Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora
Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora nchini Tanzania, leo Ijumaa Septemba 30, 2022 imewahukumu kunyongwa hadi kufa watuhumiwa watano ambao ni wakazi wa Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora.
Ni baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kumuua mume wa mwenye Ualbino wakati akimtetea mkewe asikatwe mkono kutokana na imani za kishirikina.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora, aliyekasimiwa mamlaka ya ziada, Jovin Katto, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Katika hukumu hiyo Hakimu Katto, amesema upande wa mashtaka umethibitisha pasipo shaka washitakiwa hao, ndio wametenda kosa hilo la kinyama ambalo adhabu yake ni moja ya kunyongwa hadi kufa.
Waliopewa adhabu hiyo ni Mussa Njile Masanilo, Mhoja John Shija, Regina Kashinje Kulwa, Elizabert Masanja Shija na Biria Masanja.
Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Merito Ukongoj, uliiambia mahakama hiyo washitakiwa walitenda kosa hilo Agosti 16, 2014 usiku katika kijiji cha Buhekela, wilayani Igunga.
Amesema siku hiyo saa nne usiku, washitakiwa walivamia nyumbani kwa Mapambano Mashiri ambaye kwa sasa ni marehemu na kumkata kata kwa mapanga hadi kusababisha kifo chake.
Katika shauri hilo, Hakimu Katto amemhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitano jela, Bahati Kulugu, ambaye alikutwa na mkono wa mama huyo mwenye ualbino.
Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kwamba Bahati Kalugu alikamatwa akiwa na mkono huo wa mwenye ualbino akitafuta mnunuzi.
Upande wa mashitaka ulikuwa umeandaa mashahidi 48 lakini kwa vile maelezo yao yalikuwa yanafanana waliofika mahakamani ni mashahidi 12 tu kati yao.
Hili ni moja ya matukio mabaya na ya kusikitisha yaliyotokea mwaka 2014 yakihusisha watu waliokuwa wakisaka viongo vya watu wenye ualbino kutokana na imani za kishirikina.
Hakimu Katto ambaye ni miongoni mwa mahakimu waliongezewa Mamlaka ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu, amesema washitakiwa baada ya kumshambulia kwa mapanga hadi kufa, Mapambano Mashiri, walimkata mkono wa Mkewe ambaye ana ualbino.