Na Willson Malima,JamhuriMedia, Dar

Jeshi la Polisi limetoa taarifa ya ajali ya kipindi cha mwaka 2020 hadi Agosti 2022 ambapo imesema kuwa kwa kipindi hicho kulikuwa na ajali 4589 iliyosababisha jumla ya vifo 3545 na majeruhi 58694.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 6, 2022 na Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani SACP Wilbroad Mutafungwa,wakati akizungumzia taarifa ua usalama barabarani.

Amesema kuwa kati ya ajali hizo 553 zimesababishwa na madereva wa Serikali kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kujihisi wako juu ya sheria,kujiamini kupita kiasi na kushindwa kuheshimu sheria za usalama barabarani,kujihisi sheria haziwahusu, kujivika ukuu wa viongozi wao.

Pia baadhi ya viongozi wa Serikali kujtojitambua juu ya dhamana waliyonayo kwa vyombo vya umma walivyokabidhiwa hususan magari na kukosa utashi na uelewa juu ya sheria za usalama barabarani kwa kutumia vibaya madaraka yao wakidhani wapo juu ya sheria kwa kuwapa kiburi madereva wao na kushindwa kukemea makosa hatarishi kama mwendokasi na kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.

Pia ameongeza kuwa sababu zilizochangia kupungua kwa ajali kuanzia 2020, 2021 na Januari hadi Agosti 2022 ni elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa serikali imewafikia kwa kiasi kikubwa ingawa bado kuna baadhi ya taasisi na idara za Serikali hawatoi ushirikiano wa kutosha katika wajibu huo wa elimu kwa madereva wa magari ya serikali na msako na ukamataji wa madereva wa magari ya serikali wasiotii na kueshimu sheria.

Mutafungwa ametoa wito kwa madereva wa magari ya Serikali kujitambua kuwa hawako juu ya sheria na wanapaswa kutii sheria kama madereva wengine wote pia wana dhamana na maisha ya viongozi wao na mali za umma.

Pia ametaka elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa serikali iendelee kutolewa kwa kuwajengea uwezo wa kujitambua kama watumishi wa umma wanaopaswa kulinda uhai wao na wateja wao kwa kuheshimu na kutii sheria.

“Dereva wa serikali anapaswa kuwa mtulivu na mwenye kujitambua kwani taaluma ya udereva inahitaji utulivu kwa kuwa inabeba dhamana ya maisha ya watu na dereva hapaswi kuwa na mihemko na anatakiwa kujiepusha na makandokando yanayoweza kupelekea kupoteza uweledi katika kazi zake,” amesema.

“Sheria ziko wazi na ninyi mnazijua lakini kuna kitu kinaitwa kujiamini kupita kiasi (Over Confidence) na kushindwa kuheshimu Sheria za Usalama barabarani na Kanuni zake. Hamuheshimu ishara, michoro na alama (kif.73 (2) (3) (4)) pamoja na maelekezo yanayotolewa na askari wa usalama barabarani.

KIPINDI CHA MWAKA 2020

Ajali zote zilikuwa 1,714 na katika hizo ajali 260 zilikuwa za magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 15.2 ya jumla ya ajali zote Nchini. Vifo vyote vilikuwa 1,260 na katika vifo hivyo, Vifo 82 vilitokana na magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 6.5 ya jumla ya Vifo vyote.

Majeruhi wote walikuwa 2,117 na katika Majeruhi hao,majeruhi 184 walitokana na magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 8.7 ya jumla ya Majeruhi

KIPINDI CHA MWAKA 2021

Ajali zote zilikuwa 1,698 na katika hizo ajali 158 zilitokana na magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 9.3 ya jumla ya ajali zote. Vifo vyote vilikuwa 1,245 na katika vifo hivyo, Vifo 94 vilitokana na ajali za magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia
7.6 ya jumla ya Vifo vyote.

Majeruhi wote walikuwa 2,032 na katika Majeruhi hao, Majeruhi 250 walitokana na ajali za magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 12.4 ya jumla Majeruhi wote.

KIPINDI CHA JANUARI 2022 HADI AGOSTI 2022

Ajali zilikuwa 1,177 na katika hizo, ajali 135 zilitokana ni ajali za magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 11.5 ya jumla ya ajali zote.

Vifo vyote vilikuwa 1,038 na katika vifo hivyo, Vifo 90 vilitokana na ajali za magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 8.7 ya jumla ya Vifo vyote, na Majeruhi wote walikuwa 1,556 na katika Majeruhi hao, Majeruhi 211 walitokana na magari ya Serikali, ambapo magari ya Serikali yalichangia kwa asilimia 13.6 ya jumla Majeruhi wote.