Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Geita
Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Shahende mkoani Geita, Helena Mashaka (13), ameshindwa kutimiza ndoto zake baada ya mama yake mzazi kumchoma moto mikono kwa tuhuma za kuiba sh.30,000.
Edgar Michael ni mtendaji wa kijiji Bukoli amesema kuwa tukio hilo limetokea katika Kata ya Butobela, mkoani Geita, majira ya saa 2 asubuhi, baada ya mama yake kumtuhumu kuiba kiasi hicho cha fedha.
Amesema alipata taarifa ya mtoto huyo kujeruhiwa kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo akidai kuwa kuna binti amechomwa moto na mama yake na kushindwa kufanya mitihani.
Mwenyekiti huyo alianza kumfuatilia mzazi wa binti huyo na kisha kumkamata na kudai alifanya kitendo hicho kwa sababu mtoto huyo aliiba sh. 30,000.
“Mpaka sasa mzazi huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo kidogo cha Polisi kilichopo Kata ya Bukoli, na mwanafunzi amepelekwa Zahanati ya Bukoli kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Aidha mtendaji huyo amesema taratibu zinaendelea ili mwanafunzi huyo aweze kupata nafasi ya kurudia kufanya mitihani hiyo ya kuhitimu kwa mwaka 2023.