*Asema zilikuwa mbinu za majadiliano, ataja tishio la Acacia
*Afafanua suala hilo limekwisha,atamtafuta Mwigulu amweleze
Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Mpatanishi Mkuu wa Serikali (Chief Government Negotiator), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema Dola bilioni 190 za Marekani sawa na Sh trilioni 360 walizotakiwa kulipa Kampuni ya Acacia Julai, 2017 kama kodi, malimbikizo na faini ya ukwepaji kodi, hakikuwa kiwango sahihi.
Kabudi, aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mpatanishi Mkuu wa Serikali baada ya kutenguliwa uwaziri wa Katiba na Sheria, Januari, 2022 ameliambia Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa serikali ilifahamu tangu mwanzo kuwa kiwango hicho cha Dola bilioni 190 ambazo wakati huo zilikuwa sawa na Sh trilioni 360 kilikuwa hakilipiki.
“Jamani mtu yeyote anayejua, ile haikuwa kodi halali, ilikuwa ni kodi inayobishaniwa. Kwani watu wangapi mmetoa ‘assessment’ (makadirio) ya kodi halafu mnakaa chini? Sasa nikasema siku nyingine nikipata nafasi na nikipata ruhusa, nita-share na wewe, na siyo siri, kwa sababu hata sasa wamekwishalipa ile installment (mkupuo) ya pili ya zile milioni 300.
“Lakini kuna faida nyingine nyingi ambazo tuliingia nazo kwenye mkataba… na ule mkataba sikusaini mimi, ulisainiwa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko, mimi nilichokuwa nimekisaini kilikuwa kinaitwa Agreement of Undertaking (Makubaliano ya Utekelezaji), lakini yote, ningependa siku moja nikupe details (taarifa) zote kwa sababu ule mkataba siyo siri. Mimi nasoma JAMHURI kila siku,” amesema.
Amesema kati ya mambo ambayo nchi imeyapoteza katika Kiswahili ni uandishi wa kutumia lugha ya Kiswahili nchini, ila utaalamu huo umesalia katika JAMHURI.
“Unajua bahati mbaya nilikuwa nasema hata leo, tumepoteza ladha ya uandishi wa Kiswahili, sasa miongoni mwa watu ninaopenda kusoma ni safu ya SITANII [unayoandika Balile], sasa mtu ambaye hajajua tamathali atasema, ‘huyu anaandika nini?’
“Lakini mimi ninachokipenda ni ile aina ya lugha, kwa hiyo nashukuru na nikija Dar es Salaam nitakutafuta ili tukamilishane mawazo katika mambo yatakayotusaidia kujenga. Lakini mambo mengine mimi hapana, kwa sababu ni vizuri kuona watu wanavyotafsiri vitu.
“Namtafuta Mwigulu (Waziri wa Fedha) nimwambie kuwa ile ilikuwa ni kodi inayobishaniwa. Na wao pia walitupeleka kwenye ICSD (Kituo cha Kimataifa cha Kusuluhisha Migogoro) na wenzetu wakawa wanasema mtashitakiwa, mtafilisiwa.
“Unajua hizo trilioni zilipigwa baada ya wao kuwa wamepeleka mashitaka makubwa ICSD ya kudai close to two billion US dollars (karibu dola bilioni 2 za Marekani), sasa vitu vingine huwezi kuvieleza kwa sababu hizo ni mbinu za negotiations (upatanishi). Ukivieleza utavuruga, lakini ulichosema ni kweli… wewe hiyo kodi utaitoa wapi? Inazidi GDP za nchi zote, halafu nikasema huyu bwana kweli hatanii,” amesema Kabudi.
Amesema tangu mwanzo walijua kuwa kiasi hiki hakilipiki ila walitumia kiwango hicho kama mbinu za majadiliano na upatanishi.
Ameliambia JAMHURI kuwa kwa vyovyote iwavyo, katika mgogoro kati ya Acacia na serikali, Tanzania iliibuka na ushindi na kwa masilahi mapana ya biashara hata Acacia walipata ushindi kwa kufanya biashara inayokubalika kwa pande zote mbili.
“Mimi nasoma JAMHURI kila ikitoka, sasa huko nyuma uliandika kitu nikakaa kimya, lakini cha jana nimekisomaa, nikatafakari, nikasema hebu nirudi kwa Balile niongee naye,” amesema Kabudi.
Amesema kabla ya mgogoro huu, Tanzania haikuwahi kupata kitita cha Dola milioni 300 sawa na Sh bilioni 700, ambapo Acacia mwaka 2019 walitoa Dola milioni 100 kwa mpigo na wameendelea kutoa gawio mwaka hadi mwaka bila kuacha.
Huku akisisitiza kuwa hata mwaka huu serikali imepokea fedha nzuri tu kutoka kwenye madini, akaongeza kuwa nchi imepata hisa asilimia 16, inapata mgawo wa asilimia 50 ya faida inayopata Kampuni ya Twiga ambayo ni tanzu, inayomilikiwa kwa ubia kati ya Tanzania (asilimia 16) na Barrick (asilimia 84), uwazi umeongezeka kila kinachofanywa kinaonekana.
Ameongeza kuwa kuna faida kubwa na Tanzania imekuwa mfano kwa mataifa mengi ya Afrika ambayo sasa yanaiga.
Kabudi amesisitiza kuwa mgogoro wa Acacia/Barrick ulikwisha Oktoba, 2019, hivyo waliruhusiwa kusafirisha makinikia yaliyokuwa yamezuiwa bandarini, wakaanza kulipa kodi kwa mujibu wa makubaliano na deni la Dola bilioni 190 likafutwa katika vitabu vya serikali.
Kati ya fedha hizo, Dola bilioni 40 zilitajwa kuwa ni kodi iliyokwepwa na Dola bilioni 150 zilitajwa kuwa ni faini, malimbikizo na riba ya kukwepa kodi tangu mwaka 2000.
Katika kinachoonekana kuwa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, ana hoja mahususi aliyoishikilia, Novemba 5, 2021 ikiwa ni miezi sita baada ya kifo cha Rais Dk. John Magufuli, alihoji zilipo Sh trilioni 360 ambazo Serikali ya Awamu ya Tano iliwadai Acacia na kupeleka shauri kwenye Baraza la Kodi.
Mpina alisema hayo bungeni Dodoma wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2022/2023 pamoja na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/2023.
Mpina alizungumzia serikali inavyoshindwa kukusanya fedha nyingi kutokana na kutokuwapo usimamizi madhubuti, akitoa mfano wa rufaa za kikodi zisivyofanyiwa kazi na kuigharimu serikali Sh trilioni 360 ambazo zingetumika kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi.
“Mhe. Mwenyekiti tulisema hapa wabunge tunazo trilioni 360 zimeshikiliwa na Mahakama, uamuzi haujatoka, nilitarajia kwenye mpango hapa isemwe kwamba hizo trilioni 360 ziko wapi, leo hapa Bunge zima linapiga makofi kwa trilioni 1.3 tulizopewa na IMF, fedha ndogo trilioni 1.3 tunapiga makofi mpaka mikono inauma na kwa kweli tunashukuru kwa hilo,” amesema.
Mpina alisema asilimia 10 ya Sh trilioni 360 ni Sh trilioni 36, lakini bado hilo halijawauma, Bunge halijaumia, serikali haijaumia lakini fedha zimeshikiliwa tu, kinachosubiriwa ni uamuzi tu wa mahakama.
“Kama tatizo ni hizo bodi zetu za rufaa za kodi zina shida ya wataalamu si tuajiri hata wataalamu wa kutoka nje kama tatizo ni wataalamu? Nini kinachosababisha, Mpango haujazungumzia suala hilo?” alihoji Mpina.
Septemba 22, 2022 Mpina amerudia hoja hiyo hiyo, zamu hii akisema kuna kesi 1,094 ambazo zimeshindwa kuamriwa na Baraza la Kodi lililopo chini ya TRA, hali iliyoifanya serikali kupoteza hata hizo Sh trilioni 360.
Kutokana na hilo, JAMHURI wiki iliyopita kupitia safu ya SITANII, lilichapisha uchambuzi kuhoji nia ya Mpina, hali iliyomwibua Kabudi na kutoa ufafanuzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ametoa ufafanuzi juu ya sakata hili la Sh trilioni 360 bungeni jijini Dodoma.
Dk. Mwigulu amesema, kuna jumla ya mashauri 400 katika Mabaraza ya Rufani za Kodi (TRAT) yenye thamani ya Sh trilioni 4.2 na Dola milioni 3.04 za Marekani zinazoendelea katika mabaraza hayo.
Pia amesema serikali ilikubali kupokea Sh bilioni 700 kutoka Barrick baada ya makubaliano baina ya timu ya serikali iliyoundwa na Magufuli kufikia makubaliano ya pande zote na Barrick kuhusiana na madai ya Sh trilioni 360.
Amesema baada ya makubaliano hayo iliundwa Kampuni ya Twiga inayomilikiwa na serikali kwa hisa za asilimia 16 na Barrick inamiliki asilimia 84 ya kampuni hiyo.
Ufafanuzi huo wa Mwigulu unatokana na maswali ya Mpina aliyetaka kufahamu kwa nini serikali imekubali kulipwa Sh bilioni 700 kutoka Barrick badala ya Sh trilioni 360 za
Acacia iliyokuwa inaendesha migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara ilisema tangu mwanzo kuwa kiasi hicho si sahihi kwa sababu kinazidi hata thamani ya kampuni yote.
Hata hivyo baada ya tangazo hilo la serikali, hisa za Acacia zilishuka kwenye Soko la Hisa London kwa asilimia 21, hali iliyowatia hasara kubwa.
Tangu Machi, 2017 ulipoanza mgogoro wa kuzuia makinikia, hadi Oktoba 2019 walipofikia mwafaka, hisa za Acacia zilishuka kwa asilimia 66, hali iliyowalazimu kuiuza kampuni hiyo kwa Barrick ili kuinusuru isifilisike.
Ukiacha hayo, tayari Barrick katika sehemu ya makubaliano imekubali kulipa mrabaha kwa kiwango cha asilimia sita badala ya nne za awali na kiwango hiki kinahusisha dhahabu, shaba na fedha. Pia imewekwa asilimia moja ya thamani ya mali inayosafirishwa nje ya nchi kama gharama ya ukaguzi bandarini.
Mwandishi alipomuuliza Kabudi kuhusu matamshi yake mbele ya Magufuli kuwa amemtoa jalalani na iwapo haoni kama alidhalilisha uprofesa wake akasema: “Ile profesa wa jalala, hata leo nimetoka kuongea na watu wengine ni sala ya unyenyekevu wa hali ya juu, ambayo ipo kwenye Zaburi ya 113, aya ya 7 hadi ya 8, pia ipo kwenye Kitabu cha Kwanza cha Samweli, Sura ya 2, aya ya 8.
“Na mimi baba yangu alikuwa ni Mwalimu, Bwana Shamba, Mtheolojia na Mtaalamu wa Tafakari. Alinifundisha hiyo ndiyo sala ya juu ya unyenyekevu, inaitwa sala ya Hana, kwa hiyo sikutumia jalala kwa maana hiyo, kwa sababu ingekuwa jalala kwa maana hiyo, eheee, eheee, waliotafsiri wengine siyo.
“Hata leo nilikuwa nasema natumia neno ‘Mtumishi asiyestahili au asiyefaa’ kutoka kwenye Biblia nikasema tena, msije mkaligeuza kama Profesa wa Jalala. Linatoka kwenye Zaburi ya 113:7&8, Kiswahili cha zamani ni ‘maani’, lakini ukisoma Kiswahili cha sasa ni ‘jalala’.
“Na ndiyo maana hata Tundu Lissu aliposema huyu Kabudi baba yake ni mtu wa kwetu Singida, which is true (ambayo ni kweli), alikuwa mwalimu, mama yake ni mwalimu lakini ametoka jalalani, ilikuwa ni Hana, ni ishara ya juu ya unyenyekevu.
“Kwamba unapopewa kitu, basi eheee, usiinue mabega, jinyenyekeze, na ndiyo maana nilimtafuta mpaka Askofu Bagonza nikamwambia sasa wewe Baba Askofu, umeyasoma maandiko matakatifu, basi mimi ni mtoto wa Mchungaji, ndiyo maana sisahau Zaburi.
“Hili jalala hili, nilitumia lugha ya Biblia katika mazingira ambayo hayakuwa sahihi… mazingira hayakuwa sahihi, sikuwalaumu ninyi, la hasha! Mimi mwenyewe nilitumia hiyo Zaburi katika mazingira yaliyokuwa siyo sahihi.
“Ndiyo maana leo nikasema ahaa, jamani mmeniita niwe mwenyekiti ‘mimi ni mtumishi asiyestahili’ lakini nataka nilifafanue hili, ni neno la unyenyekevu la Yesu mwenywe, msije mkasema ‘yule profesa asiyestahili.”