Hivi sasa tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu na kila mwananchi anataka kutumia haki yake ya kimsingi kupiga kura na kumchagua kiongozi anayeona atafaa kumwongoza na kumletea maendeleo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Viongozi wamefanyiwa mchakato ndani ya vyama vyao na wamejiridhisha kuwa wanatosha katika kuisimamia Ilani yao ya Uchaguzi pamoja na kutekeleza kile ambacho wamekipanga kwa manufaa ya wananchi ambao watawaongoza.

Pasi na shaka kila chama kina mbinu mbadala kwa ajili ya kuuza sera zake kwa wananchi ambao ndiyo wapigakura ifikapo muda wa kutumia hicho kilichobatizwa kwa jina la kikatio, sina shaka sana na nchi yetu ambayo imebarikiwa kuwa na amani na kwamba hili litafanyika kwa utulivu na hatimaye kukubaliana na matokeo yatakayotangazwa na tume inayohusika.

Leo katika waraka wangu nimeguswa na mambo mengi. Awali ni hadaa baina ya wananchi wenyewe kwa wenyewe na pili viongozi mbalimbali katika ngazi mbalimbali wanavyojinasibu na kujipa ushindi kabla ya kupigiwa kura, hili si jambo jema kwa sasa kwa sababu ikiwa unajihakikishia ushindi na ikiwa ushindi hautapatikana itakuwaje. 

Yapo mambo mengi yanayotamkwa na watamkaji hadi unaona kichefuchefu, kwani suala la kupiga kura ni la jamii nzima au mtu mmojammoja? Mbona tunavurugana? Nilidhani kipindi hiki ni cha kusikiliza sera na kuacha kuchanganyana na watu wa kuwapigia kura ili watuongoze kwa awamu mpya.

Nilidhani ni wakati mzuri wa kufanya upembuzi yakinifu wa vyama na siyo watu, nilidhani ni kipindi cha kutofikiria huyu ni mtu wangu au yule siyo mtu wangu, nilidhani ni kipindi cha kutafakari tulikuwa wapi, tuko wapi na tuna mpango wa kwenda wapi.

Haya yote ni mawazo yangu ambayo nadhani ndiyo yenye tija kwa mfumo wa siasa na nchi yetu, si wakati wa kuanza kufikiria kuwa huyu ni kabila langu, huyu ni ndugu yangu, huyu ni mtu wa kwetu, huyu ni jirani yangu, huyu ni rafiki yangu, huyu tunakaa naye mtaa mmoja na kadhalika.

Yapo mengi ambayo nayaona yanakinzana na utawala bora ambao kama tunahitaji mabadiliko ya kweli katika maendeleo sisi kama waajiri wao hawa wanasiasa,s tunapaswa kuyafahamu na kuyafanya pasi na kuyumbishwa na sifa au ushabiki wa kisiasa.

Tunatakiwa kuwachagua viongozi kwa faida ya miaka mitano na siyo faida ya siku moja, tunatakiwa kuangalia maslahi ya kizazi chetu na kizazi kijacho, tunatakiwa kujipambanua viwango vya uelewa wa sasa na zamani, sisi tuna miaka hamsini sasa tangu tupate uhuru, ni lazima baadhi ya mambo yatakwenda kiuhalisia zaidi na matakwa ya dunia ya leo tofauti na Tanganyika yetu.

Leo naandika barua hii baada ya kushuhudia vibweka vinavyoanza vya kisiasa katika vinyang’anyiro mbalimbali vya nafasi ya kuongoza Taifa letu, nawaona madiwani wakichukua nafasi ya wabunge na wabunge wakijinasibu kwa nafasi za urais. Hii Tanzania ya siasa za namna hiyo siyo ninayoifahamu mimi Tanganyika ile ya demokrasia ya mpigakura ya ndio au hapana.

Naandika barua hii nikitoa tahadhari kwa wapigakura, mashabiki, wanachama wa vyama vyote kufanya upembuzi yakinifu kabla ya kutoa ushindi kwa chama fulani na baadaye kuanza kulalamika kwamba hayakuwa matarajio yao.

Uamuzi wa kumuweka kiongozi si jambo la kishabiki, sijambo la kupokea rushwa na kuridhika kuuza kura yako, si jambo la kusikia umbeya na kuamua kutoa uamuzi, si jambo la kifamilia, si jambo la kiitikadi na siyo la kikabila wala kanda. Hii ni Tanzania yetu sote kwa manufaa yetu sote.

Ningelipenda siku ambayo tume wanawatangaza washindi iwe siku ya kupongezana na kupeana moyo wa kuiendeleza Tanzania mpya, Tanzania ya mfano Afrika, Tanzania ya ukombozi, Tanzania ya amani, Tanzania ya sura ya kipekee huko Magharibi yetu.

Ningelipenda tume itangaze na kusiwe na malalamiko ambayo yataleta ufa katika amani tuliyonayo, ningelipenda tume itende haki bila kujali huyu ni nani kwa maana ya kumtazama usoni lakini itazame chama na wanachama, ningelipenda tume itende haki hadi katika ngazi ya madiwani ili nchi yetu ibaki kuwa ya amani na umoja, tofauti ya vyama isitugawanye na kusababisha uvunjifu wa amani.

Wiki ijayo nitatoa ushauri wa bure kwa viongozi wetu tutakaowachagua,

 

Wasalaam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.