Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Mtifuano mkali unaotajwa kuwa na viashiria vya kunyemelea madaraka unaendelea ndani ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambapo kundi la wafanyakazi waliohamishwa baada ya mifuko kuunganishwa wamefikisha malalamiko kwenye Baraza la Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya viongozi wakuu wa PSSSF. Mifuko iliyounganishwa kuunda PSSSF ni GEPF, LAPF, PPF na PSPF.
JAMHURI linafahamu kuwa walioshitakiwa mbele ya Baraza ni Mkurugenzi Mkuu, Hosea Kashimba, Mkurugenzi wa Fedha, Beatrice Lupi, Mkurugenzi wa Tehama, Gilbert Chawe na Mkurugenzi wa Manunuzi, Ernest Kasombi. Miongoni mwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya viongozi hao ni kutumia madaraka vibaya.
Watoa tuhuma wanadai kuwa viongozi hao wa PSSSF wamejikopesha magari bila kuwapo sera ya mikopo, bila kuwapo bajeti, bila sera hiyo kuidhinishwa na Msajili wa Hazina na Katibu Mkuu Utumishi, huku mfuko huo ukiwa hauna fedha za kutosha kulipa mafao.
Wakurugenzi kukopeshwa magari
Wanadai Mkurugenzi Mkuu Kashimba alinunua gari la ofisi Toyota Land Cruiser VXR Septemba 2020 na Desemba akajikopesha gari kama hilo la binafsi, huku mfuko huo ukiwa na magari mengi na ukiwa hauna fedha za kutosha za kulipa mafao ya wanachama.
Wanasema magari yote waliyokopeshwa wakurugenzi yanafikia karibu Sh milioni 700 na kwamba sera ya kukopesha magari inatumika pale ambapo ofisa hapewi gari la ofisi.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Bodi ya Wadhamini ya PSSSF ilikutana Novemba 13, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi, Ghorofa ya Nne, jengo la PSSSF, Dodoma na kupitia ajenda Na. 5/9/2020 ya kikao hicho waliridhia mkopo wa magari kwa wakurugenzi sita, ambao ni Mkurugenzi Mkuu, Hosea Kashimba; Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Vupe Ligate; Mkurugenzi wa Usimamizi wa Hadhari na Majanga, Ansgar Mushi; Mkurugenzi wa Fedha, Beatrice Lupi; Mkurugenzi wa Tehama, Gilbert Chawe na Mkurugenzi wa Manunuzi, Ernest Kasombi.
Bodi ya Wadhamini ilijiridhisha kuwa kwa Mkurugenzi Mkuu Kashimba, chini ya kifungu cha 4.3.7 cha mkataba wake, anastahili kukopeshwa gari na hata wakurugenzi wa mifuko wengine waliomtangulia nao walikopeshwa magari, hivyo isingeweza kuwa tofauti kwake pekee. Bodi ilifikia uamuzi huo baada ya mashauriano na serikali ikakubalika kuwa itumie Sera ya Mifuko iliyokuwapo awali kabla ya kuvunjwa, ambapo sera hiyo inaendelea kutumiwa na NSSF.
Pamoja na masharti mengine, bodi iliwataka wakurugenzi wanaokopeshwa mikopo hiyo ya magari kukatiwa Bima ya Maisha, kwa maana likitokea la kutokea kabla mhusika hajamaliza kulipa mkopo huo ndani ya miaka mitano, bima ndiyo ilipe mkopo huo.
Pia kwa mujibu wa sera, wakurugenzi hao wanakopeshwa kiasi kisichozidi mishahara yao 24, utaratibu uliotumika kwa wakurugenzi wote waliotangulia.
JAMHURI limebaini kuwa kati ya kundi la wanaoongoza mashambulizi dhidi ya Kashimba na wakurugenzi wenzake, baadhi walikuwa waajiriwa wa mifuko kabla ya kuunganishwa wakahamishiwa vituo vingine vya kazi serikalini, ambao nao wamepata kukopa fedha za magari kwa utaratibu huo huo. “Tena la ajabu kabisa, wakurugenzi wawili walipohamishwa kutoka kwenye mifuko wamegoma kabisa kuendelea kulipa mikopo yao.
Mkopo ule una riba ya asilimia 5, mmoja deni limekua hadi Sh milioni 525 na mwingine limefikia Sh milioni 320.
Soma zaidi hapa (ukurasa wa 3)