Watanzania wengi tunaendesha biashara kienyeji. Hatuna mifumo ya kibiashara, hatuna malengo ya biashara na wala hatuna mwelekeo wa kibiashara. Wengi wetu tunategemea kudra za mwenyezi Mungu kutufikisha mwakani, hatuna uhakika na tunakoenda wala hatujui tutafika lini. Tuna macho ya kuitazama leo tu, hatuna malengo ya angalau hata muongo mmoja.
Watanzania wenzetu wenye asili ya Kihindi na Kiarabu wametuzidi sana katika hili. Wenzetu hawa wana tamaduni imara sana za kibiashara kiasi ambacho matajiri wengi tunaowasikia sasa wenye asili hii; mali hizo wamerithi eidha kutoka kwa baba ama babu zao. Muhindi ama Muarabu hawezi kuanzisha biashara halafu ikafa kirahisi!
Pengine tofauti na zamani, nyakati za sasa zinahitaji biashara kuendeshwa katika mifumo ya kisasa. Utunzaji wa mahesabu, utafutaji wa masoko, kuhimili ushindani sokoni, kubadilisha bidhaa kuendana na mahitaji ya soko; yote haya ni mambo yanayohitaji ukisasa. Biashara za kuuza samaki miaka nenda rudi bila kubadilika, ama kufanya biashara za magari bila kuboresha huduma; si rafiki tena kwa sasa.
Ingawa kuna mambo mengi sana hapa katika ukisasa kwa leo nitagusia maeneo matatu tu. Mosi, kuweka biashara katika mifumo rasmi; Pili kuwa na maono na tatu kutengeneza mfumo wa kurithisha biashara kutoka baba kwenda kwa watoto; kutoka kwa wajukuu kwenda kizazi cha pili.
Biashara katika mifumo rasmi ina dhana pana lakini kwa urahisi kabisa ni kuendesha biashara katika mifumo inayoelezeka. Ni ile hali ambayo mmiliki unapokuwepo ama kutokuwepo biashara inaendelea kama kawaida. Tunagusia usajili rasmi wa biashara na utamaduni wa kuendesha biashara. Kwenye usajili unaweza kusajili kama mfanyabiashara binafsi, kama mshirika na kama kampuni.
Mathalani, Unaposajili kampuni; tayari kampuni inakuwa ni mtu kamili kisheria. Ukiwa na kampuni unapoenda kukopa benki anayekopa ni kampuni na sio wewe mfanyabiashara. Ukishindwa kulipa deni kinachofikishwa mahakamani ni kampuni na sio mmiliki wa kampuni; na wala mali binafsi za mmiliki haziguswi kufidia deni la kampuni.
Tatizo la biashara za sisi wabongo ni kuwa hazitenganishi kati ya mmiliki na biashara. Mmiliki ndio biashara na biashara ndio mmiliki. Mmiliki akifa na biashara lazima ife. Lakini huku kwenye makampuni, kikawaida kampuni huwa haifi kutokana na kifo cha wamiliki wake. Ukifa anaweza kurithi mtoto hadi wajukuu.
Unaposajili biashara zako katika mfumo wa kampuni unaanza urasimishaji wa kiutendaji. Utahitaji uwe na rekodi za kimahesabu, utawala, masoko na rasilimali watu. Mwanzoni unaweza kuwa ukifanya kazi hizi zote peke yako, na mke wako, ama na mshirika wako kibiashara lakini kadiri unavyokuwa kutakuwa na urasmi zaidi na zaidi.
Kwa namna mfumo wa makampuni ulivyo rahisi ni kuwa ukifa leo ama ukiwa haupo mtu yeyote anaweza kutumia kanuni na ndoto zilizopo kuendesha biashara yako. Huu ni mfumo ambao unakuwezesha kumiliki duka Songea hata kama unaishi Dar es Salaam na bado ukawa ukivuna faida bila hata kuibiwa.
Nije sasa kinagaubaga katika suala la biashara na maono (vision). Ili biashara ziwe na dira ya muda mrefu mfanyabiashara anatakiwa kuwa na mipango ya angalau miaka hamsini ijayo. Je, wangapi wana mipango madhubuti ya biashara zao kwa miaka angalau 50 ijayo? Mfanyabiashara anatakiwa kujuwa atakuwa na mtaji wa kiasi gani baada ya miaka 10, 20, 30 na kuendelea.
Ni lazima kufahamu ni nani atarithi biashara ama mali zako pindi ukifariki. Sio tu kumjua lakini kumuandaa huyo mrithi ili nae aje awe na nafasi ya kuwarithisha wengine.. Kama ni mtoto wako, mjukuu ama mtu mwingine. Sio unakuwa na nyumba ya kupangisha halafu ukifa, hao unaowaachia hawakumbuki kujenga zingine zaidi ya kula kodi na kunyanyasa wapangaji tu.
Niharakishe kusema kuwa moja ya mambo ambayo yalisababisha biashara za marehemu ndugu yangu kumfuata kaburini ni kwa sababu hakuwa na ndoto za muda mrefu kuhusu biashara zake. Biashara zilikuwa za kienyeji, hazikuwa na mfumo rasmi, hazikuwa na mipango ya muda mrefu na wala hakumuandaa mapema wa kuzirithi. Tuonane wiki ijayo!
Watazania tunahitaji ushindi wa kiuchumi!