Dk. John Magufuli, ameshaanza kampeni kwa ajili ya kuingia Ikulu ifikapo Oktoba, mwaka huu. Kwa kuwa ameshaanza kampeni, wengi wamesikia nini anachokusudia kuifanyia Tanzania na Watanzania.
Hadi naandika makala hii, “mtani wa jadi” wa Dk. John Magufuli kwenye mchuano huu wa urais, Edward Lowassa, na Chadema kwa jumla walikuwa hawajaweka hadharani Ilani yao. Kwa sababu hiyo, nimeona nijadili hiki kilichokwishasikika kutoka katika Ilani ya CCM, na hasa maneno yaliyozungumzwa na Dk. Magufuli.
Kwa waliomsikiliza, hitimisho wanalopata ni kwamba wananchi wajiandae kuiona Tanzania mpya chini ya uongozi wenye viwango vinavyoliliwa na Watanzania wengi.
Najua kauli hii si rahisi kuwaaingia Watanzania wengi hasa wale walioaminishwa ujio wa “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania”. Pengine ni kwa kulitambua hilo, tangu awali kabisa Dk. Magufuli amewaambia Watanzania: “Sitowaangusha”.
Tena basi, akiwa mkoani Mbeya amesema kwamba hakuna ulazima wowote kwa wananchi kufanya mabadiliko ya kuiweka kando CCM. Imani yake ni kwamba mabadiliko ndani ya chama hicho na Serikali yake yanawezekana kabisa yakafanywa bila kukiondoa madarakani. Akatoa mfano wa Chama kinachotawala China ambacho kwa miongo yote kimeongoza Taifa hilo na kufanya mabadiliko makubwa ya kiitikadi na kiuchumi. Kwa maneno mengine, chama hicho kimeweza kujibadili kulingana na wakati na mahitaji ya wakati.
Matamanio ya Dk. Magufuli, ni kuona CCM inazaliwa upya na kwa hiyo inakuwa na Serikali yenye kukidhi mahitaji na matamanio ya walio wengi. Amewahakikishia Watanzania kwamba kazi hiyo anaiweza na kuwa kinachotakiwa ni yeye kupewa ridhaa ya kuingia Ikulu ili aonyeshe kwa vitendo.
Dk. Magufuli tayari ameshaonyesha wazi wazi kupingana na baadhi ya mambo yanayoendeshwa kimazoea ndani ya Serikali. Kwa mfano, amesema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na Wiki ya Maji kama wananchi hawapati maji safi na salama. Tayari ameshauona mpango huo hauna tija; na kwa ahadi yake ni kwamba endapo atashinda na kuapishwa, basi wananchi watarajie kupata maji badala ya Wiki ya Maji! Ametoa kauli kama hiyo kwenye “wiki” za kila aina ambazo maadhimisho yake ni mianya ya kuwatengenezea ulaji baadhi ya watumishi na viongozi.
Dk. Magufuli amekuwapo serikalini kwa miaka 20. Muda huo unamtosha kujua wapi serikali imefeli, sababu za kufeli na sasa afanye nini kuondoa kufeli huko. Watendaji wenye masikio, hasa katika sekta za umma wanapaswa kujiandaa kisaikolojia kwa ajili ya ku-fit kwenye uongozi wa Dk. Magufuli. Lakini sekta ya umma haiwezi kuwa na nguvu kama sekta binafsi nayo itaendelea kufanya mambo kwa mazoea au kwa ujanja ujanja.
Wale waliozoea kukwepa kodi watambue kuwa wana muda wa mwezi mmoja au miwili hivi ya kubadilika ili waweze kuendana na mabadiliko yanayoahidiwa na Dk. Magufuli.
Mgombea huyu ameshasema mengi, na kwa kweli sidhani kama yatakuwapo mengine ya kuyazidi yale aliyoyasema Jangwani wakati wa uzinduzi wa kampeni na haya anayoendelea kuyazungumza kwenye mikutano yake ya hadhara.
Watanzania wanahitaji mabadiliko makubwa kwenye sekta nyingi. Wanahitaji mabadiliko kwenye suala zima la uchumi na maendeleo yao. Wanataka kuona utendaji kazi katika ofisi zote – za umma na za binafsi – ukibadilika na kuwa wenye tija na manufaa kwa watumishi wenyewe na kwa nchi. Wezi na wahujumu ameshawaonya. Kwa wanaomjua vema Dk. Magufuli, haya anayoyasema si ya kuchangamsha baraza! Amedhamiria kweli.
Si vema kupuuza mabadiliko ambayo yameanza kuonekana kwenye baadhi ya ofisi za umma. Yapo mabadiliko mazuri. Utendaji kazi wa baadhi ya watumishi kadhaa sasa ni wa kuridhisha, hasa baada ya kushamiri kwa matumizi ya kompyuta katika masuala mbalimbali. Tunahitaji kiongozi wa kujenga mfumo wa kututoa hapa tulipo na kwenda mbele zaidi. Dk. Magufuli ameshasema hilo analimudu; na kwa kurejea rekodi yake ya utendaji kazi kauli zake haziwezi kutiliwa shaka.
Lakini kama kuna jambo lililowavutia wengi wiki ya kwanza ya kampeni za mgombea huyo, ni pale aliposema Serikali inachukiwa kutokana na utendaji kazi mbovu wa baadhi ya watumishi wa umma. Akaahidi kuanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia wezi na mafisadi wa mali za umma.
Ahadi hii ni nzuri, lakini shaka ni kwamba hapo kwenye Mahakama nguvu au msukumo wa kisiasa pekee unaweza usilete mabadiliko haraka. Lakini kwa kuwa rais ni mkuu wa nchi, inawezekana kabisa hilo ameliona na dawa yake inachemka.
Wiki kadhaa zilizopita nilijaribu kueleza kwa ufupi baadhi ya matarajio ya wananchi kwa rais ajaye. Kwa bahati nzuri Dk. Magufuli, ameshayazungumza baadhi ya matarajio hayo.
Wananchi wangependa kuona rais ajaye anaifanya taasisi ya urais kuwa taasisi ya urais kweli kweli. Wanataka kuiona Ikulu ikirejeshwa kuwa ofisi yenye kusimamia na kusukuma utendaji kazi badala ya kuwa mahali pa kupokea watu wenye malalamiko ambayo yangeweza kutatuliwa hata na watendaji wa vitongoji!
Aifanye Ikulu iwe mahali ambako endapo mtu atafika kulalamika jambo fulani, basi huko alikotoka kama ni kwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa, ahesabu kuwa hana kazi kwa kushindwa au kupuuza kulimaliza.
Tangu aanze kampeni kwa wiki moja sasa, Dk. Magufuli hajaonekana akiwa na mkewe katika majukwaa. Wapo wanaoweza kuhoji mapenzi yake kwa familia, lakini anachokifanya mgombea huyu ni kuonyesha kuwa anatafuta kazi ya kuwatumikia Watanzania, na si kazi ya kusaka umaarufu wa familia yake. Mama Janeth, haonekani majukwaani, si kwa bahati mbaya, pengine ni kwa familia hiyo kutambua kuwa ofisi inayotafutwa na mumewe ni ofisi ya Watanzania kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.
Bila shaka wakati utafika wa yeye kuonekana jukwaani ili aweze kuongeza mvuto wa kuzipata kura za kina mama. Hata hivyo, matarajio ya wengi ni kuona uwepo wake jukwaani haupitilizi.
Hivi karibuni tumeona taasisi ya urais ikihusisha familia ya rais, kiasi cha kumuona mama akiwa na msafara wenye magari mengi, pikipiki na ving’ora. Tumewaona baadhi ya watoto kwenye taasisi hiyo wakitamba kwa ulinzi na mbwembwe nyingine nyingi.
Wapo wananchi wanaohoji utitiri huo wa magari, ving’ora na ulinzi. Wanajiuliza, kuna hofu gani hata waweze kujihami namna hiyo?
Wananchi wanataka kuona taasisi ya urais ikibaki na heshima yake. Kwa miaka ya karibuni tumeshuhudia wakuu wa wilaya na hata mikoa wakisoma taarifa za maendeleo kwa mke wa rais! Wananchi wanajiuliza, mke wa rais ni nani hata aweze kupokewa na viongozi wa mkoa na hata asomewe ripoti ya maendeleo ya mkoa? Kwenye mtiririko wa uongozi, mke wa rais anaingia na kutokea kipengele kipi?
Watanzania wanataka kuona hatua zikichukuliwa dhidi ya wezi na wahujumu uchumi. Wanatambua kuwa zipo tuhuma ambazo si rahisi kuzithibitisha mahakamani, lakini rais kwa kutumia mamlaka aliyonayo, bado anaweza kumwajibisha Katibu Mkuu, Waziri, Mkurugenzi au mtendaji yeyote anayemmudu kisheria na kikatiba.
Kwa miaka ya karibuni vyombo vya habari, hasa magazeti, vimeandika habari nyingi mno zikiwahusu mawaziri wezi na wahujumu uchumi. Rais hakuthubutu kuchukua hatua hata kidogo. Matokeo yake ameendelea kuwanyamazia wezi na wahujumu uchumi ndani ya Baraza la Mawaziri. Hakuonyesha kuguswa hata kidogo. Wameshiriki kufanya hujuma nyingi kwa uchumi wa nchi yetu. Wamezitumia rasilimali za umma kwa manufaa yao. Watanzania wanayasoma haya mambo, wanayaelewa na kwa kweli wanapoona kiongozi mkuu wa nchi akiyafumbia macho wanaumia. Dk. Magufuli akiona kuna sehemu anapata wakati mgumu kidogo kupata kura atambue kuwa ugumu huo umesababishwa na mambo ya aina hii.
Dk. Magufuli amewaambia Watanzania kuwa hana deni, kwa maana hakubebwa kwa fadhila za wafadhili au makundi hadi hapo alipofika, na kwamba endapo ataingia Ikulu, hatakwazwa na ulipaji fadhila. Haya ni maneno mazuri na ya matumaini makubwa kwa Watanzania.
Mara zote Dk. Magufuli amesema atawatumikia Watanzania wote bila ubaguzi. Anasema atawatumia CCM, Chadema, CUF, TLP, NCCR-Mageuzi na wengine wa vyama vyote vya siasa katika kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo. Hii ni ahadi nzuri inayoakisi upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania. Kwa haya aliyoyazungumza Dk. Magufuli, utaona wazi kuwa endapo ataingia Ikulu, Watanzania watarajie kuiona Tanzania mpya yenye uwajibikaji wa hali ya juu. Kwa kuwa mgombea wa Ukawa naye ameshaanza kunadi sera zake, bila shaka nitakuwa na muda wa kumjadili hapa. Uchaguzi utakaotawaliwa na amani ndiyo zawadi pekee muhimu ambayo wagombea na mashabiki wote wanapaswa kuizawadia Tanzania na Watanzania.