Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekaimu Urais wa Tanzania tangu Septemba 17, 2022 hadi Rais Samia Suluhu Hassan atakaporejea nchini, JAMHURI DIGITAL imeambiwa.
Rais Samia aliondoka nchini Septemba 17, 2022 kwenda kushiriki maziko ya Malkia Elizabeth II nchini Uingereza, ambapo baada ya mazishi pia amekwenda nchini Msumbiji kwa ziara ya siku 3 aliyoianza Septemba 21, 2022.
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango aliyestahili kukaimu Urais kikatiba, baada ya Rais Samia kuwa nje ya nchi, naye yuko ziarani nchi Marekani, akimwakilisha Rais Samia, ambapo atapata fursa ya kuhutubia Umoja wa Mataifa (UN) kwa niaba ya Rais Samia.
Kaimu Rais, Waziri Mkuu Majaliwa alipoulizwa na JAMHURI DIGITAL, amejisikiaje kukaimu Urais katika muda ambao viongozi wake wawili hawapo, amesema:
“Mimi na mawaziri wenzangu tunayo kazi ya kumsaidia Mhe. Rais, mama yetu, Mama Samia kufanikisha utekelezaji wa majukumu yote ya Serikali muda wote, iwe yuko ndani ya nchi au nje ya nchi.
“Kukaimu Urais, ni jukumu ninalolifanya kwa mujibu wa Katiba na kwa unyenyekevu mkubwa. Namshikia kiti Mhe. Rais, akirejea yeye au Mhe. Makamu wa Rais nakabidhi na kuendelea na majukumu ya kumsaidia kwa wadhifa alionipa kwa mujibu wa Katiba,” amesema.
Katiba ya Tanzania (1977) kama ilivyorekebishwa, inasema endapo Rais wa Jamhuri ya Muungano yupo kwenye majukumu nje ya Jamhuri, Makamu wa Rais atakaimu Urais.
Na ikiwa Rais na Makamu wa Rais wote hawapo nchini basi Waziri Mkuu anakaimu Urais, hali inayotokea sasa.
Ibara ya 37(3)&(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inaweka utaratibu wa kukaimu Madaraka ya Rais:
(3) Endapo Rais atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano au atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu nyingine yoyote, kazi na shughuli za Rais zitatekelezwa na mmojawapo wa wafuatao kwa kufuata mpangilio ufuatao, yaani-
(a) Makamu wa Rais au kama nafasi yake iwazi au kama yeye hayupo au ni mgonjwa; basi;
(b) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.
Waziri Mkuu atadumu katika mamlaka hayo mpaka pale mmoja kati ya Rais au Makamu wa Rais atakaporejea naye ataacha kuhudumu katika mamlaka ya Rais na kurejea kwenye nafasi yake ya Uwaziri Mkuu kama iliyoainishwa kwenye ibara ya 37 (4)(a)&(b).
(4) Endapo Waziri Mkuu ndiye atatekeleza kazi na shughuli za Rais kutokana na sababu kwamba Makamu wa Rais hayupo, basi Waziri Mkuu ataacha kutekeleza kazi na shughuli hizo endapo lolote kati ya mambo yafuatayo litatokea mwanzo-
(a) Rais atakaporejea katika Jamhuri ya Muungano au atakapopata nafuu kutokana na maradhi na kuanza kutekeleza kazi za Rais;
(b) Makamu wa Rais atakaporejea katika Jamhuri ya Muungano.
Kwa mantiki hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ataacha kutekeleza mamlaka ya Rais, iwapo mmoja kati ya Rais na Makamu wa Rais atarejea nchini.