Na Omary Mngindo, TimesMajira Online,Ruvu
Taasisi ya Lions Club imemkabidhi vitanda na vifaa tiba Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete, vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 4.9.
Katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Zahanati ya Kijiji cha Ruvu Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze, ambapo vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa Ridhiwani na Mwenyekiti Mbunge Jimbo Shiraz Jessa.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Jessa amesema kuwa vifaa hivyo walivyokabidhi vimetolewa na Kampuni Refuelling Solutions T ltd.
“Sisi Lions baaada ya kupokea ombi la uhitaji huu tuliwasiliana na Kampuni ya Refuelling Solutions T ltd, ambayo imetufadhili,” alisema Jessa.
Kwa upande wake Muntazir Bharwani amesema kuwa kazi kubwa ya Lions ni kusaidia na kutatua changamoto zinazoikabili jamii, na kwamba walipopata ombi hilo kutoka kwa Diwani Mstaafu Mohsin kwa niaba ya Diwani Gama waliwasiliana na Refuelling waliowapatia vifaa hivyo.
Ridhiwani alisema kuwa taasisi hiyo imesikia kilio cha wanaChalinze na kuongeza zipo taasisi nyingi zimeombwa lakini zimeshindwa kufanya hivyo.
“Maneno mazuri yaliyozungumzwa na Muntazir ya kusema Vigwaza ni nyumbani kwake, kauli ambayo imeleta faraja kwetu sisi tuna usemi unaosema Kunogile ukaee,” alisema Ridhiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Hassani Mwinyikondo alisema kuwa Mbunge Ridhiwani ameendelea kuisaidia Chalinze, ambapo fedha kadhaa zimepelekwa kwa ajili ya kuujenga mji wa Chalinze.
Diwani Gama amesema kuwa Mbunge huyo amesaidia kupatikana kwa fedha zilizosaidia miradi kadhaa ikiwemo ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.
“Namshukuru sana Mbunge Ridhiwani kwani amekuwa msaada mkubwa katika kata yetu ya Vigwaza, fedha nyingi zimefika kwa ajili ya kiradi mingi,” amesema Gama.
Mkurugenzi Gama ameipongeza Lions kwa msaada huo, ambao unakwenda kuboresha sekta ya afya kijijini hapo na Kata kwa ujumla