Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetolea ufafanuzi tuhuma zilizoandikwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusu ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mabavu na kufafanua kwamba kilichokuwa kinafanyika, ilikuwa ni kukamata shehena ya vitenge vilivyoingizwa nchini kwa njia ya magendo.

Taarifa iliyotolewa Oktoba 13, 2022 na Idara ya Huduma na Elimu ya Mlipakodi ya TRA imeeleza kuwa asubuhi ya Oktoba 13, 2022 kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, zilitolewa tuhuma kwa serikali kwamba inakusanya kodi kwa kutumia mabavu katika eneo la Kariakoo usiku majira ya saa saba kwa mfanyabiashara aliyefahamika kama mama Kibonge.

Mamlaka hiyo imesema kuwa zoezi lililokuwa linafanyika kwenye stoo za mfanyabiashara huyo, ni ukamataji wa shehena za vitenge zilizoingizwa nchini kwa njia ya magendo.

Kwamba TRA imekuwa ikifuatilia tuhuma zilizokuwa zikitolewa dhidi ya mfanyabiashara huyo za uingizaji wa bidhaaa za vitenge nchini kwa njia za magendo ambapo hivi karibuni, uchunguzi ulibaini kuwa kulikuwa na makontena mawili yenye mizigo ambayo nyaraka zake zilionesha kuwa bidhaa zilizokuwa ndani yake zilikuwa ni mashuka zikielekea Chitipa, Mzuzu nchini Malawi.

Bidhaa hizo hazikuwa mashuka kama nyaraka zilivyoonesha bali zilikuwa ni vitenge vinavyotarajiwa kuingizwa nchini pasipo kulipiwa kodi, zikihusishwa na mfanyabiashara huyo.