Maswali mengi yameibuka kuhusu kifo cha Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Ujambazi Mkoa wa Morogoro, Mrakibu wa Polisi (ASP), Elibariki Pallangyo (53).

JAMHURI imedokezwa kwamba kifo cha bosi huyo kimezua maswali mengi kutokana na mazingira ya namna kilivyotokea, kwani baada ya majambazi hao kuvamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia Jumanne, hawakumdhuru mtu mwingine zaidi ya yeye.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya uhakika kutoka kwa watu wa karibu na marehemu, alifikwa na mauti hayo saa chache baada ya kutoka katika shughuli zake binafsi.

“Kabla hajafikwa na mauti, Pallangyo alikuwa nje ya nyumba yake na alirejea baadaye usiku, lakini cha ajabu alipofika nyumbani kwake Yombo saa chache baadaye alivamiwa na majambazi na kuuawa.

“Hata hivyo, cha ajabu ni kwamba majambazi walipovamia nyumba yake hawakumdhuru mtu mwingine yeyote zaidi ya Pallangyo mwenyewe, hivyo hali hii inatia shaka kwamba huenda kukawa na kisasi au vinginevyo,” kilieleza chanzo kingine cha habari ambacho JAMHURI imelinda jina lake.

  Hata hivyo, habari nyingine kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinapasha kwamba Pallangyo anadaiwa kuaga katika kituo chake cha kazi kwamba anakwenda Dar es Salaam ambako familia yake inaishi kuuguza mgonjwa.

Lakini taarifa hiyo ya awali inakinzana na nyingine ambayo inaeleza kwamba baada ya kufika nyumbani kwake asubuhi ya siku aliyokumbwa na mauaji hayo, Pallangyo anadaiwa kumuaga mkewe kwamba anakwenda mahakamani kutoa ushahidi.

  “Ndugu yangu, mazingira ya tukio hili yanatia shaka, ninachoweza kusema mimi ni kwamba kwa kuwa jamaa amewahi kufanya kazi kwa muda mrefu hapa Dar es Salaam, katika kitengo cha kuzuia ujambazi (Anti-Robery), amekuwa na kesi nyingi ambazo mara kwa mara amekuwa akishughulika nazo mahakamani ama kwa kutoa ushahidi au la, lakini alipokuja safari hii sijafahamu kama alikuja kwa ajili ya ushahidi.

“Kikubwa ninachofahamu ni kwamba amejenga makazi yake Yombo Kilakala, Dar es Salaam na alifika hapa jijini akitokea katika kituo chake cha kazi Jumamosi, Agosti mosi usiku, kisha kuungana na familia yake, lakini alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumanne, Agosti 4,” kimeeleza chanzo hicho cha habari.

Chanzo hicho kimeeleza kwamba baada ya majambazi kufika nyumbani kwa Pallangyo na kufanikiwa kukiona chumba chake, walimpiga risasi na kama hiyo haikutosha waliona kama hajafa, ndipo walipoamua kummalizia kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Hata hivyo, chanzo hicho cha habari kinapasha kwamba baada ya majambazi hao kuvamia nyumbani kwa Pallangyo, walimsaka sana na kufanikiwa kumkuta katika moja ya vyumba, lakini kabla hawajammiminia risasi alijificha nyuma ya mlango.

Chanzo hicho kinasema majambazi hao hawakumwona ndipo kwa ujasiri wake alifanikiwa kumjeruhi jambazi mmoja kwa kumkata kwa panga mkononi na kumfanya avuje damu nyingi na ndipo waliporudisha mashambulizi kwake na kufanikiwa kumuua.

“Pallangyo alimkata panga jambazi mmoja na hali hiyo ilizidisha machungu kwa mjeruhiwa na wenzake kwani baada ya kitendo hicho jambazi huyo alisikika akilalamika kwamba ‘nimekatwa panga na sasa namuua huyu mtu’ na ndipo azma hiyo ilipotimia baadaye kwani askari waliokwenda kuchunguza kuhusu tukio hilo walikuta kukiwa na alama za damu,” kimeeleza chanzo hicho cha habari.

Inaelezwa kwamba kabla hajahamishiwa Morogoro, Pallangyo alikuwa akifanya kazi Dar es Salaam kwenye Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Ujambazi. Alihamishiwa Morogoro baada ya kupandishwa cheo.

Akithibitisha kutokea kwa kifo cha bosi huyo wa polisi hivi karibuni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Andrew Satta, amesema Pallangyo alifariki dunia papo hapo baada ya kufyatuliwa risasi kifuani.

Kamanda Satta alisema kwamba majambazi hao waliokuwa katika kundi la watu zaidi ya 10, walivamia nyumbani kwa Pallangyo kwa kuruka ukuta na kisha kuvunja mlango na kuingia ndani kabla ya kufanya mauaji.

Ameeleza kwamba baada ya uvamizi huo majambazi hao wanaonesha kwamba walikuwa na nia na Pallangyo tu, kwani baada ya kuingia ndani kwake walichukua Sh. 130,000 pamoja na simu nne za mkononi ambazo ni mali ya wasichana wanne waliowakuta ndani ya nyumba hiyo, kisha kuelekea kwenye chumba cha Pallangyo na  kufanya mauaji hayo na kutokomea kusikojulikana.

Kamanda Satta amesema kwamba baada ya kutimiza azma yao, majambazi hao walisahau kifaa kinachotumika katika milipuko.

Kutokana na tukio hilo, tayari Jeshi la Polisi kupitia Naibu Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, limetangaza kuwakamata watu watatu ambao inadai wamehusika katika mauaji ya ofisa Pallangyo.

Mauaji ya bosi huyo wa polisi ni mwendelezo wa matukio ya mauaji ya askari polisi kunakodaiwa kufanywa wa raia wasio na imani na jeshi hilo, jambo ambalo limezua maswali mengi kwa jamii.

Miongoni mwa matukio yaliyotikisa ni lile lililotokea katika Kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga baada ya baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuwaua askari polisi wanne na raia watatu kisha kupora silaha zaidi ya 20.

Hata hivyo, wadadisi wa mambo wameyahusisha matukio hayo na visasi vinavyodaiwa kufanywa na majambazi dhidi askari polisi, na wengine wamekwenda mbali zaidi kwa kuyahusisha matukio hayo na visasi miongoni mwa vigogo wa jeshi hilo dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu.