Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinaendelea. Mengi yanazungumzwa na wagombea na wafuasi wao.

Ahadi nyingi za wagombea urais zinalenga kuwashawishi wapigakura wawachague. Zipo ahadi zinazofanana.

Elimu, maji, vita dhidi ya mafisadi na wala rushwa, mikopo kwa wajasiriamali, ajira na ukomeshaji aina zote za uonevu katika jamii, ni baadhi tu ya ahadi zinazowavutia wengi. Bila shaka kinachofanywa na wapigakura kwa sasa ni kutafakari nani miongoni mwa wagombea hawa anayeweza kutekeleza kwa dhati ahadi zake kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya chama chake.

Mzee Yusuph Makamba, akimnadi mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, mjini Morogoro, alizungumza jambo ambalo liliniingia. Nalo si jingine, isipokuwa la kumtaka mgombea huyo, pamoja na kutangaza Ilani ya chama chake, aingize na yake mwenyewe.

Akatoa mfano wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho hakikuwa kwenye Ilani, lakini Rais Jakaya Kikwete, akaweza kukijenga na kuifanya Tanzania kuwa na chuo kikuu kikubwa kuliko vyote katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa kweli utashi wa mgombea na dhamira yake ya kubadili hali ya maisha ya wananchi vinaweza kuwa na msaada mkubwa kwenye ushindi wa mgombea na chama chake. Sidhani kama Watanzania wana utamaduni wa kusoma sana yaliyo kwenye Ilani za vyama, isipokuwa mara nyingi wamependa kumchagua mtu wanayedhani anaweza kutimiza matamanio yao.

Mwaka 2005 nilishiriki kwenye kundi la wanahabari tulioaminishwa – nasi tukawaaminisha wananchi- kuwa Maisha Bora kwa Kila Mtanzania yangewezekana. Dhamira hiyo ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, si kwamba haikutekelezwa; isipokuwa swali ni je, wangapi waliofaidika?

Ukiwauliza watu waliosafiri na Rais Kikwete safari zaidi ya 400 nje ya nchi kama Maisha Bora kwa Kila Mtanzania lilikuwa ni jambo la kufikirika, watakuona mtu wa ajabu! Ukiziuliza familia ambazo hazikuwa na kitu, lakini ghafla ndani ya miaka 10 zimejikuta zikimiliki mamia ya malori ya mizigo, hoteli kubwa kubwa na vitega uchumi vya kila aina; hizo zitakuambia kuwa ahadi ya Mheshimiwa Kikwete imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa sana!

Kwa wale waliokuwa wakihaha kusaka maisha kwenye mashine za kusaga unga, ghafla wamejikuta wakimiliki mashirika makubwa yaliyokuwa ya umma, bila shaka hao wako tayari kuanzisha ugomvi endapo watamsikia yeyote awaye akiisema “vibaya” Serikali ya Awamu ya Nne.

Wale ndugu ambao watoto wao wameendelea kuketi chini ya mawe kwa kuyafanya “madawati mbadala”; au wale ambao daktari anawaandikia vyeti na kuwaelekeza wakanunue dawa kwenye maduka yao au waliyo na ubia nayo; wakulima wanaokopwa, wakulima wanaouziwa mbegu za pamba zisizoota; hao na wengine wa aina hiyo kwao hakuna cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.

Nimezitafakari baadhi ya ahadi za wagombea na kuamini kuwa zinaweza kuleta usumbufu baadaye. Kwa mfano, karibu wagombea wote wanazungumza juu ya kutobughudhiwa kwa waendesha bodaboda, wachuuzi na makundi mengine kama ya wafugaji na wakulima.

Ahadi za aina hii zinapaswa kutolewa kwa hadhari kubwa kwa sababu mbalimbali.

Mosi, nchi yoyote iliyostaarabika, imestaarabika kwa sababu watu wake ni wastaarabu. Ustaarabu hauwezi kuja wenyewe tu kama mana, isipokuwa ni matokeo ya mpangilio wa maisha ulioamuriwa na kukubaliwa na jamii husika.

Mpangilio huo unapatikana kupitia kanuni, mila, desturi na sheria mbalimbali. Katika jamii ya watu waliostaarabika, kutii sheria si suala la mjadala, na wala si jambo la kwamba mtu anaweza kuwa na chaguo la kutii au kutotii sheria. Utii wa sheri ni wajibu.

Miongoni mwa mambo yanayoiumiza Afrika, ni kwa baadhi ya watu wake kukosa utii kwenye sheria zinazotungwa ili ziwe mwongozo wa maisha ya kila siku. Lakini wapo Waafrika wanaoelekea kuondokana na tatizo hilo.

Waliofika Rwanda wanaweza kuona mfano halisi wa nchi au jamii iliyokubali kutii sheria. Nchini Rwanda, mwananchi kuvaa kandambili “mjini” au kuwa mchafu-chafu ni kosa. Adhabu zake zipo. Kuendesha gari likiwa limejaa vumbi katikati ya mji ni kosa. Madereva wa Tanzania wanajua kabisa wanapofika mpakani, kabla ya kuingia Rwanda ni lazima waoshe malori yao na pia wao wenyewe waoge, wavae nguo safi na waonekane nadhifu. Wanajua wakiingia Rwanda spidi iliyopangwa lazima iheshimiwe. Wanajua wakiwa nchini humo ni marufuku kutema mate hovyo, kurusha chupa za maji au kufanya jambo lolote ambalo ni uchafu. Wakiwa Rwanda wanatii vema kabisa sheria hizo, lakini wakishaaga mpakani, basi utawakuta wameegesha malori upande wa Tanzania-wakijisaidia hovyo! Wanatupa chupa za maji na wanafanya kila aina ya uchafu. Wanafanya hivyo kwa sababu utawala hausimamia sheria.

Kinachoonekana Rwanda kipo katika miji kadhaa ya Tanzania. Mfano ni Moshi, Arusha (kidogo), Musoma na hata pale Gairo. Mgeni au mweyeji anayetupa taka hovyo au anayeengesha gari bila kufuata utaratibu katika miji ya Arusha na Moshi, anaadhibiwa. Hatua hiyo imeifanya miji hiyo iwe misafi hata kama ni kwa maeneo yale ya katikati tu.

Ahadi ya wagombea urais wetu ya kwamba watahakikisha wamachinga hawasumbuliwi, nadhani inapaswa kufafanuliwa vizuri. Wengi walivyoelewa ni kuwa iwe Dk. Magufuli, au Lowassa, yeyote kati yao akiingia madarakani atahakikisha hawabughudhiwi!

Hapa tukubaliane kuwa miongoni mwa kazi kubwa zitakazopaswa kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Watanzania wanarejeshwa kwenye utaratibu wa kuishi kwa kufuata taratibu na sheria za vijiji, miji na nchi. Haiwezekani kila mahali kukawa ni sehemu ya wamachinga kufanyia biashara. Haiwezekani muuza wali akaegesha masufuria yake mbele ya choo cha umma eti mgambo wasimwondoe kwa sababu anatafuta riziki! Utaratibu huu ndio uliolifanya Taifa letu lifunge ndoa na kipindupindu- ugonjwa ambao kwa kweli ni wa aibu na ni kielelezo cha nchi isiyozingatia misingi za afya za watu wake licha ya kuwa na mabwana na mabibi afya kila kona.

Haiwezekani wamachinga na wachuuzi wengine wakahodhi maeneo ya waenda kwa miguu na kuwalazimu wenye kustahili kutumia maeneo hayo kubanana kwenye barabara kuu za magari.

Kuwaondoa wachuuzi kwenye maeneo ya waenda kwa miguu ni jambo jema na linalopaswa kutekelezwa kisheria. Haiwezekani maeneo ya vituo vya mabasi kama vile vya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi yawe ya wachuuzi wa machungwa, maji, vocha na kadhalika.

Kuwaahidi wamachinga kuwa hawatabughudhiwa ina maana siku wakiamua kutundika sidiria, mitumba ya nguo za ndani, na wanasesere kwenye kuta za Ikulu, hakuna atakayewaondoa! Nani awaondoe kama Rais kaagiza wasibughudhiwe? Je, hapo tutakuwa na nchi ya aina gani? Rais akithubutu kuwaondoa, ataibua machafuko maana alishaingia nao mkataba wa yeye kupewa kura kwa masharti ya kuhakikisha hawabughudhiwi!

Bodaboda: Si sahihi kuwaahidi kuwa hawatabughudhiwa. Madai yao ni kwamba polisi wanawaonea. Wanawaonea kwa lipi? Polisi gani aliyekula kiapo ataacha kumuuliza dereva wa bodaboda leseni inayomruhusu kuendesha chombo cha moto? Kwanini wasiulizwe bima za pikipiki wanazoendesha? Polisi wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria. Kuna kosa gani polisi kuhoji vitu hivyo? Je, kuuliza hivyo vitu ndiyo kuwanyanyasa bodaboda? Asiyejua janga la bodaboda azuru wodi ya majeruhi MOI, Muhimbili na katika hospitali zote nchini. Wagombea urais wazuru huko wajionee balaa. Wakifanya hivyo watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa ahadi!

Jingine linalofanana na hilo ni la madereva wengine, hasa wa daladala. Wanapodai kuwa trafiki wanawapiga faini, nani anaweza kusimama kwa hakika na kuthibitisha kuwa kapigwa faini ilhali gani lake likiwa halina kosa? Je, kuwaandama hawa ili watii sheria ni kosa? Nadhani wagombea wetu wanachopaswa kukisema hapa ni kwamba kama kuna dereva –awe wa bodaboda, lori, daladala n.k-anayeona kaonewa, afikishe malalamiko yake kwenye ngazi zinazohusika. Kuwapa kiburi hawa madareva maana yake ni kutoa kibali cha wao kuendelea kuvunja sheria za nchi na kusababisha maafa barabarani. Hapa ikumbuwe kuwa adhabu za makosa ya usalama barabarani kwa Tanzania ni dhaifu mno. Zinawapa kiburi cha hali ya juu madereva. Matokeo yake Tanzania kila mwaka inazika maelfu ya watu wanaokufa kwa ajali za barabarani. Hili halikubariki.

Wiki iliyopita nilitetea Dk. Magufuli kwa namna anavyoshutumiwa kwa masuala kama ya bomoabomoa ya nyumba za watu waliojenga ndani ya hifadhi za barabara. Wasomaji kadhaa walinishutumu wakihoji kwanini namtetea. Lakini baadaye nikabaini kuwa waliochukizwa na utetezi huo ni wale waliojenga nyumba ndani ya hifadhi za barabara. Hapo nikaona hawana hoja.

Lakini mmoja akasema kwenye uongozi wa nchi kunahitajika busara zaidi kuliko kusimamia sheria! Hilo nalo likawa jipya kwangu. Kuwa kiongozi wa nchi ni muhimu sana kutumia busara, lakini nadhani hili la busara sasa linatumiwa na watu ambao kwao utii wa sheria ni jambo la hiari. Nchi hii imekwama mambo mengi kwa sababu hiyo hiyo ya “busara”. Nchi hii kuna watu wameiba mabilioni ya fedha za umma, lakini “busara” iliyotumika si ya kuwapeleka mahakamani wakafungwa, isipokuwa kuwabembeleza wazirejeshe. Walipozirejesha mambo yakaishia hapo!

Busara ya aina hiyo sasa ndiyo inayopigiwa debe ilhali kuna wezi wa vitasa vya magari wakiozea magerezani. Watanzania wanataka kuona wanampata Rais ambaye ataapa kuzilinda sheria za nchi.

Rais hatapendwa kwa kuwaachia wamachinga au madereva wa bodaboda wafanye wanavyotaka. Atapendwa kwa kuhakikisha sheria zinafuatwa maana anaapa kuzilinda. Hii haina maana kwamba hakuna sheria mbaya. Zipo. Sheria zisizofaa, kama zile zilizoainishwa na Tume ya Jaji Nyalali ndiyo muda wake wa kuziondoa.

Kiongozi msimamia sheria ni mtenda haki. Mtenda haki hupendwa na wengi. Waziri Mkuu Edward Moronge Sokoine, alipendwa si kwa sababu aliruhusu watu wavunje sheria, la hasha! Alipendwa kwa sababu alisimamia sheria na kwa njia hiyo akawa mtenda haki aliyependwa pengine kuliko mawaziri wakuu wote ambao Tanzania imeshawapata.

Wagombea urais wawaeleze ukweli wananchi kuwa wakiingia madarakani kitu muhimu zaidi cha kurejesha imani yao kwa Serikali ni kusimamia kwao utawala wa sheria katika Taifa letu. Tanzania mpya inakuja.