Kila siku ni nafuu ya jana, watu wana sura za furaha lakini hawajui kesho yao itakuwaje, mimi ni mmoja wao kati ya hao ambao kesho yao ni hadithi sijui itakuwaje, leo ni nafuu ya kesho lakini ngumu kuliko jana na maisha yanaenda.

Unapoambiwa Mungu ni mwema na Mungu ni mkubwa ndio kama hivi, unapoambiwa anatenda miujiza sina sababu ya kukataa ukweli huo, usiku wa jana unaanza kwa kutokuwa na bakaa yoyote ya akiba kwa baba mwenye familia ya watoto sita, asubuhi inafika hujui kifunguwa kinywa kimepatikanaje kwa kuungaunga viporo.

Nje ya kibanda changu  kuna mabango mengi yaliyobandikwa bila ridhaa yangu yakiwanadi wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa, wapo waliodiriki kuja kunitaka niwape kura yangu, wengine wanaondoka wakiwapungia wanangu kwa kuwapa vijisenti kama zawadi huku nikiwa nimeachiwa bendera na ahadi, siku inapita naingoja kesho ambayo siijui ujio wake.

Siasa kwa sasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu zinanivuruga  na kunifanya nione maisha magumu kupitiliza, nashiba siasa, maendeleo siyaoni, nasikia sera lakini sizielewi, nawasikia wagombea lakini siwafahamu wana nia gani na mimi, na hata wale wenye kauli nzuri najiuliza ni kweli?

Yapo mengi ambayo yananivuruga kila siku, nachukua uamuzi ambao hubadilika kila uchao, nina hofu hadi siku ya mwisho nitashindwa kupigakura na kuamua kukaa nyumbani, hebu fikiria ugomvi wa kila siku wa viongozi wanaogombea kuniongoza.

Kipindi hiki cha uchaguzi zinafunguliwa Biblia kutuaminisha kuwa wagombea ni wacha Mungu, inafunguliwa Misahafu na kusomwa mbele yetu ili tuamini kuwa hao siyo watu wabaya, wapambe wao wanaongoza ibada kutuonyesha kuwa hao ndio wateule wa Mungu.

Kipindi hiki wenye nguvu ya fedha wanaonekana kuwa watu wazuri na wakarimu, wanatangaza kuyajua matatizo yetu na kuahidi kuyamaliza pindi tu tutakapowapa kura zetu, kipindi hiki wao wanatukanana kuonyesha kuwa wengine siyo waadilifu ni wabaya, umekuwa mchezo wa kuigiza, kusikia matusi na kejeli miongoni mwa waliobandika picha zao katika mbavu zangu za mbwa.

Sitaki kujuta kwanini nipo hapa, nitajuta nikifa nikiwa bado maskini ninayeshindwa kumudu milo mitatu, kushindwa kupata matibabu ya kisasa badala ya kutibiwa na waganga wa kienyeji, nitajuta nitakapogundua kuwa wanangu wamekosa elimu kwa sababu ya umaskini wangu.

Nitajuta baada ya kuona kuwa kura za wenzangu zimenunuliwa na kutupatia kiongozi mbovu, nitajuta nitakapogundua baadhi yetu wapiga kura tunashughulika na ushabiki badala ya siasa, nitajuta nikigundua kuwa wapigakura ndio tunaosimika uongozi mbovu.

Majuto ni mjukuu, na nilianza kujuta siku nyingi, ndio maana leo nawahusia wanangu juu ya uongozi bora na si bora uongozi, tumeshuhudia wabunge wetu ambao sasa wanarudi majimboni kwa mbwembwe nyingi huku wakijua fika kuwa tangu tumewapa dhamana ya uongozi uliopita hawakuwahi kurudi japo kutusabahi.

Sasa hivi wamerudi na mbwembwe nyingi wakitusabahi huku wakipiga magoti, wakishiriki misiba yetu na kutoa michango, wakitoa magari yao ya kifahari kutupa lifti, wakiacha suti zao na kuvaa matambara kama sisi lakini wao wamenona, wakiongea vizuri lugha yetu lakini siyo lugha yao ya bungeni ambayo huwa hatuelewi, wamerudi na maelezo ya kupinga miswada ya kutusaidia na kuwasilisha hoja zilizopingwa.

Wamerudi na kutukuta kama walivyotuacha na shida zetu, wamerudi na posho zao kutuhadaa tena na tunahadaika kutokana na ugumu wa maisha, viongozi bora tunawaona lakini tunawasikiliza wao kutokana na fimbo ya fedha zao, kila siku itaendelea kuwa nafuu ya kesho.

Natamani uchaguzi uwe kesho maana labda hizo fedha walizonazo zitaingia katika mzunguko ili name niuze samaki na mafuo yangu ya nazi, natamani uchaguzi uwe kesho ili nisikumbushwe machungu yangu kwa hotuba zao, natamani uchaguzi uwe kesho ili matumizi ya fedha za kampeni zisaidie kutuchimbia hata visima vya maji tunywe kama wanyama.

Natamani uchaguzi uwe kesho ili ugomvi baina yao upunguwe tuwe na amani, natamani uchaguzi uwe kesho ili tupate viongozi bora ambao hawajahonga watu na kuwafanya wale wanaonunua uongozi wabaki na hela zao wanazotegemea kutumia siku za mwisho ili kuturubuni na tukarubunika.

Natamani uchaguzi ufanyike kesho tupate viongozi wapya wenye mtazamo thabiti na sisi, Mungu ibariki Tanzania

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.