Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Bodi ya Filamu Tanzania imeunda kamati maalum ya kuhamasisha Watanzania kurejesha utamaduni wa kuangalia filamu katika kumbi za sinema.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo, Dkt. Kiagho Kilonzo leo Jumanne Oktoba 4, 2022 wakati akielezea utekelezaji wa shughuli za bodi na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka 2022/2023.

Kilonzo amesema hivi sasa Tanzania kuna kumbi tisa ambazo ziko katika mikoa ya Mwanza,Tanga,Dodoma,Dar es Salaam na kwamba Serikali haiwezi kuhamasisha uwekezaji katika eneo hilo bila kuongeza idadi ya watu wanaokwenda kwenye kumbi hizo.

“Tumeunda kamati maalumu ya kuhamasisha Watanzania kurejesha utamaduni wa kuangalia filamu katika kumbi za sinema na hivi sasa kuna kumbi tisa,” amesema.

Ameongeza kuwa pia katika kuhakikisha utaratibu wa uendeshaji unakuwepo tumeanza uhakiki wa vibanda vya kuonyeshea filamu maarufu vibanda umiza vilivyopo mtaani lengo ni kuvisajili.

Aidha, Dk Kilonzo amesema kwa kupitia Kamati ya Kutetea Haki za Wasanii wamefanikiwa kurejesha Sh.milioni 300 kwa wasanii akiwemo marehemu King Majuto ambazo walidhulumiwa kutokana na mikataba mibovu.

Amesema pia bodi inaratibu kamati maalumu ya kutetea haki za wasanii ambapo malalamiko 22 yamesuluhishwa huku nane yapo katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa.