Leo nimeona vyema niandike makala hii kugusia suala la Katiba Inayopendekezwa (mpya). Nimeamua kugusia suala la Katiba Mpya, baada ya kuona Chama Cha Mapinduzi (CCM) suala hili kwenye Ilani yao wameliacha kama fumbo la imani, hawaligusi, huku Ukawa wakisema watahakikisha inapatikana Katiba Mpya.
Kabla sijazungumzia kwa kina suala la Katiba mpya, niseme nimefuatilia kwa karibu mchakato na utartibu wa kuzindua kampeni za vyama vya siasa. Nimefuatilia uzinduzi wa CCM, nimefuatilia uzinduzi wa CHADEMA/UKAWA na ACT-Wazalendo. Nasema, sijafurahishwa na ratiba za vyama vya siasa wakati wa kampeni zao.
Sitanii, vyama hivi vitatu nilivyovitaja hakuna chama hata kimoja kilichotenga angalau muda wa saa moja kuzungumza sera za vyama zilizopo kwenye Ilani zao za uchaguzi. Vyama vimejaza wasanii, wapiga vijembe, na watoa hotuba zisizohusiana na Ilani. Wagombea wanaanza kuhutubia zikiwa zimesalia dakika 20, hivyo wanakosa muda wa kunadi sera zao.
Nilimshuhudia mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli, alipewa fursa ya kuzungumzia sera za chama chake ikiwa zimesalia Dk. 20. Dk. Magufuli alilazimika kuhutubia hadi saa 12:36, na ukiangalia jinsi mambo yalivyokuwa yanakwenda na kasi aliyokuwa anaitumia basi unaona kuwa muda haukumtosha Magufuli kunadi sera zake.
Alipokuja mgombea wa CHADEMA/UKAWA, Edward Lowassa zilikuwa zimesalia dakika 16. Katika hali ya kukimbizana na muda, akalazimika kusema hotuba yake ipo kwenye mtandao wa CHADEMA, na kwamba polisi wangepambana naye iwapo angezidisha muda. Binafsi nadhani kama ni ukosefu wa muda waliosababisha ni wao CHADEMA.
Walijua fika kuwa mgombea anayo hotuba iliyohitaji saa zaidi ya 1 kufafanua sera zao, lakini hata Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema mara kadhaa kuwa muda ulikuwa ukiwaacha. Binafsi nasisitiza kuwa hili si sahihi. Walipaswa kuanza mbwembwe mapema na kumalizia na sera kuanzia saa 8 mchana. Mgombea wa ACT alibakiziwa dakika 23.
Sitanii, kimenishangaza chama cha ACT-Wazalendo. Nilitaraji Prof. Kitila Mkumbo achambue sera za chama chake, lakini naye kama wanasiasa wengine akatumbukia katika mkumbo wa kushambulia vyama vya upinzani kwa mafumbo. Wazungumzaji karibu wote wa ACT walifanya kazi ya kutukana wapinzani wenzao badala ya kueleza wakiingia madarakani watafanya nini.
Narudia, matarajio yangu ni kuwa vyama vitarekebisha hali hii. Vitapanga ratiba zao kueleza sera zaidi badala ya burudani za wanamuziki. Wagombea watatoa fursa za kuulizwa maswali na wananchi na kufafanua sera zao kwa umakini na kujibu dukuduku za wananchi. Bila kufanya hivyo, nchi yetu itaishia kuchagua viongozi kutokana na burudani za majukwaani, ila maendeleo milele hatutayaona.
Kingozi wa ACT, Zitto Kabwe ameonyesha ukomavu mkubwa. Ameomba radhi kwa mpigadebe wao kuanza kutaja wagombea wengine kuwa wanaumwa kifafa na magonjwa yasiyofahamika. Suala la afya milele si la kufanyia mzaha. Sisi sote ni walemavu watarajiwa, ikiwa yupo anayeamini hawezi kuugua au kupata ulemavu anipigie na kunijulisha hilo. Muhimu hapa ni kueleza sera na mikakati ya kuondoa matatizo yanayowakabili Watanzania.
Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema “CCM, Ukawa hawawezi Katiba Mpya”. Nafahamu kadri muda utakavyokwenda na kampeni kupamba moto, hoja ya Katiba mpya itazungumzwa kwa kina. Vyama vyote vya siasa vitataka kuonyesha kuwa wao watategua kitendawili hiki. CCM wameanza kuikimbia Katiba Inayopendekezwa.
Hatujasikia hadi leo Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akirejea tena kauli yake kuwa kura ya maoni itafanyika mwaka huu. Ukawa kwa upande wao wanasema: “Tutasimamia Katiba mpya inayolinda haki za msingi za wananchi na kuweka bayana mipaka ya madaraka ya serikali na viongozi, Bunge na Mahakama.”
Nilipata kulisema hili, na leo ninalizungumza kisheria zaidi. Mchakato wa Katiba mpya ulikuwa batili tangu mwanzo. Chama tawala kilipaswa kufuata mkondo wa kisheria kuhalalisha mchakato wa Katiba Inayopendekezwa. Hapa namaanisha nini? Katiba ya Tanzania ya sasa hairuhusu kuifuta. Haina ibara yoyote inayoruhusu kufutwa kwake, isipokuwa kurekebishwa.
Ibara ya 98 ya Katiba ya Tanzania inasema: “98 (1) Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata Kanuni zifuatazo:-
“(a) Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b) ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa katika Orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote;
“(b) Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya Sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni wa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.
“(2) Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (1) kubadilisha masharti ya Katiba hii au masharti ya sheria maana yake ifahamike kuwa ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti haya au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo.”
Sitanii, ukisoma kwa umakini ibara hii inayolipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria na kuirekebisha Katiba iliyopo, ni wazi kuwa hakuna ibara yoyote inayoruhusu Bunge au Serikali kuifuta katiba hii. Kwa kutumia Ibara ya 98(1), Serikali ilipaswa kwanza kupeleka bungeni muswada ukatamka maneno yenye kuonyesha utaratibu wa kuifuta Katiba iliyopo iwapo kuna haja ya kufanya hivyo.
Iwapo masharti ya kuibadili Katiba yanataka wabunge theluthi mbili kutoka Bara na Zanzibar wapige kura kupinga au kuridhia kubadilishwa kwa ibara, inakuwaje suala la kuifuta kabisa Katiba hii? Kwa mantiki hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, imekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sheria hii ilianzisha mchakato wa kuifuta Katiba ya mwaka 1977, wakati hakuna ibara yoyote inayoruhusu kufutwa kwa Katiba iliyopo. Kuepuka mtego huu, Serikali ilipaswa kupeleka kwanza muswada bungeni wakabadilisha ibara ya 98 na kuongeza maneno yenye kuruhusu utaratibu wa kuifuta Katiba hii.
Kwa hali ilivyo sasa, kabla ya kubadili Ibara hii ya 98 kuruhusu ufutwaji wa Katiba, hata ikitipishwa Katiba Inayopendekezwa bado akitokea mtu akaenda mahakamani akafungua kesi kwa kutumia Ibara ya 64(5) ya Katiba ya Tanzania, mchakato wote huu utafutwa.
Ibara ya 64(5) inasema: “Bila ya kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba hii kuhusu mambo yote ya Tanzania Zanzibar yasiyo Mambo ya Muungano, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba itakuwa batili.”
Kwa mantiki hiyo, kwa kuwa hakuna kifungu chochote ndani ya Katiba ya sasa kinachoruhusu kufutwa kwa Katiba hii, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayoanzisha mchakato wa kuifuta Katiba hii na kutunga Katiba mpya, basi inavunja si tu Ibara ya 98 bali Katiba nzima kwani hakuna sehemu inayoruhusu kuifuta.
Sitanii, hata hiyo Katiba Inayopendekezwa haina ibara inayoruhusu kufutwa kwake. Kwa mantiki hiyo, tukiruhusu mchezo wa kila anayeata ndoto kufuta Katiba ya nchi yetu, mwisho wa siku tutajikuja Tanzania inakuwa taifa la kuandika Katiba kila uongozi unapoingia madarakani.
Kwa heshima ya utawala wa sheria, naomba tukubali tu kuwa kwa kila hali Katiba Inayopendekezwa imeshindikana. Tusiangalie suala la gharama. Tukianza kuvunja Katiba kwa kisingizio cha gharama, mwisho wa siku tutaacha kuiheshimu kabisa.
Katika hili nasema hapana. Tulipofikia tufunge breki. Bunge letu lijalo libadili Katiba kwanza kuruhusu kufutwa kwa Katiba hii, kisha mchakato wa kutunga Katiba mpya uanze. Navishauri vyama vya siasa katika kampeni hizi vieleze sera, badala ya matusi. Tujadili tutakavyowaondoa Watanzania katika umaskini na si vinginevyo. Tukutane wiki ijayo.