nmb-4Mimi nimefarijika sana na ninamshukuru Mungu kuona Makala zangu zinavyosomwa na watu na zinavyotoa changamoto miongoni mwa wasomaji. 

Nimekuwa nikiandika makala katika magazeti mbalimbali na kwa hivi karibuni katika gazeti la JAMHURI. Kutokana na makala hizo nimekuwa nikipokea meseji nyingi na hasa nimekuwa na mazungumzo katika simu za viganja. 

Meseji kadha nimepata kuhusiana na zile makala za udini, elimu, ushoga, uwajibikaji, utawala bora na hii ya juzi juzi umamluki! Asanteni sana kunikosoa, kunishukuru na kunielimisha kwenu katika yale niliyopata kutoka meseji na simu zenu. Mathalani suala la umamluki katika siasa, nawaleteeni baadhi tu ya meseji nilizopokea muone hisia tofauti za wasomaji. 

Kutoka simu Na. +255 785 503 043 ya Agosti 11, anasema, “Ndicho kilichowadanganya CCM kwamba Lowassa ni fisadi hivyo CHADEMA hawatampokea. Kwani Jakaya hakutajwa kwenye ile orodha ya mafisadi 11 mbona ni Rais? Lazima tuing’oe CCM. Baba wa Taifa alisema wananchi wakichoka wanaweza kuchagua hata kichaa.”

Kutoka simu No. +255 759 705 052 ya Agosti 11 2015 alisema “Mzee Francis Mbenna nimesoma kwa makini gazeti la Jamhuri uk. 10 umeeleza vizuri sana mzee wangu hongera mwenye macho aone mwenye masikio asikie, mwenye ufahamu mzuri aelewe. Mungu akubariki na kukulinda uendelee kutuelimisha”.

Kutoka simu Na. +255 719 683 236 ya Agosti 11, 2015 amesema, “Mzee Mbenna najua wewe ni kada mzuri tena mwaminifu wa CCM, lakini kumbuka siasa ni mapambano akina Dk. Lwamwai, Wasira, Limbu Kabouru, Makongoro Nyerere walitukana sana CCM walipokuwa upinzani, leo wako ndani ya CCM wanawatukana na kuwabeza wapinzani. Ndiyo siasa mzee. 

Kutoka simu Na. +255 755 277 181 anasema, “Makala yako inatetea sana CCM unataka kuvuruga UKAWA. Wewe tuache na CHADEMA yetu baki na CCM yako”

Basi ningeweza kuwaleteeni meseji zaidi, lakini hakuna ulazima huo. Hizi nimezichukua tu kidharura (random sampling) bila mpangilio kuonesha hisia mbalimbali za wasomaji kimtazamo juu ya mojawapo za makala ninazotoa kama uraia kwa wenzangu. 

Napenda ieleweke wazi hapa kuwa mimi siandiki makala kama wale waandishi wataalam waliobobea katika uandishi (professional writters) kama akina Jenerali Ulimwengu, Profesa Rioba, Deodatus Balile, Johnson Mbwambo na Manyerere Jackton na kadhalika. Mimi ni mwandishi mwagenzi (amateur writer) tu.

Na nimejitumbukiza kwenye uandishi baada ya kuvutiwa na neno la Mwalimu wangu Julius K. Nyerere katika kile kitabu chake alichokitafsiri cha William Shakespeare mchezo wa Julius Kaizari – Mwalimu aliandika hivi “Nia yangu ilikuwa kupata jambo la kufanya wakati kazi zangu za kawaida zilipokuwa zimenichosha sana na nataka kiburudisho (Nyerere: Tafsiri ya Julius Caesar uk. 3 toleo la 1963). 

Mimi kabla ya kustaafu kutoka utumishi wangu Serikalini (JWTZ) nilikuwa ni mwalimu wa darasani kabla ya kujiunga na Jeshi (professional classroom teacher) nilijisikia uchovu mkubwa (very much bored) kukaa bila kitu cha kufanya. Baada ya kustaafu hapo ndipo nitakafuta jambo (hobby) la kufanya ndipo nikajitumbukiza kwenye kuandika makala kutoa uraia kwa wananchi wenzangu.  Hivyo makala zagu zisomwe kwa mrengo huo wa uraia wala siyo ushabiki wa siasa. 

Kutokana na meseji nyingi kuelekea kwenye lile la Mheshimiwa Edward Lowassa kuhama kutoka CCM kwenda CHADEMA, mie naona tufuate ile falsafa ya Mwingereza mmoja inayosena “Small minds talk about people average minds talk about events and big minds talk about issues.” Hii maana yake watu wenye akili finyu wanaongelea watu kama vile fulani kuvaa nini, anakula nini, anatembeaje yaani kumchambua mwenzi wake.

Lakini watu wa kawaida na ndio tulio wengi, wanaongelea matukio zaidi mathalani mpira wa Yanga na Simba au Azam, Man U na Chelsea, Vita vya Kagera, Sunami, kukatika kwa umeme mara kwa mara na kadhalika. Kumbe watu makini wasomi kama wahadhiri wa Vyuo Vikuu na au wasomi makini mbalimbali wao watazungumzia mambo yaani “issues”. 

Jambo kama la Uchaguzi Mkuu, jambo la uchumi wa nchi, maliasili ya nchi na kadhalika. Sasa mimi ninapoandika makala, natumia daima nomino za maarifa (abstract nouns) ndiyo maana naweka u mwanzoni mwa makala zangu kulenga hayo wala si matukio au watu wenyewe (personalities). Hivyo ni hisia, ni dhana basi kamwe haziwezi kulenga chama wala mtu bali zinatoa taswira ya uwepo wake hali fulani. 

Mtindo huu wa hamahama ya wanasiasa kutoka chama A na kwenda chama B ni tukio tu kama matukio mengine. Katika magazeti kadhaa waandishi wamelenga mtu mmoja zaidi ndiye Mhesh. Edward Lowassa. Lakini hiyo kwa mtazamo wangu siyo “Issues” hata kidogo ni tukio la kawaida kutokea.

Turudi kwenye historia. Uhamaji sasa imekuwa kama upepo unaovuma kutoka upande huu na kuelekea upande ule. Neno hili upepo unaovuma lilianza kusikika tangu mwaka 1960. Waziri Mkuu mmoja wa uingereza alieitwa Harold Maurice MacMillan (1957 – 1963) alipotembelea Afrika ya Kusini 1960 alipata kusema haya “the wind of change was blowing through the African Continent, and so the British Government was opposed to the policy of apartheid” katika Bunge la Makaburu (Taz. Encyclopedia Britannica, Vol. 14 uk. 542). Tamko  hili la kihistoria lilionesha changamoto za vyama vya siasa barani Afrika katika harakati za kudai Uhuru katika nchi zao. Tamko lenyewe kule kutolewa mbele ya makaburu huko Afrika ya Kusini. Kulikokuwa na hali mbaya sana ya ubaguzi wa rangi na kuwakandamiza wananchi weusi waliokuwa wengi huko, lilikuwa na uzito wa pekee.  Aidha lilileta msisimko miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa, waliokuwa wanapigania Uhuru wa nchi zao. 

Hapa nchini Tanzania, mwimbaji maarufu, hayati Kepteni John Komba akiongoza kwaya ya JWTZ Lugalo miaka ile ya 1970 alichukua tamko lile la MacMillan akalitungia wimbo maarufu uliokiimbwa na kwaya ya JWTZ ukisema, “The Wind of change is blowing across the African continent” wapigania Uhuru nchini Tanzania hapa Dar es Salaam (kutoka Msumbiji, Angola, Namibia, Southern Rhodesia (leo ni Zimbabwe na Afrika ya Kusini) walisisimka sana kwa wimbo ule. Walikazana kudai mabadiliko ya Serikali. Basi kuvuma kwa upepo ule wa siasa kulileta mabadiliko Msumbiji, Angola, Zimbabwe na Afrika ya Kusini yenyewe. 

Sasa huku kuhama kwa wanaCCM kwanini kuonekane waziwazi mwaka huu? Mimi narudia kwenye historia tu. Wimbi la hama hama ni jambo la kawaida wala lisiwaondoe wananchi kutoka kwenye jambo kubwa la uchaguzi wa mwaka huu tukakazania kuongelea watu na tukasahau suala hilo la  maana sana kwetu linalotukabili “Uchaguzi huru” na wa kidemokrasia. 

Mwaka 1958, mwezi wa Januari kule Tabora, TANU walikuwa na mkutano mkubwa wa kutoa uamuzi mgumu. Kukubali kuingia uchaguzi wa kura za mseto au kususia uchaguzi na kumpa mkoloni nafasi aendelee kutawala – TANU pale ilimeguka!

Ndugu yangu mchambuzi wa Siasa za TANU Mohamed Saidi, aliandika haya “when the agenda for tripartite voting came up for discussion, the Tanga strategy was unfolded – Nyerere who chaired the conference left the chair to Mwalimu Kikere ….. as Nyerere had earlier envised, all hellbroke loose; delegates shouted and banged tables in anger, others moved chairs noisly in irritation” (soma Abdulwahid Sykes by Mohamed Said uk 241)

Hayo yaliyotokea Tabora Januari 1958 ni kama yaliyotokea pale Dodoma mwaka huu wakati chama kilipotangaza mgombea wake wa urais wanaCCM walionekana kuchanganyikiwa na kuanza kudai kanuni za uchaguzi ndani ya chama hazikufuatwa. Ikawa patashika. Tuliona baadhi ya wajumbe wamesimama wakiimba ule wimbo wa JKT kuwa tuna Imani na Lowassa, oya oya oya….

Matokeo yake yalikuwaje? Mwaka ule 1958 Katibu Mkuu wa TANU, Zuberi Mtemvu alikiacha Chama cha TANU na baadhi waliokubaliana naye wakahama TANU na kwenda kuanzisha Chama kipya cha upinzani. Mwaka huu, baada ya Chama kutoa ule uamuzi mgumu, mjumbe wa Kamati Kuu, Lowassa alitafakari kukihama chama, na hatimaye Julai 28, 2015 alitangaza rasmi amekihama chama kilichomlea! 

Pamoja naye wamehama mawaziri, wenyeviti wa mikoa na wilaya na kukimbilia upinzani. Hivyo jamani kuvuma kwa ule upepo wa MacMillan, 1960 ni jambo la kawaida ulimwenguni, watu kuhama kutoka chama kimoja na kuingia chama kingine, hawavunji Katiba yoyote ya nchi. 

Mwaka 1967, TANU walipitisha Azaimio la Arusha Januari 29 kule Arusha na lilitangazwa rasmi katika viwanja vya Arnatoglu Februari 05, 1967. Wapo baadhi ya viongozi wa TANU hawakulipenda Azimio lile la Arusha. Ulikuwa uamuzi mgumu wa TANU. Mmoja wa viongozi wale alikuwa Katibu Mkuu wa TANU, Oscar Kambona huyu alitoka ndani ya TANU na akaimbikia nchi akaenda Uingereza kuishi.  Nasema, kuhama viongozi kutoka CCM siyo tukio la ajabu wala la kipekee Chama hakikutetereka kikawa bado ngangari tu. 

Mwaka 1995 kada maarufu wa CCM, Mzee wa Kiraracha, Augustino Lyatonga Mrema alikihama CCM kuingia NCCR Mageuzi akakipa nguvu na kukiinua sana (enhanced and revamped) chama hicho. Ulifika wakati wafuasi wake walikuwa tayari kumbeba katika machela (ndugu zangu wandamba kule Ifakara) na wafuasi wake walikuwa tayari kulisukuma gari lake kama nguvukazi watu badala ya nishati ya petroli. 

Basi Mwalimu Julius Nyerere kwa mizaha yake na utani wa kejeli alisema hivi, “kama watu wa kubeba wapo, na huyo anayependa kubebwa yupo mwacheni abebwe, ila msimpe kura”! Wale tunaokumbuka, Uchaguzi ule wa 1995, mteule wa NCCR Mageuzi, Mrema aliambulia kura 1,808,616 hivyo NCCR – Mageuzi ilibwagwa na CCM ambayo ilivuna kura 4,026,422 na mteule wake akatinga Ikulu. Ndipo mzee wa Kiraracha akagutuka na kuona kumbe wale wengi waliokimfuata walikuwa bure tu hawakuwa wapiga kura”. It was a mob – appraisal with no voting power! 

Ulipofika Uchaguzi ule wa mwaka 2000 tuliona mashabiki wakitamba na CUF. Ulifika wakati Profesa Ibrahim Lipumba sehemu za Mbagala Zakiem akipita tu washabiki walimwita Rais, Rais, Rais. Katika upigaji kura Oktoba 2000 mwaka ule matokeo yalionesha CUF kupata kura 1,329,077 wakati CCM walikomba kura 5,863,201. Ile tamba tamba ya CUF eti wao ni ngangari ikayeyuka hapo hapo. Baadhi ya washabiki wa CUF walihamia CCM. 

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa baada ya kuenguliwa ubunge wa Karatu kwa kadi ya CCM alikihama Chama na kuingia CHADEMA hata akateuliwa kuwa Katibu wake mkuu. Mwaka 2010 akawa na mvuto mkubwa sana. Akagombea Urais kwa tiketi ya CHADEMA. Inasemekana umati uliohudhuria mkutano wake kule Mbeya, ulivunja rekodi kwa kufurika, wala haijapata kutokea mpaka sasa.

Basi tena tunaona “mob-appraisal” inavyoweza kupumbaza watu. Matokeo ya Uchaguzi wa 2010 miongoni mwa wapiga kura wapatao 8,626,283 ni wapiga kura wapatao 2,271,491 tu walipigia CHADEMA wakati wapiga kura zaidi ya 5,276,827 waliipigia CCM. 

Najaribu kuonesha kuwa la msingi ni idadi ya wapiga kura ndiyo inayomleta mtu Ikulu na siyo mafuriko ya wastajabiaji katika mikutano. Hao wengi wao hawakujiandikisha kupiga kura na wala hawaendi kupiga kura bali wanakuwa mashabiki wa kiongozi tu. Hapa inafaa wananchi tutambue ya kwamba kila mmoja wetu anao Uhuru wa kumchagua ampendaye. Katiba inasema hivyo. Lakini si kila mtu huru anaweza kupiga kura. Haki hiyo ya kupiga kura ni ya wote waliojiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura na waende kituoni kupiga hiyo kura yake. “Wishful thinking”, haimpi umpendaye nafasi ya ubunge au urais bali kura yako tu ndiyo ina uwezo huo. 

Nimechambua matukio kabla ya chaguzi mbalimbali ili kuonesha licha ya kasoro ndani ya CCM bado CCM ina mvuto nchini. Baba wa Taifa mwaka ule 1995 alikosoa pia CCM yake katika kitabu chake kile “UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA” uk. 66. Tunasoma maneno haya, “Nilisema awali kwamba Kansa ya ungozi ndani ya CCM isingekuwa jambo la kutisha kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuongoza nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi.

Nalitamani kuwa tunawerza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuongoza nchi yetu badala ya CCM, au ambacho kingalilazimisha CCM kusafisha uongozi wake” bila upinzani mzuri wa nje na bila demokrasia halisi ndani ya CCM, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu”. Matatizo ndani ya CCM ni kama ugonjwa wa kansa yamekuwepo toka zamani wala hayakuanza mwaka huu.

Kuanzia hapo, maneno haya ya mwasisi wa TANU na CCM alipokuwa angali hai tujifunze kitu. Kuwa upo uongozi mbovu ndani ya CCM.  Matokeo yake kanuni za uchaguzi au uteuzi wa wanachama wanaogombea umekuwa na mazonge mazonge karibu nchi nzima. Malalamiko yamesikika toka Karagwe, Bukoba, Mwanza, Sengerema, Ukonga, Upanga, Songea, Mbinga, Iringa, Katavi, Kibamba, Mbeya, Namtumbo, Rufiji na kwingineko. Swali, hii inaonesha nini? Ni ishara ya Ubovu uliokithiri ndani ya CCM. 

Tumelifuta Azimio la Arusha, tumeacha miiko ya uongozi sasa imetokea vurugu mechi mtupu tangu katika hatua za mwanzo za uchaguzi kwenye KURA ZA MAONI. Mnaposikia hata Waziri anamtwanga konde msimamizi wa Uchaguzi hapo mjue demokrasia katika Chama hicho haipo (Mwananchi toleo 5499 la Agosti 15 2015 uk. 4 kichwa WAZIRI ATEMBEZA MKONG’OTO”) Chama kinaelekea kutawawaliwa na ubabe, dhuluma, uonevu na dharau kwa wanyonge. Isitoshe uadilifu wa viongozi unaweza kuwa mashakani (intergrity of leadership is questionable!) pia.

Mwalimu Nyerere kwa kuchoshwa na uongozi mbovu ndani ya Chama alifikia kujiuliza, “sasa mimi nifanyeje? Wala CCM wasije wakaninung’unikia, maana ndicho Chama kinachotawala na wala wa Vyama vingine wasije wakasema” “Mbona mwalimu unasema kama unapendelea CCM!” Aka! Kama wanataka niwabomoe ninaweza kuwabomoa, lakini sitaki. (Hotuba ya Mwl. Nyerere, kwenye sherehe za Mei Mosi 1995 uk. 16).

Jamani, CCM imekuwa na Serikali inayotawala nchi hii tangu tupate Uhuru hapo  Desemba 9 1961. Ni miaka 54. Mimi mzee nasema tuhesabu tangu siku ilipopata Serikali ya ndani yaani Septemba 3 1959. Basi mimi niwakumbushe tu wasomaji wangu. Matamko ya aliyekuwa Gavana wa Tanganyika wakati akiwaapisha Mawaziri wa TANU wananchi 9 na wazungu 3 alitamka hivi. “Neither party when in power would accept the view that its Parliamentary party could instruct or control the Cabinet. This is constitutionally correct for it is important to the House of common as a whole and through Parliament to the nation”. (HE the Governor and Commander in Chief Tanganyika in 1959 speech pg 6 – 7).

Maneno hayo yanatosha kuonyesha kikatiba Chama Tawala, baada ya Uchaguzi kina wajibu gani katika Serikali na Bunge. 

Pia nataka kuonesha TANU imeanza kutawala tangu Septemba 1959 takribani leo tunaweza kusema ni miaka 57. Huo kweli ni muda mrefu. Wanaelekea kulewa na madaraka na wamesahau yale majukumu yao ya chama cha kutetea wanyonge, wakulima na wafanyakazi wa nchi hii. Kwa uchovu huo unaonekana sasa wapinzani wanasema basi afadhali wang’olewe kutoka madarakani. Utawala mpya uingie madarakani sasa. Hiki ni kilio cha vijana wengi siku hizi – mabadiliko!

Malalamiko yote haya wakati huu wa kura za maoni ni kiashiria tosha cha uchovu na kukosa umakini katika utawala. Inawezekanaje kweli chama kikongwe namna hii, kina leja zenye orodha ya wanachama wake hai wote. Sasa katika kura za maoni wananchi wanalalamika orodha za wanachama hai katika matawi hazikufuatwa. Inawezekanaje waje watu na kadi feki waruhusiwe upigaji kura za maoni wanatawi hawawajui? Kura za maruhuni zinatoka wapi? Basi CCM inapaswa ijitafiti na ijirekebishe kuwapa watu imani ile waliyokuwa nayo tangu enzi za TANU. 

Yametokea malalamiko ya rushwa na ule utamaduni wa kubebana. Ndiyo maana mimi nasema elimu ya uraia ni muhimu kwa wananchi wote hasa wapiga kura wajue haki na wajibu zao wakati wa uchaguzi. Tunahitaji mawazo mapya kwa vijana wetu wanaodaii mabadiliko katika utawala. Kuanzia mwaka ule 1995 kulikwisha kuonekana dalili za ukiukwaji wa maadili na miiko ya uongozi. Hali namna ile iliwafanya wanachama wa ile Klabu ya Waandishi wa Habari nchini wamwalike Mwalimu aje awazungumzie hali iliyojitokeza katika nchi. Walitaka maoni ya Mwalimu. Basi Mwalimu alikubali mwaliko ule akaenda hapo Kilimanjaro Hoteli Machi 13 1995 na kuongea nao wanahabari wale.

Mwalimu alianza kwa kusema, “Nilifikiri ati labda nitakaporudi naweza nikazungumza na jamaa hawa kuhusiana na misukosuko iliyoanza kuhusu uchaguzi wa Rais wa mwaka huu (1995) mwezi Oktoba. Akaendelea, mimi nadhani, kama tunataka kusaidia nchi yetu, hatutazungumza majina sahihi sasa hivi. Tutazungumza masuala (issues) yanayokabili Taifa letu kwanza” (ona Nyufa: uk 5) Hapo peke yake mtu unaona, Mwalimu alijua kuna mizengwe katika uchaguzi mwaka ule. Kuna majina ya watu na kulikuwa na masuala ya uchaguzi wa kidemokrasia hapo (the issue was proper democratic elections in my opinion).

Katika mazungumzo yake Mwalimu alitaja Nyufa 5 zilizokuwa zinalitikisa Taifa letu. Moja ya Nyufa alizoziongelea Mwalimu iligusu Uchaguzi wa mwaka ule 1995, ulikuwa UFA aliouita ”RUSHWA”. Katika hili Mwalimu alisema hivi, “lakini sasa katika uchaguzi nasikia mtu anakuja na pesa. Uchaguzi mwaka huu (1995) utakuwa uchaguzi wa pesa. Zamani katika CCM na katika TANU tunapochagua mgombea wetu kama ana mali kilikuwa kigezo cha kukupotezea sifa ya kuwa mgombea. Mwaka huu (1995) mali itakuwa ndiyo kigezo namba wani. Wanazipata wapi? Wamezipata wapi?

Basi viongozi wetu wa sasa wayaone maneno mazito hayo toka kwa Mwalimu mwaka ule 1995 yalikemea sana mwenendo wa CCM kukumbatia fedha (na matajiri) katika Uchaguzi wa mwaka ule. Na leo hii 2015, kelele za rushwa zimesikika sana, kutoka kila upande wa nchi yetu. Inaashiria nini kwa chama kuona kero za rushwa zinasikika kila upande?

Chama cha CCM kule Dodoma katika vikao vyake Agosti 10 – 14, mwaka huu wamelazimika kuagiza uchaguzi urudiwe katika baadhi ya majimbo na wameagiza kura zihesabiwe tena katika baadhi ya vituo ili wajiridhishe kuwa haki imetendeka katika uteuzi wa wagombea wao. Luninga zimeonyesha tafrani za kupinga matokeo ya kura za maoni mathalani Upanga magharibi, Songea, kule Simiyu na kadhalika. 

Huu mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi umekomaza demokrasia katika nchi yetu. Vyama vya upinzani vina umri wa miaka takribani 23 hivi sasa. Tabia ya kuhama hama kutoka chama hadi kingine nilielezea katika makala iliyopita ni utamaduni tuliofikia unaopanua uwigo wetu wa demokrasia. Kitu waafrika wengi, viongozi na tusiokuwa viongozi, ni kutokuwa na maadili ya utu (no integrity) hakuna uwajibikaji, tunalenga kupata tu.  Dhana ya kukosa au kushindwa haipo kabisa katika msamiati wa kiafrika. Hilo ndilo linafanya viongozi wengine wa nchi kung’ang’ania madaraka mpaka wafie humo! Kwa nini sijui! Hatuoni au hakutubali ule ustaarabu wa kupokea kushindwa (concede defeat or failure) au kupumzika walivyofanya Nyerere na Mandela na hivyo kupisha wengine kwenye wadhifa ule. 

Gazeti la Mwananchi toleo Na. 5499 la Jumamosi Agosti 15, 2015 katika ukurasa wake wa 4 limeweka idadi ya viongozi waliohama kutoka chama kimoja na kuingia chama kingine baada ya kushindwa kura za maoni katika vyama vyao vya mwanzo au kutokubaliana na kanuni zilizotumika katika uteuzi wa mgombea urais. Wameorodhesha hivi: wabunge waliohama CCM na kwenda CHADEMA walifikia 6; wabunge wa CHADEMA waliohamia CCM na TADEA walikuwa 3; wabunge wa CUF waliohamia ACT walikuwa 2; wabunge wa CHADEMA kwenda ACT walikuwa 2. Aidha wenyeviti mikoa wa CCM waliohamia CHADEMA walifikia 4. Mbunge wa CHADEMA kwenda ACT alikuwa 1. Sijaona waliotoka CCM au CHADEMA au CUF kwenda TLP au UDP sijui hakuna mshiko huko au vipi.

Lakini bado nashangazwa na utoajii taarifa wa Mwanasheria wa CHADEMA Tundu Lissu. Hapa katika Mwananchi amenukuliwa kusema tu kuwa “ukiangalia wote waliohama utaona walikuwa “anonymous” hapo sijaelewa maana ya neno anonymous ninaliona lina utata (ambiguous) na wanasheria hawapendi kujifunga. Linamaanisha wasiojulikana, hawana majina, hawana nyadhifa au hawana uzito kisiasa sijui – lakini ndiyo ilivyoandikwa katika Mwananchii (ule uk. wa 4) kajisomee uelewa wako bwana. Hayo ni maelezo ya kuwadhalilisha maana kwa kiasi ni kama kusema watu wasiohitajika vile huko walikohamia.

Baada ya vikao vile vya Chama kule Dodoma kati ya  Julai 08 – 13, 2015 vilivyoteua mgombea wa CCM kwa urais hali ya hewa ilionekana kuchafuka katika Mkutano Mkuu wa Chama. Madai ya kukiukwa utaratibu mzima wa Chama katika kumteua mgombea wake yalisikika. Mzee Pius Msekwa alinukuliwa kusema, “kwani ukweli wenyewe ni kwamba kanuni za CCM zinazohusika zilifuatwa kwa ukamilifu. Kanuni zilizotumika zinaitwa kanuni za usalama na maadili, toleo la mwaka 2012, kwa mujibu wa kanuni namba 3 (3) (vii). Kanuni hii ndiyo inaipa uwezo Kamati ya Usalama na Maadili kufanya uchambuzi wa maadili ya wagombea wote, kabla, majina ya kupelekwa kwenye vikao vinavyofuata vya CC na NEC (Taz. Mwananchi Toleo No. 5475 la Jumatano  Julai 22, 2015 uk. 5).

Hapo sasa waliokipiga kelele kama utaratibu au kanuni zilikiukwa mbona hawazitaji ni kanuni namba ipi imekiukwa? Hao waliohama kutoka CCM baada ya uamuzi wa Chama kule Dodoma wa kumkata Lowassa na kumwibua Magufuli si wanajua kanuni hiyo aliyoitaja Mzee Msekwa? Kama hawakujua siyo kosa la Chama ni kosa lao. Kisheria inasemekana “ignorance of the law is not admissible in Court of law as a defence” . Ahadi mojawapo ya TANU ilisema nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote. Hapo ndipo ninajiuliza ni kweli viongozi wote wa CCM wanazijua zile ahadi za mwanaCCM? Chama kinabidii kiwaelimishe viongozi wake wote zile IMANI za CCM na zile AHADI za mwanachama.

Mimi nina utamaduni wa kumnukuu Mwalimu wangu Nyerere Baba wa Taifa toka hotuba zake au maandiko yake. Pia ninapenda kujiridhisha kwa upande wa Imani yangu kunukuu toka kitabu cha maandiko matakatifu, Biblia, kuthibitisha uhalisia (authencicity) wa kile ninachoandika. Basi katika hili la RUSHWA niwaombe viongozi wangu wa vyama vyote vya siasa na wale wa Serikali wasome Biblia inasema “usipotoe maamuzi, wala usipendelee uso wa mtu wala usitwae RUSHWA, kwa sababu Rushwa hupotosha macho ya wenye akili na kugeuza daawa ya wenye HAKI. Yaliyo haki kabisa ndiyo utakayotafuta ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana. Mungu wako (Kumbukumbu ya Torati sura 16 mistari ile ya 19 – 20).

Pale viongozi wa Chama kama wabunge au wenyeviti wa mikoa, wanapohamaki baada ya kura za maoni hata kufikia kutupa Makonde kwa wasimamizi wa uchaguzi, tujue tumefikia pabaya, kiutawala. Hili halina mabishano. Tujisahihishe na turudishe imani ya wananchi kwa uongozi mahiri wenye utulivu na usikivu. TANU ilikuwa hivyo. 

Baadhi ya wasomaji wa Makala katika magazeti wanajenga hisia ya kujifikiria wanasemwa wao au chama chao. Hili siyo dhana endelevu bali ni mtazamo rajua sana (pessimistic opinion). Inafaa kuwa wasomi endelevu (constructively and perceptively) ndiyo sababu waandishi wa sarufi sahihi wanatumia misemo ya nomino za maarifa (abstract nouns). Hayati Shaaban Robert katika kitabu chake kile cha KUSADIKIKA ametumia mawazo ya ughaibuni zaidi. 

Tukiwa sote na mawazo ya kulijenga Taifa letu kwa uzalendo kweli, uchaguzi ujao tutauendesha kwa Amani na utulivu. Sote ni wananchi huru kabisa kikatiba. Lakini wenye uwezo wa kukiweka Chama madarakani katika uchaguzi ni wale wapiga kura wapatao 24 milioni hivi ambao walijiandikisha na watakaokwenda vituoni kupiga hiyo KURA. Tusibweteke na mashabiki lukuki katika mikutano. Wanao Uhuru kudai hili au lile lakini uwezo wa kukutia ndani ya Bunge au kukupeleka Ikulu ni wa mpiga kura mmoja mmoja. Tuchunge hilo. Suala muhimu kwetu ni UCHAGUZI WA KIDEMOKRASIA, uendeshwe kwa haki, utulivu na Amani.

 

Mwandishi wa Makala hii, Francis Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.