Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amehutubia Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaondelea Jijini New York nchini Marekani.
Makamu wa Rais ametoa hotuba hiyo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Akitoa hotuba hiyo, Makamu wa Rais amesema Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla zinahitaji mabadiliko ya haki na ya utaratibu katika kufikia matumizi ya nishati mbadala kwa kuzingatia hali za Maisha ya watu wa bara hilo wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa nishati hizo.
Ametoa wito wa kuondolewa kwa upinzani dhidi ya ufadhili wa kimataifa katika utekelezaji wa miradi ya mageuzi katika nchi za Afrika ambayo inalenga kutumia rasilimali ikiwemo gesi kwaajili ya nishati na matumizi mengine katika kufikia maendeleo.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba biashara ya hewa ukaa barani Afrika inapaswa kufanyika kwa uwazi na kuwanufaisha wananchi waliotunza mazingira na misitu inayozalisha hewa hiyo kwa matumizi ya dunia huku akiitaja Tanzania kama nchi iliowekeza zaidi katika uhifadhi wa misitu ambapo asilimia 30 ya eneo la ardhi ya taifa hilo imehifadhiwa.
Katika kudumisha amani na usalama, Makamu wa Rais amesema Tanzania siku zote inaamini kuwa diplomasia na meza za mazungumzo ndiyo chombo bora cha kutatua migogoro duniani.
Amesema licha ya migorogoro iliopo duniani mataifa yanapaswa kulinda maisha ya binadamu hasa watoto na wanawake pamoja na ustawi wa watu.
Aidha ameongeza kwamba ni muhimu kushiriki katika kutafuta utatuzi wa migogoro kwa amani ili kukabiliana na athari zitokanazo na migogoro hiyo kama vile ongezeko kubwa la bei za chakula na mafuta pamoja na kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na viwanda duniani kote.
Makamu wa Rais amesema katika kulinda amani Tanzania inajivunia kuchangia Askari katika misheni 5 kati ya 16 zilizopo za kulinda amani duniani kote na kueleza kwamba taifa lipo tayari kuchangia zaidi iwapo itaombwa kufanya hivyo na kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuongeza uungaji mkono wake kwa juhudi za kikanda katika za kujenga na kulinda amani.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kuchelewa kwa Afrika katika upatikanaji wa chanjo za Uviko19 wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo kunasisitza hitaji la Nchi za Kiafrika kufanya kazi pamoja katika ukuzaji wa masuluhisho asilia kupitia utafiti wa pamoja wa kisayansi.
Amesema ugonjwa huo pia uliweka wazi hitaji la kuwekeza zaidi katika elimu ya afya ya umma hususani dawa za kinga ili kujenga ustahimilivu wa mtu binafsi ikiwa ni pamoja na usawa wa mwili, lishe bora na tabia.
Pia Makamu wa Rais ameshuruku misaada wa kimataifa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kukabiliana na kuenea kwa janga la Uviko19 kupitia utoaji wa vifaa vya uchunguzi, dawa, programu za msaada wa chanjo, ambazo zimekuwa muhimu katika kushinda vita dhidi ya janga hilo.
Vilevile Makamu wa Rais amepongeza juhudi za Umoja wa Mataifa katika kukuza lugha ikiwemo tamko la kihistoria la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) lililoitaja “7 Julai” kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani.
Ametoa wito kwa mataifa kuweka vipaumbele vya vitendo hasa kwenye malengo ya maendeleo endelevu ambapo amayasihi mataifa kujitolea kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa na Nchi Wanachama wake, kwa nia ya ushirikiano na mshikamano wa kimataifa kuelekea mustakabali endelevu.