Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Kila ifikapo Oktoba 15 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Unawaji Mikono Duniani, lengo likiwa ni kuendelea kujenga ulimwengu wenye afya na kusaidia kupigana vita dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko.
Katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma maadhimisho hayo yamefanyika katika Shule ya Msingi Mtumba iliyopo Kata ya Mtumba yakiwa yamebeba kaulimbiu isemayo “Tuungane pamoja kuhakikisha usafi wa mikono kwa wote”
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema kuwa ili kuhakikisha Wilaya ya Dodoma inajilinda na kujikinga na magonjwa ya mlipuko amewataka maafisa Afya kufanya ukaguzi katika vilabu vya pombe ili kuhakikisha kuwa maeneo hayo kuna vifaa vya kunawa mikono na matundu ya kutosha ya vyoo.
Amesema kuwa kunawa mikono kutaisaidia jamii kuepukana na magonjwa ya mlipuko na kuifanya jamii kuwa imara na yenye afya hivyo ni vyema maafisa afya wakapita katika maeneo ya vilabu vya pombe ili kukagua kama maeneo hayo wameweka vifaa vya kunawa mikono, na ikiwa hakuna vifaa vya kunawa mikono basi kilabu kifungwe.
“Nasisitiza kunawa mikono kwani mekuwa ni kawaida ukitembea kwenye vichochoro na kwenye vilabu vya pombe unakuta mtu anaingi kichaka anajisaidia na humuoni akinawa mikono” amesema Shekimweri
“Sasa nielekeze ya kwamba hata katika vilabu vya pombe maafisa afya wapite wahakikishe kuwa maeneo hayo kuna sehemu kwa ajili ya kunawa mikono na ili wamiliki waendelee kufanya biashara ni lazima waweke maeneo ya kunawa mikono na matundu ya kutosha ya vyoo, kwa kufanya hivyo nina imani tutapambana na magonjwa ya mlipuko,” amesema Shekimweri.