi kuchukuliwa mwaka 2012 katika Halmashauri ya Bagamoyo, kwao Mheshimkwa Rais, ambako Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alitiwa msukosuko mkubwa na Waziri Mkuu, baada ya mambo kutokwenda vizuri! Inasemekana alihamishwa! Lakini ilitarajiwa moto wa Bagamoyo ungesambaa kwenye Halmashauri nyingine, nyingi zao zimekuwa zikifanya “madudu” mabaya zaidi kuliko ya Bagamoyo. Wapi, moto uliishia hapohapo!

Kutokana na kulegalega katika utekelezaji, Rais ilibidi auige mpango wa BRN kutoka Malaysia ambao kwa hakika ni mpango wa gharama kubwa mno kusimamia utekelezaji. Linaibuliwa jambo, wadau na wataalamu mbalimbali wanalichambua, wanalifanyia kazi, wanatoa mapendekezo ya utekelezaji, anakabidhiwa jukumu mtekelezaji na baadaye anafuatiliwa na kitengo maalumu kilichoko Ofisi ya Rais.

Katika hatua zote hizo hapo juu mabilioni yanatafunwa, kwa posho za semina, vikao, ziara n.k. Kuibuliwa kwa BRN ni ushahidi wa ugoigoi katika utekelezaji. Kumekuwa na vitengo vya ufuatiliaji Wizara ya Mipango iliyo chini ya Ofisi ya Rais (Tume ya Mipango); Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu) na Wizara ya Fedha. Kwa nini na vipi havikuhamasishwa kutimiza wajibu wake, hakuna ajuaye. Hivi, mbona mradi wa matumizi ya Maji ya Ziwa Victoria yaliyofikishwa Shinyanga ulitekelezwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu bila ya BRN?

Hivi Ujenzi wa Barabara za kuunganisha miji mikuu ya mikoa ulioanza kutekelezwa wakati wa Awamu ya Tatu na unaoendelea sasa, ilikuwa ni BRN? Hivi ujenzi wa sekondari kila Kata na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika miaka ya mwanzo ya Serikali ya Awamu ya Nne, ni BRN? Kimetokea nini tena hadi utekelezaji umelala na kuibuliwa BRN?

 

Hata Katibu Mkuu wa CCM alithibitisha uozo katika utekelezaji

 Uozo wa utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Nne siyo majungu, bali ulithibitishwa na ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika mikoa yote nchini, ambako alijionea “madudu” makubwa mpaka akawabaini mawaziri “mizigo” na kuahidi kwenda kuwashitaki kwa Rais!

Katibu Mkuu wa CCM alilalamikiwa na akajiridhisha kuwa wakulima wanakopwa badala ya kuliwa fedha taslimu, wafanyabiashara ndogo ndogo wanapigwa, wananyanyaswa na wanadhulumiwa bidhaa zao huku watendaji wa Halmashauri nyingi wanashindwa kutekeleza na kusimamia miradi – alimradi vurugu tupu!

Kwa hiyo tatizo kubwa na kuchokwa kwa Serikali ya CCM siyo Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa; bali, kwanza, ni kushindwa kutekeleza kwa umakini na kwa kasi inayostahili ahadi zake yenyewe na pili, kushindwa kuchukua hatua thabiti kwa uozo kama rushwa, “ufisadi”, uonevu, kuwanyima watu haki n.k. Nini kinafanywa kukabiliana na uonevu wa baadhi ya wawekezaji, hasa katika sekta ya madini wanaowabana wachimbaji wadogo wadogo, kwa mfano?

Nini kimefanyika kwa kuchinjwa kama kuku kwa albino? Nini kimefanyika kwa wakulima wanaokopwa mazao yao? Walioathiriwa na Operesheni Tokomeza? Walioathiriwa na ugomvi usiokwisha kati ya wakulima na wafugaji? Wanaokosa usafiri wa uhakika wa reli kwenda Bara kutokana na kupuzwa kwa kuimarishwa kwa njia za reli? Gharama kubwa za usafirishaji na uchukuzi, kutokana na kushamiri kwa biashara ya kampuni za wakubwa ya malori? Nini kinafanyika kuondoa msongamano wa magari Jiji la Dar es Salaam?

Kama hayo masuala ya kutosimamia vizuri uchumi hayatoshi, CCM ikajitumbukiza katika mgogoro wa kisiasa kutokana na uchujaji usiokuwa wa haki wa wagombea nafasi za uongozi. Si tu kwa madiwani na wabunge, bali hata kwa nafasi ya urais. Waliotumia fedha, wengi wamepita; wasiokuwa na fedha, wamekatwa. Baadhi ya viongoni wakubwa, ilibidi wahojiwe na Takukuru kwa tuhuma za rushwa na kukutwa na fedha za kugawa.

 

Wala rushwa, wazembe wanatukuzwa, Lowassa aligeuzwa mbuzi wa kafara

 Ndipo linapotajwatajwa jina la Lowassa; kwamba wakubwa wa CCM, kinyume cha kanuni walizojiwekea wenyewe, wakaenda katika vikao vya mchujo wakiwa na majina yao mfukoni. Tunaambiwa kuwa wengine walikuwa wana shinikizo la familia, wengine walikuwa wakimwogopa Lowassa bila ya shaka kwa mambo ambayo wanahisi hawakumtendea vizuri na wengine walifuata utaratibu wa “Kuna Mgongo Wangu na Mimi nikune wa Kwako”.

Siyo siri kwamba Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ambaye ni mmoja wa waliokuwa katika orodha ya wale waliotakiwa, alipoamua kugombea urais, nafasi yake ya ubunge wa Mtama, Lindi siyo alimpatia, bali alimkabidhi Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. Je, haiyumkiniki vipi Katibu huyo ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM asimpigie “debe” Membe na kumshindilia kwa nguvu zote Lowassa, ambaye alikuwa anaonekana tishio?

Yaliyotokea, yanajulikana wala hayana haja ya kuyarudia. Mkakati wa uongozi wa juu wa CCM ulioratibiwa rasmi, ulikuwa na Plani “Aa” na Plani “Be”, lakini hawakuwa na Plani “Che”! Plani “Aa” ni kumkata Lowassa, kwa vyovyote vile lazima achinjwe tu kama mbuzi wa kafara; Plani “Be” ni kuwa kama Membe na wale wengine waliotakiwa hakuwakupita, basi atasukumizwa mtu ambaye yatafikiwa maridhiano kuwa awe yeye. Sasa Plani “Che”, ambayo ni je, kama Lowassa aliyekatwa atahamia upande wa upinzani, atashughulikiwaje? Plani hii haikuwapo kwa kuwa wakubwa wa CCM waliaminishwa kuwa Lowassa akikatwa, atanung’unika tu, lakini hatohama, atabaki CCM! Taharuki kubwa iliyoikumba CCM ni kuwa siyo tu Lowassa, kafanya uamuzi mgumu wa kuachana na CCM kujiunga UKAWA, kupitia CHADEMA, bali kwa mara ya kwanza katika historia ya Chama hicho, wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM ambao ni karibu nusu ya wajumbe saba wa kuchaguliwa kutoka Tanzania Bara katika Kamati hiyo, waliupinga wazi wazi uamuzi wa Kamati Kuu kuhusu uteuzi wa mgombea urais mwaka huu na kulaumu kuwa kanuni zilikiukwa!

 Naye muasisi wa CCM, alipoona utaratibu wa kufikia maridhiano katika vikao haukutakiwa kuhusu jambo hilo, akatoka hadharani kuwaunga mkono wajumbe hao watatu. Wenyeviti wa CCM wa mikoa ya Shinyanga na Singida, nao wakajitoa CCM na kufuatiwa na baadhi ya wabunge na makada wengine mashuhuri, akiwamo Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye. CCM inaweza kusema haijatetereka, lakini ni dhahiri haijawahi kupata pigo kama hili ambalo, mchambuzi mmoja wa mambo alisema hakuna haja ya kuwaonea huruma kwa kuwa huo ni kama “msiba wa kujitakia, huwa hauna kilio”.

   Mchambuzi mwingine aliandika kuhusu Lowassa kwa Kiingereza:

 “Lowassa the humble man, the scapegoat & the wild card- why I think he Will Win the Preidency…

Speaking from a voter’s point of view, I was very impressed by Lowassa’s gesture yesterday and today, when he went to visit the commoners. To me, it looks like Lowassa is indeed a skilled politician, and I am starting to think that he will indeed win the presidency…

“Lowassa enjoys a huge following the likes of which has hitherto not been seen in our land. This is a FACT and it has been evident since last year – way before the election season – in all the places he visited across the region. CCM knew it, UKAWA knew it, and so did all the ‘bigwigs’ in the government corridors of power.

“In fact, this was a threat to them and that is why they have always fobbed him off. In politics, anyone who has the support of the majority has the mandate. And obviously, having a mandate means having power, and that’s what politics’s about. There’s nothing like the majority’s mandate – voters don’t care about what the critics say once they make up their mind – and that’s exactly what’s happening here.

“The other monumental thing that people don’t quite get yet is that Lowassa is now profiting from public empathy because of what happened in his career before – how he was treated by his colleagues…”

Kwa tafsiri yangu:

“Lowassa, mnyenyekevu, msingiziwa na karata ya turufu…nikizungumza kama mpigakura, nilivutiwa sana na hatua ya Lowassa jana  alipokwenda kuwatembelea walalahoi (alivyokwenda Gongo la Mboto,  Tandika, Mbagala na kupanda daladala na kuzungumza na wananchi wa kawaida). Kwangu mimi Lowassa ni mwanasiasa mahiri, na naanza kufikiri kuwa anaweza akashinda urais…

“Lowassa ana wafuasi wengi ambapo haijapata kutokea nchini mwetu. Huu ni ukweli usiopingika na ulidhihirika tangu mwaka wa jana – muda mrefu kabla ya msimu huu wa uchaguzi- popote anapokwenda nchini. CCM ilikuwa inalijua jambo hili, UKAWA inajua, na pia wakubwa wenye madaraka serikalini walijua…

“Kwa kweli hali hii ilikuwa ni tishio kwao na ndiyo maana mara kwa mara wamekuwa wakijaribu kumzuiazuia. Katika siasa, yeyote anayeungwa mkono na watu wengi basi anakuwa na mamlaka. Na kuwa na mamlaka maana yake ni kuwa na uwezo na nguvu, na siasa maana yake ni hiyo. Na hakuna kitu muhimu katika siasa kama mamlaka inayotokana na kuungwa mkono na watu wengi – wapiga kura wanapotaka kufanya maamuzi yao huwa hawajali wakosoaji wanasema nini – na hiki ndicho kinachotokea sasa hivi…

“Jambo jingine muhimu ambalo watu hawajalielewa ni kwamba Lowassa sasa anavuna huruma ya watu wengi, kutokana na yale yaliyomtokea katika maisha ya kazi yake – yale ambayo wanasiasa wenzake walimfanyizia…”

Inadaiwa kuwa Lowassa amekatwa kwa sababu za kukiuka maadili, kanuni (sijui maadili na kanuni gani?) na tuhuma za ufisadi. Hakuna hata taarifa rasmi ya CCM inayoeleza kwa hakika, sababu hasa ya kuliondoa kinyemela jina la Lowassa, kiasi kwamba inawafanya watu waamini kulikuwa na hila.

Mwenyekiti wa CCM Taifa alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa uamuzi huo ulipata baraka kwa mashauriano na viongozi wakuu wastaafu waliokuwa wamealikwa kushiriki katika mchakato wa kumpata mgombea. Mahitaji ya ushauri wa viongozi hao katika mchakato wa kutafuta wagombea haumo katika Katiba wala Kanuni za CCM.

Haijulikani, labda watu wa Kamati ya Maadili inayoongozwa na Mzee Phillip Mangula ndiyo wanaojua, maadili gani na kanuni gani hasa alizozikiuka Lowassa, ambazo wagombea wenzake walizifuata kwa ukamilifu wake. Haijulikani ufisadi gani alioufanya mpaka akaonekana hafai kuwa mgombea wa CCM.

 

Mbona kashfa nyingi, Serikali ya CCM imeshindwa kuzichukulia hatua?

 Kama ni kashfa ya Richmond ya mwaka 2008, mbona Lowassa alikwishajiuzulu pale pale wakati huo ili kuwajibika kisiasa na “kukinusuru Chama chake na Serikali?” Vilevile Serikali ilikwishatekeleza mapendekezo ya Bunge kuhusu kashfa hiyo; kama ni ufisadi, mbona kuna vitendo vingi vya kifisadi na uzembe, ambavyo Serikali imevifumbia macho na wala havimhusu Lowassa? Vipo vingi, lakini kwa uchache: Kashfa ya mfanyabiashara Chavda inayohusu mashamba ya mkonge; Kashfa ya Loliondo; Kashfa ya Sukari; Magogo na Mbao kuuzwa nje kwa magendo; Ubinafsishaji holela wa Taasisi za Serikali kama NBC, TTCL, Mgodi wa Kiwira; Madai ya Rushwa ya Rada; Mikataba mibovu ya uwekezaji katika Madini; Fedha za EPA zilizochotwa Benki Kuu; Kusafirishwa nje kwa magendo kwa Meno ya Tembo na kukamatwa huko; Kuuawa kwa Faru; Wanyama kutoroshwa Nje kwa magendo, wakiwa hai; Kuruhusu Uvuvi haramu bila ya kuchukua hatua; Kashfa ya Fedha za Pembejeo zilizoliwa; Fedha za Gaddafi; Fedha za Rushwa za Escrow; Ununuzi wa Mabehewa Mitumba?

Je, Lowassa yumo humo? Mbona wahusika wanaotuhumiwa na madhila hayo hawakuchukuliwa hatua?

Anguko la CCM lilitabiriwa hata na Mwenyekiti wake wa sasa. Akifunga mafunzo kwa Makatibu wa Mikoa, Makatibu na Wenyeviti wa Wilaya wa Chama hicho Oktoba 2013, Rais Kikwete alikaririwa akisema endapo rushwa haitakomeshwa ndani ya Chama hicho, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, kitaanguka vibaya.

Ni dhahiri rushwa, tangu alipotoa onyo hilo mpaka leo hii, haijapungua, bali imeongezeka.

Naye, muasisi wa CCM, Peter Kisumo, akihojiwa na wanahabari kuadhimisha miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Nyerere alikaririwa akionya kuwa tatizo kubwa la CCM ni kuendelea kuwa Chama dola, kiko mbali na wananchi, huku kikishindwa kudhibiti rushwa na kuwawajibisha wahusika wa vitendo hivyo.

“Kila mtu amekuwa mlalamikaji, hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji…kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa Chama cha Upinzani, na hasa CHADEMA, kutumia mwanya huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi…,” alisema Mzee Kisumo. Hali hiyo inajidhihirisha sasa!

Chini ya Mfumo huu wa Demokrasia ya vyama vingi vya siasa, ambao CCM yenyewe iliukubali, ni kwamba lazima ifike mahali, CCM ikubali kuachia ngazi na kukipisha chama kingine kiendeshe Serikali. Nacho chama hicho kingine kikishindwa kutimiza matarajio ya wananchi, pia kiondoke kwa desturi ya mfumo huo.

Kwa hali ilivyo sasa, inaonekana CCM inaumwa, hivyo itulie wakati huu daktari wake- wananchi wapigakura, anaipiga sindano, isipapatike! Sindano yenyewe ni kunyimwa kura kwenye kisanduku cha siri cha kupigia kura. Bila ya shaka baada ya dawa hiyo kuiingia CCM taratibu, Chama hicho kitapona kwa kujipanga upya na kupata nguvu za kutekeleza kwa ukamilifu sera zake, kuridhisha matakwa ya wananchi katika uchaguzi miaka ijayo. Ndiyo maana ya Mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa, kama ilivyo Uingereza – mara Labour, mara Conservative; au Marekani, mara Democrats, mara Republicans.

Wala siyo jambo baya, kwani CCM “ikiachia ngazi” mwaka huu, itakuwa kitendo cha kiungwana kuimarisha demokrasia ya vyama vingi. Hakuna sababu ya kung’ang’ania!