Na Julius Konala,JamhuriMedia,Namtumbo
WANANCHI na wanafunzi wa kijiji cha Mtonya kilichopo katika Kata ya Likuyu Seka wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, wamenufaika na mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kupitia ufadhili wa kampuni ya Mantra Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa lengo la kupunguza ajali na vifo kwa watumiaji wa barabara hizo wilayani humo.
Mafunzo hayo ya siku moja yalifunguliwa hivi karibuni na kaimu kamanda wa polisi(OCD)wa wilaya ya Namtumbo ASP John Ntunde katika viwanja vya shule ya msingi Mtonya na kuhudhuriwa na Diwani wa kata ya Likuyu Seka,mtendaji kata na kijiji,walimu,wanafunzi,askari polisi pamoja na wadau wa usalama barabarani toka kampuni ya Mantra Tanzania.
Akifungua mafunzo hayo kwa wananchi na wanafunzi wa shule ya msingi Mtonya,ASP Ntunde ambaye pia ni mkuu wa kikosi cha usalama wilayani humo amewataka watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ikiwemo kuepuka ulevi na kukimbia mwendo kasi.
Aidha amekemea tabia inayofanywa na baadhi ya waendesha bodaboda wilayani humo ya kubeba abiria juu ya mzigo,kubeba abiria wengi( mishikaki)kuweka mziki mkubwa kwenye pikipiki zao hali inayosababisha pindi wanapopigiwa honi washindwe kusikia pamoja na kuendesha vyombo vya moto bila ya kuwa na Bima.
Naye kaimu mkuu wa kikosi cha usalama barabarani(DTO)wa wilaya ya Namtumbo Kaunda Kaunda akitoa tathmini ya utendaji kazi wa kikosi hicho alisema kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2021/2022 ajali za vifo zilikuwa 2 na Februari hadi Machi 2022 ajali za vifo zilikuwa 3 sawa na ongezeko la asilimia 33.33 na kwamba katika kpindi hicho jeshi hilo limeweza kupunguza ajali kutoka 13 hadi kufikia 7.
Hata hivyo Kaunda aliyataja mafanikio yaliyopatikana tangu elimu hiyo ya usalama barabarani ianze kutolewa kwa wananchi,wanafunzi na watumiaji wa vyombo vya moto kuwa ni kupungua kwa ajali kwa watembea kwa miguu na waendesha vyombo vya moto huku akizitaja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni uhaba wa vyombo vya moto kwa watoa elimu ya usalama barabarani wilayani humo.
Meneja uhusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Khadija Pallangyo alisema kuwa lengo la kuendesha mafunzo hayo kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu ni kutaka kukabiliana na changamoto ya ongezeko la magari baada ya mgodi kuanza kazi.
Pallangyo alisema kuwa tangu kampuni hiyo ianze kutoa elimu ya usalama barabarani wanafunzi 14,000 wamefikiwa na elimu hiyo ambapo amedai kwamba katika kipindi cha mwaka 2022 kampuni hiyo inatarajia kutoa elimu hiyo kwa shule 28 zilizopo katika barabara kuu itokayo Songea kuelekea Tunduru pamoja na zilizopo katikati ya wilaya hiyo.
Awali askari wa kikosi cha usalama barabarani wilayani humo Nurdin Juma na Rashid Bilinji walitoa mada mbalimbali kwa washiriki wa mafunzo hayo ikiwemo namna ya kuvuka barabara kwa watembea kwa miguu na watumiaji wa vyombo vya moto.