Mkoa wa Arusha umeanza kuchukua tahadhari ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kutokana na kuwa na muingiliano mkubwa wa wageni kutoka nchini Uganda kulikoripotiwa kuwa na ugonjwa huo.
Akizungumza na kamati ya afya ya msingi katika kuweka utayari wa kukabiliana nao, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema kuwa tangu ugonjwa huo uripotiwe kuingia nchini Uganda Septemba 20,mwaka huu, zaidi ya wageni 135 kutoka Uganda wameingia nchini Septemba 24 hadi Oktoba 10, mwaka huu.
“Wakati Uganda wanakabiliana na ugonjwa huu lakini wananchi wake wanapenda sana kuja hapa Arusha ambapo kati ya hao 135, wananchi 77 waliishia katika Jiji la Arusha kwa shughuli mbalimbali, hivyo naomba mtambue kuwa Arusha tuko katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huu endapo wahusika wanaokuja wakiwa na maambukizi” amesema Mongela.
Amesema kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa aliyeripotiwa kuambukizwa ugonjwa huo kwa Mkoa wa Arusha, hivyo kuwataka kamati hiyo kufanya kazi Kwa weledi ikiwemo kufanya vipimo Kwa makini kwenye mipaka ya mkoa mzima kujiridhisha wageni wanaoingia hawana dalili za ugonjwa wa Ebola.
“Tumeomba msaada wa Wizara ya Afya juu ya uhitaji wa vifaa hasa vipimo vya kutambua virusi vya ugonjwa wa Ebola na vifaa vitaingia kesho Oktoba 13, hivyo naomba ugonjwa huu msichukulie fursa ya upigaji kwani Serikali kwa sasa inapitia katika kipindi kigumu cha ujenzi wa madarasa lakini inabidi tununue tena vifaa vya tahadhari ya ugonjwa huu” amesema.
Aliwataka kamati hiyo ya msingi kuhakikisha wanafanya kazi Kwa ushirikiano na kutoa taarifa za haraka pindi wanapopata mgonjwa mwenye dalili Ili mkoa uweze kuchukua tahadhari za haraka Kwa kushirikiana na wizara kabla ya kuleta madhara makubwa”
Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa, Dkt.Silvia Mamkwe amesema kuwa mlipuko wa Ebola wanaohofia ni virusi aina ya Sudan ambavyo bado watafiti wa afya nchini hawajapata ufumbuzi wa kinga na tiba yake.
Amesema kuwa idara ya afya mkoa imeshachukua tahadhari mbali mbali za ugonjwa huo ikiwemo wanakamati ya msingi ya afya 122 kupatiwa mafunzo juu ya ugonjwa huo Kuanzia utambuzi wa dalili za ugonjwa, upimaji na tahadhari ya mgonjwa mwenye dalili.
“Tumetenga baadhi ya vituo vya kuchukua tahadhari ikiwemo upimaji na kuhifadhi washukiwa , lakini changamoto kubwa ni vifaa vya upimaji na tahadhari zingine za wahudumu wa afya ,pamoja na gari la kubebea wagonjwa ambapo ziko nane pekee Kwa mkoa wa Arusha” amesema.
Amesema kuwa wamefanikiwa kuunda mfumo maalum wa kiteknolojia inayotumika na madaktari kutoa taarifa na kufika kwa haraka ngazi husika za wanapopata mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola ili nchi iweze kukabiliana kwa haraka huku akiwaomba wananchi kuchukua tahadhari mbali mbali za ugonjwa huo ikiwemo kushikana mikono.
Mamkwe aliiomba ofisi ya mkoa kupata ufumbuzi wa eneo la kuhifadhi wagonjwa watakaoonesha dalili za ugonjwa wa Ebola, Ili kuepuka kusambaa na kuambukiza wengine.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wakuu wa wilaya mkoa wa Arusha, Frank Mwaisumbe amesema kuwa tahadhari hiyo ni muhimu lakini maafisa usalama wanatakiwa kupata kipaumbele baada ya wataalamu wa afya kupata vifaa vya kujikinga.
“Niombe hawa askari wanaolinda vituo vya washukiwa wapatiwe vifaa vya kujikinga Ili wapate nguvu na uhakika wa kumkamata mgonjwa aliye kwenye kituo wasitoroke kwani wanaweza kuogopa kumkamata Kwa hofu ya kuambukizwa, kama walivyokuwa wanaogopa kipindi cha uviko” amesema.
Aidha Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kuzuka katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo April mwaka huu kabla ya kuingia Uganda Septemba 20222.