Rais Jakaya Kikwete ameibua hisia za baadhi ya akina mama wanaopinga hoja yake inayosema kwamba mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ni “Chaguo la Mungu”.
Akinamama hao waliokuwa wakishiriki kongamano la maombi na amani nchini wameeleza kuwa uteuzi wa Dk. Magufuli ndani ya CCM uligubikwa na migongano ya rushwa na makundi kutoka kwa wajumbe wa vikao vya juu vya chama hicho na sio chaguo la Mungu.
Washiriki wa kongamano hilo kutoka ndani na nje ya nchi, wametoa kauli hiyo wiki iliyopita katika mji mdogo wa Makambako, mkoani Njombe ambako kongamano lilifanyikia kwa kuwataka wananchi wasikubali kupokea unabii huo.
Washiriki wa kongamano hilo lililojumuisha wanawake 2,300 kutoka katika mikoa mbalimbali, wamesema wameshangazwa na kauli hiyo ya Rais Kikwete ambaye tangu awali, kabla ya uamuzi wa vikao vya juu vya chama hicho tayari alikuwa na mgombea wake wa urais mfukoni mbali na Dk. Magufuli.
Wanasema kuondoka CCM kwa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa anayewania nafasi ya urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kumetokana na Rais Kikwete kutumia rungu la uenyekiti kuminya haki ndani ya chama, lakini sasa anageuka na kudai Magufuli ni chaguo la Mungu.
Dk. Margaret Shayo, mtaalamu wa masuala ya afya mkoani Njombe amesema Rais Kikwete anajitafutia laana ya Mungu kwa kutoa kauli hiyo.
“Yeye alinadiwa hivyo kwa upofu wa baadhi ya viongozi wa dini kwamba alikuwa chaguo la Mungu jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote kutokana na utendaji wa serikali yake ulivyokuwa,” anasema.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita alipokutana na Wazee na wanachama wa CCM, kwa ajili ya kumtambulisha mgombea wa urais wa chama hicho, Dk. Magufuli kwa niaba ya wazee wa Tanzania nzima.
Huku akishangiliwa na wana-CCM waliokuwa ndani ya ukumbi huo Rais Kikwete alisema kuna watu wana uwezo wa kununua watu, lakini hawawezi kununua watu wote na kwamba Dk. Magufuli amefikia hatua hiyo kutokana na mpango wa Mungu.
Anasema Dk. Magufuli hakufanya kampeni za mbwembwe wala kujitangaza kwa waandishi wa habari kama walivyofanya baadhi ya waliojitokeza kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya urais, alifanya kampeni zake kimya kimya kwa kuwa hakuwa na fedha.
“Mungu ametaka awe kwa wale wanaomwamini Mungu, Magufuli ndiye chaguo sahihi,” alisema Rais Kikwete alipokuwa akiwahutubia wazee na wana-CCM.
Baada ya kauli hiyo washiriki wa kongamano la Dua na Maombi ya Amani kwa Taifa wamemtaka Rais kutubu kwani kwa kauli hiyo amewakosea Watanzania.
Akielezea madhara ya rushwa nchini, Mchungaji Eliniwako Mwaipopo wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Magharibi, Mpanda amesema, “Taifa sasa linanuka kwa rushwa na ufisadi katika kila sekta.”
Mchungaji Mwaipopo amemtaka Rais Kikwete kujitathimini upya kabla ya kugeuka kuwa nabii mwenye uwezo wa kupambanua kiongozi yupi ni chaguo la Mungu au vinginevyo.
“Dhambi ya rushwa imeshika kasi nchini tangu hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipong’atuka nafasi ya uenyekiti wa CCM, mwaka 1987, huku waliofuata wote wakipoteza mwelekeo na kukigeuza chama hicho na Serikali kuwa pango la wanyang’anyi,” anasema.
Anasema kwa Ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania imekuwa kinara wa rushwa na vitendo vya ufisadi na kusababisha haki za wananchi kukosekana katika huduma muhimu za afya, mahakama, elimu na maji.
Pamoja na hayo ameutaja pia ubovu wa barabara ambazo zinajengwa chini ya kiwango sehemu mbalimbali nchini kuwa ni mazao ya rushwa na ni ufisadi unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya viongozi wa serikali waliolenga kujinufaisha wao binafsi badala ya kuangalia maslahi ya umma.
Mtawa Daniel Katunzi (88), akichangia mada katika kongamano hilo, amemtaka Rais Kikwete aelewe kuwa chanzo cha kusambaa kwa rushwa nchini ni CCM, ambao walithubutu kuibariki kwa kuibatiza jina la “takrima,” na hiyo ndio sababu ya wananchi kukichukia chama hicho na kutaka mabadiliko.
Anasema bado Rais Kikwete amepigwa “upofu” kwa kutaka kumnadi mgombea urais kupitia CCM, Dk. Magufuli kwa kutumia kauli ya “chaguo la Mungu” kama ilivyoelezwa kwake alipokuwa akiwania nafasi hiyo, mwaka 2005 na kuona kuwa hakuna mtumishi wa Mungu aliyejitokeza kuipinga hivyo kuwaaminisha Watanzania unabii usio wa kweli.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste mkoani Mbeya, William Mwamalanga, amesema kwamba kitendo cha kuwaaminishwa Watanzania kuwa Rais Kikwete alikuwa chaguo la Mungu kilikuwa ni ulaghai wa kisiasa uliopenyezwa kanisani na wajanja wachache kwa kutafuta umaarufu na tamaa ya fedha za aibu.
Mwamalanga anasema inawezekana Dk. Magufuli hana tatizo isipokuwa chama anachotoka ndio kimekuwa tatizo kubwa kwani kimepoteza mwelekeo na kuwa chukizo kubwa kwa Watanzania.
“Sisi watumishi wa Mungu tunaifuta kauli ya Kikwete kwa damu takatifu ya Yesu Kristo, kwani ni kauli ya machukizo mbele za Mungu. Tulitengemea kauli ya toba kutoka kwake kutokana na kukithiri kwa rushwa ndani ya chama chake.
“Rushwa ndani ya CCM, imesababisha watu wengi kubaki vilema baada ya kupigwa au kupigana kama ilivyotokea mkoani Dodoma katika Jimbo la Kongwa ambako aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kumshambulia mgombea mwenzake kwa ngumi na fimbo hadi kulazwa hospitalini,” anasema.
Baadhi ya wanawake walioshiriki kongamano hilo la siku tatu lililomalizika Agosti 21, mwaka huu wamewaonya wanawake nchini kutokukubali kulishwa maneno ya uovu na kuwataka wanasiasa kuacha mara moja kulitumia jina la Mungu kuhalalisha uovu.
Kwa upande wake profesa Agnes Mac Donald kutoka Marekani ambaye aliwahi kutembelea Tanzania kipindi cha mwaka 1976 na 1980, amesema rushwa iliyopo Tanzania ya leo imetokana na kuongezeka kwa magugu ya viongozi ndani ya CCM ambao hawataki mabadiliko, hivyo amewahimiza wanawake nchini kushikamana kukiondoa chama hicho madarakani.
Profesa Agnes, anasema kukiondoa chama hicho madarakani ndio jibu na tiba sahihi ya rushwa kwa Watanzania.
“Rushwa inatia aibu ndani ya Tanzania hivyo njia muhimu ya kumaliza tatizo hili ni kuiondoa CCM kwa kuinyima kura katika uchaguzi mkuu mwaka huu badala ya kusubiri kife chenyewe,” anasema na kuongeza:
“Tangu niwasili hapa Tanzania wiki zaidi ya wiki moja iliyopita nimezungumza na baadhi ya wagombea udiwani, ubunge na wanachama wa kawaida wa chama hicho na wote kilio chao ni rushwa tu.”
Katika jambo jingine lililomshangaza ni kilio cha rushwa kutoka kwa wagombea wanaoeleza kwamba ili ushinde nafasi yoyote kupitia CCM, lazima uwe na kiasi kikubwa cha fedha ambazo zinatumika kununua kura.
John Emmanuel mkazi wa Mkoa wa Geita, akiilezea rushwa ilivyoshika kasi katika kipindi hiki cha uchaguzi, anasema baadhi ya wagombea wa CCM katika kata mbalimbali wanatoa rushwa kwa wananchi wakitaka kupigiwa kura katika uchaguzi mkuu.
Anasema kila kaya mgombea anagawa kilo moja ya chumvi ya mawe ambayo kiafya haipaswi kutumiwa na wanadamu kwa kuwa haina madini joto.
Anaongeza kuwa umaskini na ujinga sasa vimekuwa mtaji mkubwa kwa wanasiasa wenye uchu wa madaraka ambao wameendelea kuwalaghai wananchi kwa kuwahonga kilo moja ya chumvi.
Washiriki wa kongamano hilo la siku tatu walitoka katika mikoa Kigoma, Mara, Mwanza, Geita, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Lindi, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Kagera, Dar es Salaam, Pwani, Ruvuma, Iringa, Singinda, Makete, Njombe, Tabora, Rukwa, Manyara na Simiyu.