Na Angel Meela,JamhuriMedia,Arusha

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania pamoja na Taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na Uhifadhi wa Mazingira na Usalama wa Wanyamapori ‘PAMS Foundation’ kinaendesha mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ikiwepo ujangiri na makosa yanayohusiana na hayo kwa wadau wa haki jinai ili kuwawezesha kuendesha ipasavyo mashauri hayo.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tano jana Oktoba 10 2022 yanayofanyika katika ukumbi wa ‘Palace Hotel’ jijini Arusha, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,Dkt. Paul Kihwelo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaleta pamoja wadau wa haki jinai na kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo sheria za kimataifa na kitaifa za wanyamapori na ushahidi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha,  Mhe. Joachim Tiganga akitoa salaam fupi na neno la ukaribisho kwa washiriki wa Mafunzo hayo (hawapo katika picha).

“Mafunzo haya yanatarajia kuwafikia Majaji 15, mahakimu 75, waendesha mashitaka 25 na wapelelezi 25 katika mafunzo kama haya yatakayofanyika sehemu mbalimbali,” amesema Kihwelo.

Jaji Kihwelo amesema kuwa, katika mafunzo hayo watajadiliana kuhusu vitu gani vya kuboresha kwenye upelelezi hadi hatua ya uendeshaji wa mashauri hayo ili waweze kutenda haki na kuongeza kuwa, changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa mashauri hayo ni pamoja na upelelezi na suala la ukusanyaji wa vielelezo.

“Mafunzo haya yana lengo la kuwaleta pamoja wadau wote na hivyo kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Sheria za kimataifa na kitaifa za wanyamapori na ushahidi, uandishi bora wa hukumu, utoaji wa adhabu, utekelezaji wa amri za Mahakama katika mashauri ya wanyamapori, pamoja na upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na makosa yanayohusiana na hayo,” amebainisha Jaji Kihwelo.

Kihwelo ametumia nafasi hiyo pia kumshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, uongozi wa Mahakama pamoja na ‘PAMS Foundation’ kwa ushirikiano ambao wameuonesha tangu kuanza kufanyika kwa mafunzo haya.

Aidha; Mkuu huyo wa Chuo aliongeza kwamba, baada ya mafunzo hayo, anatarajia washiriki watakua bora zaidi na pia watakua wametimiza lengo kwani hiyo ndio fursa pekee ya kujadiliana maeneo yote yenye changamoto.

Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Makosa dhidi ya Wanyamapori wakimsikiliza Mgeni rasmi alipokuwa akitoa hotuba yake ya ufunguzi.

Jaji Kihwelo aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuhusu umuhimu wake na kushiriki kikamilifu huku akimnukuhu Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis kuwa, “Rais Samia Suluhu Hassan alizindua filamu ya ‘Royal Tour’ lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji na watalii, hivyo kama hatutawalinda ile kazi itakuwa ya bure (Royal Tour) na tutakuwa na athari kubwa kiuchumi hivyo jukwaa kama hili litasaidia kulinda rasilimali ili wageni waje na kuingiza fedha za kigeni.”

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mwandamizi na Wakili Mwendesha Mashitaka Kiongozi Mkoa wa Singida, Karen Mrango alisema eneo hilo la wanyamapori kuwa muhimu ni lazima juhudi za wadau zifanyike ili kulinda na kutunza rasilimali zilizopo.

Mafunzo hayo ya siku tano ambayo yamefunguliwa na Mhe. Dkt. Kihwelo ambaye amezindua rasmi mtiririko wa mafunzo ya namna hiyo ambayo yatafanyika pia kwa makundi mengine ya washiriki pamoja na Maafisa wengine, ufunguzi huo umehudhuriwa pia na Bw. Joseph Pande, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka na Maafisa kutoka Mamlaka ya Ngorongoro na TANAPA.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Maafisa wa Mahakama ya Tanzania wakiwemo Majaji na Mahakimu na watumishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na kadhalika.

Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya ‘IJA’ na ‘PAMS Foundation’ ambayo yalisainiwa tarehe 23 Juni, 2022 jijini Dar es Salaam kati ya Mkuu wa Chuo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ‘PAMS Foundation.’