Julai Mosi, mwaka 2015 ilikuwa siku ya historia ya pekee kwangu. Nilipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Rubondo. Safari hii ilikuwa ya aina yake. Juni 28, nilipanda ndege ya Auric Air kutoka Bukoba kwenda Mwanza, ghafla rubani akatangaza kuwa angepitia Rubondo. Ilituchukua dakika 32 kutoka Bukoba hadi Rubondo. Wakati tunatua katika Uwanja Mdogo wa Ndege wa Rubondo, nilishuhudia uoto wa ajabu. Hii ilinivutia.
Niliangalia tena Hifadhi ya Rubondo kwa jicho la husuda wakati ndege inaruka kutoka Rubondo kwenda Mwanza, nikatamani kuwa lazima nirejee Rubondo siku moja na si zaidi ya mwezi, niweze kushuhudia uuambaji wa Mwenyezi Mungu, katika eneo hili la Rubondo. Kwa bahati, nilipofika Mwanza nikakuta mkutano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa wahariri. Nikawasiliana na Meneja Mawasiliano, Paschal Shelutete, akaniunganisha na Muhifadhi Mkuu wa Rubondo, Massana Mwishana.
Julai Mosi, nikiwa na Mwishana tulianza safari ya kutoka Mwanza, hadi Geita Mjini, kisha tukafika katika Kijiji cha Nkome. Hapa ilikuwa miale ya saa 12:40 jioni. Tulipanda boti ya Rubondo. Jua lilikuwa limeanza kuzama. Tulisafiri hadi giza likaingia. Ilifika mahala ikawa tunaona maji tu na mwanga wa nyota na mbaramwezi. Hatimaye tukafika Rubondo.
Nilipelekwa katika moja ya hosteli za Rubondo zenye vitanda vizuri, maji ya moto na mwanga wa uhakika. Wenyeji wangu walinieleza kanuni za kulala ndani ya hosteli hizo. Wakaniambia nisithubutu kuingia ziwani kuogelea wakati wa usiku na wakati mwingine si vyema kufanya hivyo hata mchana kwa sababu ya wingi wa mamba katika eneo hilo. Nikaelezwa kuwa nisishituke kusikia viboko wakila majani nje ya nyumba niliyolala na wakati mwingine kugusa mlango kama kuna mtu anayebisha hodi.
Sitanii, walinidokeza pia kuwa Hifadhi ya Rubondo imejaliwa chatu wa kutosha, wakahitimisha kuwa huo ni utangulizi. Moyo wangu ulianza kwenda mbio. Nilipoingia ndani sikutaka kutoka tena, na hata hivyo hakukuwapo sababu ya kutoka maana kila kitu kipo ndani ya chumba ulichopanga. Nitakuwa mwongo nisiposema kuwa baada ya kusafiri majini, nikapata simulizi za uwapo wa mamba, chatu na viboko, hakika nilipiga sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni…
Usiku nililala usingizi wa mang’amung’amu. Ilipofika saa 5 usiku viboko wakaanza kutoka ziwani na kuja kula majani nchi kavu. Majani yaliyozunguka chumba nilicholala nadhani ni matamu kuliko ya sehemu nyingine. Nilihesabu viboko kama 20 wakipishana kula majani jirani na chumba changu, huku wengine wakigusa mlango sawa na nilivyojulishwa mapema.
Kulikuwapo mbaramwezi. Hakika kwa macho yangu niliona bila kupepesa. Pamoja na woga wa awali, nilishukuru Mungu kupata fursa ya kuwaona viboko kwa karibu kiasi hicho, huku wakinguruma. Si hilo tu, hofu yangu ilizidi kuondoka na furaha kuchukua nafasi, baada ya kufika kwenye mazalia ya samaki, nikaona mamba wengi kwa mara moja wakiwa hai kuliko umri wangu, nikashuhudia uhifadhi wa uoto wa asili uliotukuka, hakika nilifurahi. Nitaeleza baadaye.
Sitanii, asubuhi nilipata chai yenye heshima kutoka mgahawa unaoendeshwa na kina mama wanaofanya kazi Hifadhi ya Rubondo. Baada ya hapo nilikutana na wenyeji wangu kuelezwa historia na utendaji wa Rubondo kabla ya kuanza safari ya kuzungukia hifadhi ya Rubondo na kushuhudia maajabu ya uumbaji wa Mungu, ambayo naamini simulizi pekee haitoshi, ikikupendeza fika Rubondo uone kwa macho yako, kisha upate cha kusimulia maishani.
Tukiwa katika ofisi za Mhifadhi Mkuu Mwishana, nilikutana na Mhifadhi Idara ya Ujirani Mwema, Obokela Mwamjengwa na Mtaalam wa Kuzoesha Sokwe, Shahibu Utenga. Hawa walinipa maelezo ya kina juu ya hifadhi ya Rubondo na historia ya kuanzishwa kwake.
Historia ya kuanzishwa
Wataalam hao walinieleza kuwa miaka ya 1960, dunia ilianza kupata wasiwasi kuwa baadhi ya wanyama wangeweza kutoweka katika uso wa dunia. Wataalam wa Ikolojia waliangalia uwezekano wa kuhamisha baadhi ya wanyama kama tembo na wengine kuwapeleka nchi za Ulaya ikiwamo Ujerumaini, lakini baada ya kulinganisha mazingira na uoto wa asili ikaonekana sehemu pekee duniani ya kuhifadhi wanyama hao na wanapoweza kuishi sawa na maeneo yao ya asili ni Rubondo.
Wakati katika maeneo mbalimbali ya nchi hadi sasa baadhi ya wanyama kama tembo wanapotea kwa ujangili, hali ni tofauti katika Hifadhi ya Rubondo. Kila kukicha tembo waliopandikizwa wanaongezeka. Tembo na wanyama wengine nitakaowataja katika makala hii, walipandikizwa Rubondo kwa nia ya kuwahifadhi na hifadhi hii ilitangazwa rasmi katika gazeti la Serikali mwaka 1977.
Sitanii, Rubondo ni mazalia pekee ya samaki yaliyosalia katika mazingira ya asili ndani ya Ziwa Victoria. Ni moyo wa Ziwa Victoria. Kuna msitu wa asili, maji yaliyotulia na ukiwa kwenye boti unaona vifaranga vya samaki vikiruka juu na kuzama tena ziwani. Katikati ya Msitu wa Rubondo, ndege wanaimba na kufurahia. Wanyama waliopandikizwa katika Hifadhi ya Rubondo wako tofauti na wa sehemu nyingine. Ni wapole, Mhifadhi Mkuu Mwishana, anasema upole huo unatokana na ukweli kwamba hawabugudhiwi kwa kuwindwa hivyo kila anayetalii katika hifadhi iliyoko kisiwani humo wanamuona ni rafiki hawamkimbii wala kumdhuru.
Mhifadhi Obokela anasema mbali na hifadhi hiyo kutangazwa rasmi mwaka 1977, ilianza miaka 10 kabla ya mwaka huo. Wenyeji wa eneo hilo, maarufu kama Banyarubondo waliondolewa kwa tangazo la waziri mwenye dhamana na masuala ya maliasili.
Shirika la Frankfurt Zoological Society la Ujerumani lilifanya utafiti na kubaini hatari ya baadhi ya wanyama kutoweka katika uso wa dunia.
Kati ya wanyama walioonekana wako hatarini kutoweka ni pamoja na sokwe mtu, tembo, farasi na twiga. Kutokana na umuhimu wa kuhifadhi wanyama hao, mwaka 1964 ilibidi serikali kuwaondoa kwenye kisiwa cha Rubondo, Banyarubondo na kuwalipa fidia kazi iliyokamilika mwaka 1965. Mwaka huo Rubondo ililtangazwa kama pori la akiba. Miaka 10 baadaye, yaani mwaka 1977 ikapandishwa daraja na kuwa hifadhi ya taifa.
Hifadhi ina ukubwa wa kilomita za mraba 456.8, ambazo kati yake 236.8 ni nchi kavu na 220 ni majini. Eneo la hifadhi linajumuisha visiwa vidogo 11. Hifadhi hii ipo katika Mkoa wa Geita, lakini baadhi ya maeneo yake kiutawala ni jirani zaidi na Mkoa wa Kagera katika Wilaya ya Muleba, kwa kiwango cha kuwaaminisha watu kuwa iko Mkoa wa Kagera.
Umuhimu wa Hifadhi ya Rubondo
Rubondo ni makazi muhimu ya wanyama waliokuwa katika hatari ya kutoweka si Tanzania tu, bali dunia nzima kama nilivyoeleza hapo juu. Rubondo ni makazi ya ndege na mazalia ya samaki. Samaki wanaovuliwa katika Ziwa Victoria zaidi ya asilimia 80 wanazaliwa katika Hifadhi ya Rubondo. Kwa ufupi, pale Rubondo kuna tani na tani za samaki, lakini kama ilivyo sheria ya hifadhi hairuhusiwi kuvua samaki katika eneo hili, isipokuwa wale tu wanaosafiri nje ya mikapa ya hifadhi.
Kwa wingi wa samaki niliowashuhudia, binafsi nilidhani ningekula au kuchoma samaki, lakini kwenye mgahawa wa Rubondo, nilipewa kuku. Nilipodososa, nikaambiwa wahifadhi wakiwa na hamu ya kula samaki, basi huagiza samaki kutoka Mwanza waliovuliwa nje ya mipaka ya hifadhi. Sikuamini, ila nikakumbuka wakati tunakwenda tulipofika Geita, Mhifadhi Mkuu Mwishana alinunua nyama katika soko la Geita.
Nikushangaze jambo msomaji. Tukiwa ndani ya Hifadhi ya Rubondo niliona mmea ambao ni maarufu sana kwa sasa katika Mkoa wa Kagera, hasa Wilaya ya Bukoba unaoitwa “akarandarugo”.
Nilipouona mmea huu, nikasisimka. Nikakumbuka jinsi Bukoba unavyopaswa kuwa na mlinzi ukimiliki ‘karandarugo’. Wakijua unao, waungwana wanang’oa hadi shina usiku wa manane. Mmea huu unaponya ‘presha, UTI”, unadaiwa kuongeza CD4, na unaelezwa kuponya magonjwa zaidi ya 40.
Mhifadhi mmoja tuliyekuwa naye (jina nalihifadhi kwa sababu za sheria za kitabibu) nilipomweleza sifa za mmea huo, ambao upo kwa wingi Rubondo, akaniambia unaliwa mno na tembo, ila naye anasumbuliwa na shinikizo la damu, lakini akasema: “Kwa kuwa mmea huu upo kwenye hifadhi, nitaangalia unafananaje nione kama naweza kuupata huko nyumbani Musoma niwambie waupande niwe natumia maana hapa kwenye hifadhi hata kama najua unatibu pressure shiwezi kuchuma hata jani lake, ni marufuku na kinyume cha sheria kutoa au kuingiza kitu kwenye hifadhi.”
Kwa hali ya kawaida huku mtaani wangesema ‘hazimtoshi’ kwani dawa ya kumponya ‘presha’ ipo, ila anasita kuichuma kwa ajili ya uhifadhi, ila kwa welede wa taaluma ya uhifadhi, huyu anastahili tuzo.
Anastahili kupandishwa cheo ikiwa ipo ngazi ya juu zaidi ya aliyonayo. Mhifadhi anaamini huruhusiwi kuingiza au kutoa kitu chochote kwenye hifadhi. Hata hao Rubondo walipandikiza wanyama kwa mujibu wa sheria.
Sitanii, hifadhi ya Rubondo imefunikwa na msitu kwa asilimia 80. Hapa mbali na kuwa mazalia ya samaki na ndege, hutumiwa na ndege wanaosafiri masafa duniani kupumzika kabla ya kuruka kwenda kwenye misitu ya Minziro, baadae Kaskanzini mwa Uganda na kuendelea na safari kuvuka jangwa la Sahara ambako ndege wengi hufia njiani kutokana na joto kali na kukosa mahala pa kupumzikia wawapo kwenye hili jangwa.
Wengi hufia jangwani, ila wanaosalia huruka hadi Alexandria nchini Misri, kabla ya kuruka tena kuvuka Bahari ya Mediterranean kwenda Ulaya. Misitu ya Rubondo inatajwa kuwa na uoto sawa na misitu ya Congo (DRC).
Vivutio Rubondo
Hifadhi hii ina vivutio vingi vya utalii. Wamo tembo, twiga, sokwe mtu, mbega na kasuku wa kijivu. Kasuku hawa wana historia ya pekee. Walikamatwa miaka ya 1980 katika Uwanja wa Ndege Nairobi, mwenye nao akawakimbia na dunia ikaamua waletwe Rubondo kuhifadhiwa. Wameendelea kuwapo na wanazidi kuongezeka.
Wengi wa wanyama na ndege waliopo Rubodo wana historia jinsi walivyofika. Sokwe kwa mfano, walipokuwa katika hatari ya kutoweka duniani, walihamishwa kutoka sehemu mbalimbali za Afrika wakapelekwa Ulaya. Kinyume na matarajio, pamoja na matunzo makubwa waliyopewa, badala ya kustawi waliendelea kusinyaa na kufariki. Ilipofika mwaka 1964, Wazungu wakaanza kuwarejesha. Kazi hii ilikamlika kwa kurejesha sokwe 17 katika hifadhi ya Rubondo mwaka 1967. Kwa sasa idadi yao imeongezeka na kuwa zaidi ya 50.
Miaka ya 1980, ujangili ulikuwa mkubwa nchini. Hofu ilitawala kuwa faru wangeweza kutoweka kama hali ilivyo sasa, Serikali ilipeleka faru kadhaa Rubondo. Waliendelea kuwapo, ila walizidi kupungua na wahifadhi wanasema Faru wa mwisho alionekana Rubondo mwaka 1996.
“Hatuwezi kusema waliuawa, ila tunadhani sababu za kiikolojia zaidi ziliwafanya wasiweze kuishi hapa Rubondo,” anasema Mwishana.
Rubondo inao ndege wa aina mbili. Kuna ndege wa kudumu, na ndege wanaohama. Hawa wa kuhama, ukifika msimu hufurika Rubondo kwenye misitu iliyofungana vilivyo, hujenga viota vingi, hutaga mayai, wakatotoa na kuondoka tena kuendelea na safari ya kuzunguka dunia. Ndege hawa wanasafiri katika mabara yote ya dunia hii kwa njia ya mzunguko. Rubondo imewekwa katika kundi la maeneo muhimu kwa ndege (Important Bird Area – IBA) kutokana na maelezo yaliyotangulia.
Sitanii, miaka hiyo Rubondo walihamishiwa tembo wanane. Kutokana na hali ya utulivu, mazalia salama na ulinzi mkali kuzunguka Hifadhi ya Rubondo, ambapo kuna boti za doria nyingi ajabu zinazofanya kazi saa 24, hadi leo hakuna tukio hata moja la ujangili kwa hifadhi hii ya Rubondo.
Tembe wameongezeka kutoka wanane waliopelekwa na kwa sasa wako zaidi ya 100. Wanacheza na miti, kwani wao wanaangusha miti mikubwa kula matunda. Ustawi unaendelea.
Rubongo walipelekwa twiga wachache, lakini kwa sasa kuna makundi kadhaa ya familia za twiga. Katika baadhi ya makundi, wanakuwapo hadi twiga 26.
Nzohe (kwa kihaya Enjobe) wapo Rubondo. Kwa kuwa hawawindwi, wapo wengi ajabu. Inaaminika katika hifadhi zote duniani, Nzohe wamebaki Rubondo pekee. Je, wewe msomaji ulipata kumuona Nzohe, ukiacha hadithi za uwindaji za wazee waliokuwa wanamfukuza tangu asubuhi hadi saa 11 jioni wakiwa na mbwa zaidi ya 20 ndipo achoke wamuue? Ukipenda, unaweza kwenda Rubondo, utaweka historia kwa kumuona Nzohe bila mawaa.
Pongo ni wengi Rubondo. Unaweza kumkaribia na kumgusa, kwani hawakimbii kama swala wa Serengeti. Kuna mamba wengi ajabu. Ikumbukwe hii ni sehemu ya mazalia ya samaki. Mamba kwa kawaida wanaishi kwa kula samaki. Ukiona anakula binadamu au wanyama waliokwenda kunywa maji, ujue ni sawa na anasukutua kwani miaka yote anayoishi, unaweza ukakuta hadi anakufa hajawahi kumla binadamu hata mmoja.
Kuna nguruwe pori, vicheche, nguchiro, sato na sangara wenye uzito wa kutisha. Wahifadhi wanasema wapo sangara wenye uzito wa hadi kilo 112. Nilidokezwa kuwa kwa Rubondo wapo sangara waliokomaa wanakula hadi mamba. Hakika, hii ni moja ya sehemu za kutembelea kushuhudia maajabu haya ya dunia.
Sitanii, kwa kuwa eneo hili lilipata kuwa na wenyeji, asili haijapotea. Bado wazee wanakwenda kwa mitumbwi kutambika. Kuna eneo linaitwa Pongo View, hapa kuna madhabahu, altare na chungu.
Kabla ya wenyeji kuondolewa alikuwapo mganga mkuu wao akiitwa Mukabala. Hadi leo wenyeji wa visiwa jirani kama Maisome na wengine kutoka Mwanza huenda na mbuzi, kondoo na kuku kutambika katika eneo hili.
Kuna mapango yenye mafuvu matatu na mifupa, hii ikionyesha kuwa wakati wa vita watu walikuwa wanakwenda kujificha huko. Kwenye mapango hayo, familia zilizokuwa zinakwenda kutambika ilipotokea mikosi, nuksi, kukosa uzazi na mambo mengine ya aina hiyo, zilifika Rubondo ‘kuangaliwa nyota’ ambako sasa pamegeuka sehemu ya utalii pia. Mwishana anasema uongozi wa vijiji kuna nyakati unapeleka maombi kuruhusiwa kufanya tambiko na huruhusiwa.
Maji kuongezeka
Ukiwa Rubondo unabaini kuwa maji yameongezeka katika Ziwa Victoria. Mwishana anasema maji yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika mito ya Kagera, Mara, Simiyu na Rusumo inayoingiza maji katika Ziwa Victoria kutokana na hatua ya serikali kudhibiti kilimo kisicho endelevu kando kando ya mito. Anasema haya ni matunda ya uhifadhi. Anasema kutokana na uoto wa asili kuimarika, mvua zimenyesha kuliko kawaida na hiyo imeongeza maji. Uhalisia madaraja ya Mlanga na Kasenda (Geita) yamemezwa na maji.
Uongozi wa Hifadhi
Rubondo inazo idara za Ikolojia, Ulinzi na Usalama, ambayo inasimamia usalama wa kisiwa kwa kukamata wahalifu na kuwapaleka mahakamani. Pia wanayo Idara ya Mahusiano na Idara ya Huduma, inayosaidia kuongoza watalii na kutoa huduma mbalimbali kwenye hifadhi. Zipo pia Idara ya Uhasibu, Ununuzi na Utawala na Idara ya Kazi.
Ukitaka kutalii Rubondo
Rubondo inazo boti za kisasa kwa ajili ya utalii na ulinzi wa kisiwa. Usafiri wa kufika Rubondo ni kwa njia ya anga na maji, baada ya kutumia barabara. Kuna uwanja wa Ndege ndani ya hifadhi, ambapo kuna ndege zenye ratiba ya kwenda huko, lakini wakati mwingine watalii wanakodisha. Ukitokea Mwanza, unaweza pia kusafiri kwa basi hadi Geita, kisha ukachukua magari ya kwenda Nkome, ambako unapanda boti ya Rubondo, na kusafiri kwa njia ya maji hadi kwenye hifadhi.
Kwa basi kutoka Mwanza hadi Nkome ni wastani wa saa 4, kisha kulingana na nguvu ya boti anayotumia muhusika kutoka Nkome hadi Kageye, ambapo ni makao makuu ya hifadhi ni kati ya saa 1 hadi saa 1:30 kwa boti ya mwendo kasi. Kwa watalii wanaotokea Bukoba, Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wanapita barabara ya Biharamulo – Bukoba, na wakifika Kyamyolwa wanafuata njia ya Chato, ambako wanakwenda hadi Muganza. Ukifika Muganza hata kwa mguu, unakwenda eneo liitwalo Kasenda unakopanda boti ya hifadhi na kwenda Kagenye. Hapa boti inachukua kati ya dakika 20 na 25 kufika Rubondo kushuhudia maajabu.
Sitanii, kufanikisha ziara hii yanapaswa kuwapo maandalizi ya awali. Mwenye nia ya kwenda Rubondo anapaswa kuwasiliana na hifadhi kwa njia ya email ([email protected]). Sitatunga ni Nzohe kwa Kiingereza, ambaye hapatikani sehemu yoyote kwenye hifadhi za dunia, isipokuwa Rubondo na nilijulishwa kuwa upekee huu katika hifadhii hii ikilinganishwa na nyingine duniani, ndio uliowafanya hata email yao itangaze uwapo wa Nzohe (sitatunga) mnyama anayependwa na watalii duniani.
Kwa watalii wa ndani, kuanzia mmoja hadi saba, wanatozwa Sh 100,000 kwa ajili ya kwenda na kurudi kisiwani Rubondo kupitia Kasenda. Kwa wageni kutoka nje, hutozwa dola 100 kwa idadi ya watu mmoja hadi saba. Kwa wanaopitia Nkome, boti inakodishwa kwa Sh 240,000 kwenda na kurudi, ambayo ina uwezo wa kuchukua hadi watu 12. Kwa watalii wa nje wanatozwa dola 185 kwa idadi hiyo hiyo.
Ukifika Rubondo, kwa watalii wa ndani kila mmoja analala kwa Sh 25,000 kwa siku chumbani, wakati wageni kutoka nje wanalipa dola 35 kwa kila mtalii kwa siku. Hapa chakula watalii wanajitegemea, ila hifadhi inatoa jiko, gesi na vifaa vya kulia chakula bure.
Sitanii, kwa anayetaka raha ya kuona uumbaji wa Mungu, kama nilivyofanya mimi kuna utalii wa aina mbalimbali kama nitakavyoeleza. Kuna njia ya maji kwa boti (boat excursion) au kutembea kwa miguu kisiwani. Zote hizo, kwa mtalii wa ndani analipa Sh 10,000 na wa nje analipa dola 20, kisha mwongoza watalii analipwa 15,000 kwa watalii wa ndani au dola 20 kwa watalii wa nje kwa kundi lote analoliongoza. Gharama ya kutumia boti (excursion) ni dola 110, bila kujali wageni wa ndani au nje.
Iwapo ukiamua kujipa raha kwa kuzunguka hifadhi kwa kutumia gari, watalii wa ndani wanalipa Sh 100,000 na wa kutoka nje wanalipa dola 100 kwa muda wa saa nne. Vivyo hivyo kwa uvuvi wa kitalii, ambapo mtalii awe wa ndani au wa nje anapomvua samaki kutoka majini, anampima uzito na kumrejesha, kitendo hicho anapaswa kulipiwa Sh 10,000 kwa kila anayepanda boti na Sh 200,000 kwa ajili ya kukodisha boti, huku wageni kutoka nje wakilipia dola 25 kila mmoja na dola 110 kukodi boti.
Huduma za kambi na nyinginezo zipo na zinapatikana kwenye mtandao, huku kwa nia ya kukuza utalii Rubondo ikitoa punguzo kwa wanafunzi kulipia Sh 2,000 kuingia kwenye hifadhi na Sh 5,000 kama gharama ya malazi. Ndege zinazotua Rubondo pia zinatozwa Sh 15,000, ingawa gharama inaongezeka kadri ukubwa wa ndege unavyoongezeka pia.
Kukamilika kwa barabara za lami kumepunguza gharama za kutalii Rubondo na kuweka gharama halisi kwenye mtandao kumeongeza idadi ya watalii kwani, zamani ilikuwa mawakala wanatoza hadi dola 900 kwa mtu kutalii Rubondo, lakini kwa sasa mtu anapanda gari kwa Sh 12,000 kutoka Mwanza hadi Geita na anapanda bodaboda Sh 5,000 anafika Nkome na kupanda boti, hali iliyovutia watalii wengi kutembelea Rubondo.
Kwa nia ya kuimarisha ujirani mwema, Hifadi ya Rubondo imekuwa ikisaidia wakazi jirani na hifadhi kwa njia mbalimbali. Imekuwa ikiendesha semina, ikichangia mafunzo kwa viongozi, ikisafirisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo kwenda Rubondo kushuhudia uhifadhi ni nini na umuhimu wa uhifadhi kwa kulinganisha mazingia ya Kisiwa cha Rubondo na visiwa jirani ambavyo havikuhifadhiwa kama Maisome, ambacho hakuna tena mazalia ya samaki na miti imechomwa mkaa.
Hifadhi imetoa misaada kwa njia ya ujirani mwema kama zahanati ya Ikuza (Muleba), mabweni katika sekondari ya Zakia (Nkome), maabara katika sekondari za Kitangiri na Mboka, Buchosa – Maisome (Sengerema) na sehemu nyingine. Wamejenga gati Kasenda kuepusha watu kubebwa na wakati mwingine kutumbukia kwenye maji. Gati hili lilikamilika mwaka 2011 watu wakaacha kutumbukia majini.
Pia, Rubondo imesaidia vifaa kwa Kituo cha Polisi na Mahakama, vitabu kwa shule za sekondari Mwanza na kuunda Klabu za Mazingira, ambapo shule hizi hushindanishwa jinsi ya kuhifadhi mazingira na mshindi wa kwanza hupatiwa Sh 350,000, wa pili 300,000, wa tatu 200,000 na wa nne 100,000. Mshindi wa kwanza hupatiwa safari ya mafunzo huko Saa Nane.
Sitanii, pamoja na kwamba Rubondo wanafanya uhifadhi wa mazingira na kudumisha mazalia ya samaki, kwa sasa wameanzisha Mradi wa Rafiki wa Mazingira, ambapo wanapanda miche ya miti, wanahamasisha majiko banifu na ufugaji wa samaki. Hadi sasa kuna Vijiji na Kambi 14 wanaofuga samaki kando mwa ziwa Victoria na baada ya Nkome kuanza kuhifadhi mazalia ya samaki kwa sasa wanasema samaki wameongezeka.
Ujangili
Uongozi unasema zamani ujangili ulikuwa mwingi ajabu, lakini kwa sasa hali imedhibitiwa baada ya kuwa na vifaa vya kisasa wakifanya kazi kwa saa 24. Mhifadhi Mkuu anasema kwa sasa wanatumia teknolojia ya GPS inayoweza kuwajulisha jangili yupi ameingia kwenye eneo la hifadhi na yuko umbali gani, hata kama ni usiku wa manane wakawasha boti na kwenda kumkamata.
Mbali na GPS hifadhi imeingia gharama ya kununua darubini zenye kuona hadi gizani usiku, hivyo mvuvi yeyote anapoingia tu kwenye mipaka ya hifadhi, Mwishana anasema anaonekana mara moja na kukamatwa. Anasema nusu ya wafungwa na mahabusu waliopo katika Gereza la Geita, wamekamatwa kwa kosa la ujangili wa samaki.
“Ujangili unapungua, tunafanya doria usiku na mchana, majini, nchi kavu na angani – kwa macho yetu na kwa kutumia viona mbali kwa ajili ya kulinda rasmali ya taifa na tumewashinda, ingawa bado wapo wachache na tunaendelea kuwakamata, wamepungua mno,” anasema Mwishana.
Wito anaotoa Mwishana ni kudhibiti umaskini. Anasema baadhi ya watu wanafanya ujangili kwa kukosa kazi za kufanya. Anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau ikiwaanzishia miradi mbalimbali kama ufugaji wa samaki, kuku na wanyama wengine, basi watu wataondoa umaskini na hawatakuwa na hamu ya kujihusisha na ujangili wakati wana fedha, ilihali wakijua matokeo yake ni kuishia gerezani.
Nilichokishuhudia Rubondo
Nikiwa Rubondo, nilifanikiwa kufika kwenye Kisiwa cha Mamba na Kisiwa cha Ndege. Hakika kama mnavyoona picha nilizochapisha, utapenda. Ingawa woga unakuingia, lakini inafurahisha kushuhudia mamba zaidi ya 20 kwa mara moja wamejianika juani. Visiwa vya mamba viko viwili. Vyote hivi vinaelekea kuzama majini kutokana na wingi wa maji.
Kutokana na hali hiyo, nafasi iliyobaki juu ni ndogo. Mamba kwa kuwa muda wote anaishi majini hulazimika kuota jua kwa ajili ya kurejesha joto mwilini linalopotea akiwa majini. Kwa maana hiyo, wanakusanyika kwa wingi katika jiwe moja lilosalia juu ya maji kujianika baada ya kuwa wameshiba samaki. Ukiwa Rubondo unaona mamba wengi kwa mara moja hadi unastaajabu.
Mazalia ya samaki pia yamehifadhiwa. Kuna utando wa kijana juu ya maji, ambao unaona vifaranga vya samaki vikiruka na kutambaa kwa raha zake. Ndege pia, wamezingira visiwa viwili kwa kiwango cha kufurahisha. Kuna ndege wengi wenye rangi na sauti za kuvutia, hadi kama una mawazo yanapotea bila kujua, sawa na alivyoandika mwandishi maarufu wa vitabu James Hadley Chase kwenye kitabu chake kitwacho “Have a Change of Scene” akimaanisha badili mazingira.
Pia nilishuhudia miti iliyokomaa, ambayo kwa maajabu ya Mungu inaangushwa na tembo kula matunda yake. Msitu ulivyosukana, ulinikumbusha mbili kati ya safari zangu za Kwenda Lubumbashi na Kinshasa, huko DRC nilikoshuhudia mawingu mazito yametanda hadi ndege inacheza shere kuyakata lakini kadri unavyotua unashuhudia misitu iliyokomaa na kufungana, na hilo ndilo nililolishuhudia Rubondo, ila kwa upande wa pili ukitupia jicho kisiwa jirani cha Maisome ambacho hakikuhifadhiwa, unakiri wazi umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Si hayo tu, bali nilipata fursa ya kupita katika eneo la Irumo, linalotajwa kuwa na kina kirefu kuliko sehemu yoyote katika Ziwa Victoria. Mwonekano wa V wa eneo hili, na mkatiko wa mwamba unaozaa kina kirefu, ni kivutio cha aina yake.
Mwisho si kwa umuhimu, ni uungwana na ukarimu wa wafanyakazi wa hifadhi ya Rubondo. Pamoja na upweke walionao, kwa maana hakuna gari, pikipiki, baiskeli au chombo chochote cha usafiri nje ya boti za hifadhi inayoingia Rubondo hivyo mfanyakazi akiishaingia Rubondo ni kazi tu, bado ni wachanamfu.
Hawezi kuchepuka maana Rubondo kwa kuwa na samaki wengi kisiwa kimezungukwa na mamba hivyo hata wataalam wa kuogelea kama kutoka Ukerewe wanapofuga “Kakira” hawawezi kuthubutu kuogelea kwenda nchi kavu. Wakithubutu mamba wanawafanya asusa.
Sitanii, bado wafanyakazi hawa ni wachangamfu. Wanajua kupokea wageni. Ingekuwa amri yangu, nigewaongeza mshahara mara mbili ya hifadhi nyingine. Ukitaka kuitendea haki nafsi yako, nenda Rubondo ukasuhudie maisha yalivyo na ujifunzi kuondokana na umaskini kwa kufuga samaki. Katika maandalizi unaweza kuanzia hapa www.tanzaniaparks.com.