Moyoni nina majonzi. Natumia neno hili kwa vile siamini macho yangu, lakini ndivyo ilivyo. Hili linatokana na kifo cha mwanahabari mwandamizi, Alfred Mbogora. Nilimwona Mbogora siku moja kabla ya kifo chake, lakini zamu hii hakuwa akifahamu kama nilifika kumjulia hali katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini angalau alitikisa mkono na mguu nilipoingia wodini. Hii ilikuwa Ijumaa.
Kabla ya hapo tulikuwa tumezungumza kwa kirefu na Mbogora ofisini kwake pale Baraza la Habari, kwani tulikuwa tukifanya kazi pamoja kuandaa hoja tunduizu ya kuieleza Serikali msimamo wa wadau katika suala la Haki ya Kupata Habari. Nikiri tu, maana najua tangu amefariki alfajiri ya Jumamosi ya Agosti 18 yameandikwa mengi na kunenwa mengi.
Simu ya Wakili Juma Thomas aliyekuwa Tabora, ilinipasua moyo aliponiambia Mbogora amefariki. Mbogora alikuwa mcheshi, mchangamfu na mtu anayetoa msaada kwa yeyote aliyeuhitaji. Nilimfahamu Mbogora siku nyingi kidogo. Mara ya kwanza nilikutana naye mwaka 1997 katika chumba cha habari cha The Guardian Limited. Sitasahau msaada alionipatia wakati huo.
Kwa sasa akiwa katika Baraza la Habari alikuwa akisimamia mafunzo katika kitengo cha kuimarisha maadili ya taaluma ya uandishi wa habari nchini. Hadi siku moja kabla ya kuugua ghafla akiwa safarini kuelekea Bagamoyo, alinipigia simu akinifafanulia jambo juu ya ziara ya Tabora na Kigoma kufanya mafunzo ya Azimio la Dar es Salaam. Sina ujasiri wa kusema mengi juu ya Mbogora zaidi ya kukiri tu kuwa wema hawadumu. ‘Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.’
Wakati ndugu yetu Mbogora akiwa ameaga dunia, nimeona nimuenzi kwa kuwa wiki moja iliyopita nikiwa ofisini kwake pale MCT tuliingia katika mjadala wa kina juu ya mgogoro wa Tanzania na Malawi kuhusu Ziwa Nyasa. Sitaki kurejea mjadala huu, kwani matokeo yake ni habari tuliyoichapisha katika toleo la Jumanne iliyopita, lililochambua kwa kina mgogoro huu.
Nimelazimika kugusia mgogoro huu leo kwa sababu moja tu ya msingi. Nayo si nyingine. Najiuliza iwapo nchi yetu bado inatumia utaratibu wa uwajibikaji wa pamoja. Zamani enzi za Mwalimu Julius Nyerere nchi hii ilikuwa na utaratibu wa uwajibikaji wa pamoja. Kwamba nchi hii ilikuwa Waziri akitamka jambo, basi huo ndiyo msimamo wa Serikali.
Sitaki kutamka yaliyopita katika masuala kama ya uwapo wa Katiba mpya na mengine, ila hili la karibuni si busara kutolisemea. Kwamba Agosti 6, 2012 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisimama bungeni akatoa kauli ya Serikali. Alitamka maneno haya:
“Napenda kuyaonya makampuni yote yanayofanya utafiti kwenye eneo hilo kuanzia leo (Jumatatu) kuacha shughuli za utafiti katika maeneo hayo. Serikali haitaruhusu – narudia – Serikali haitaruhusu utafiti huu kuendelea hadi makubaliano na majadiliano kuhusu mpaka yatakapofikiwa kati ya nchi mbili, yaani Tanzania na Malawi. Let us give diplomacy a chance.
“Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi wote wa eneo la Ziwa Nyasa kuendelea na shughuli zao ziwani na nchi kavu kama kawaida na bila wasiwasi wowote kwa sababu Serikali yao ipo macho, ipo imara, ipo tayari kulinda mipaka ya nchi yetu kwa gharama yoyote.”
Maneno ya Membe yalifuatiwa na kauli za Kaimu Waziri Mkuu, Samuel Sitta, kisha Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa. Wote hawa walitoa msimamo mzito juu ya utayari wa Tanzania kulinda mipaka yake.
Rais Kikwete alipokutana na Rais wa Malawi, Joyce Banda, mjini Maputo kwanza akamwalika kuja hapa kwetu, lakini si hilo tu, akasema: “Yapo maneno yaliyotiwa chumvi na vyombo vya habari, wakidai eti Tanzania inataka kupigana na Malawi, nasema wala hili halijapata kuwa wazo letu.”
Maneno haya ya Kikwete ndiyo yanayoweza kuwa yalilenga kutuliza ghasia, lakini kwa waliomsikiliza Membe wakati akiwasilisha tamko rasmi la Serikali, sitanii wanajiuliza nini maana ya maneno haya.
Sitanii, katika hili nasema tunapaswa kuwa makini kama taifa. Turejee katika utamaduni wa zamani. Kama ni mawaziri na viongozi wengine wanakurupuka, basi tuelezwe. Tujenge utamaduni wa kuwasiliana na kusimamia kauli zetu kama Serikali badala ya kuionyesha jamii kuwa tumeparaganyika. Leo sitaki kusema mengi, ila tusipochukua mkondo huu, nchi yetu itayumba.