Wanasiasa kadhaa waliokuwa makada na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama kadhaa vya upinzani wilayani Karagwe na Kyerwa wamejisalimisha na kujiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumfuata mwanasiasa mahiri nchini, Edward Lowassa.

Dhana kubwa ya wanasiasa hao ni kuamini kuwa kwa kwenda Chadema, wanaweza kufanya vema katika uchaguzi mkuu ujao huku wakidai CCM imepoteza dira na mwelekeo kwa sababu ya kukiuka kanuni na taratibu hasa katika uchaguzi wa ndani wa mwaka huu.

Aliyekuwa Diwani Bugene, Karagwe Aristides Muliro, anasema, “Alama za nyakati zinajionyesha wazi. Mazingira ya sasa ya rushwa na mizengwe ndani ya CCM, vimenitoa huko na nimeamua kujiunga Chadema.” Kwa nafasi aliyoshika hiyo, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.

Kujiengua kwa kiongozi huyo Chadema, kumeongezea CCM maumivu makali wakati wa kura za maoni za udiwani Kata ya Bugene ambako Muliro  amepita kwa kishindo kwa kupata kura 92 kati ya kura 138 huko akiwaacha wana CCM kumtafuta mgombea anayeweza kushindana naye.

Madiwani wengine maarufu waliojiunga Chadema ni Adventina Kahatano kutoka CUF wakati Prudence Mweyunge na Consoratha Kanyima wa TLP nao walijiunga na makamanda hao wa vuguvugu la mabadiliko (M4C).

Ripoti kutoka sehemu mbalimbali katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa zinasema kuwa hatua ya Lowassa kutoka CCM na kujiunga na Chadema imewavuta pia wananchi wa kawaida kama vile Jackie lshengoma (38) wa Tarafa ya Mabira anayesema, “Lowassa ameonesha ujasiri na kihistoria katika siasa za nchi yetu.”

Wakati huo  huo, vikundi  vya hamasa kutoka  CCM na  Chadema vinapishana kwa  mbwembwe kuhamasisha wananchi kushiriki katika mikutano ya kuwanadi na kuwachagua wagombea wao katika urais, udiwani na ubunge.

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Deodatus Kinawiro amehutubia wananchi wa wilaya hii akiwataka wahimize amani  wakati wa uchaguzi.

Kinawiro aliyehutubia katika kijiji cha Bujuruga, Kata  ya  Bugene,  anasema, “Ninawataka   na  kuwaasa wagombea  udiwani  na   ubunge wasitumie  fujo  na lugha chafu za matusi, ili uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015  ufanyike katika hali ya usalama na utulivu.”