JKNeno mamluki limekuwa linatumika zaidi kwa askari wa kukodishwa hapa ulimwenguni. Wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linasherehekea mwaka wake wa tano tangu kuasisiwa kwake  Septemba 1, 1969, Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Julius Nyerere, alitamka neno “MERCENARY” hapa nchini.

  Hebu tujikumbushe kwanza alivyosema Amiri Jeshi Mkuu; “Askari wako wa aina mbili. Lakini ingawa nazungumza habari za askari, kila mfanyakazi asikilize nitakavyosema, ajijue mwenyewe. Wako askari wa fedha, huitwa “mercenary”, na yuko tayari kufa, yuko tayari hata kuua kwa sababu ya fedha anayolipwa.

Leo anaweza kuwa upande huu akapigana na wale; kesho wale wa kule wakimuwahi, kumwambia huko unalipwa nini? Akawaambia, huku nalipwa kadhaa. Wakamwambia huku tutakulipa mara mbili. Atageuka atakwenda kule. Huyu huitwa askari wa fedha (ndiyo mamluki), anapigania fedha. Sisemi askari tu lakini tuko wengi ambao sasa hivi naweza kusema ni wafuata fedha (au madaraka).

Mathalani, nikiwa mwalimu, nataka fedha, ikitokea nchi fulani ikaniambia, mwalimu njoo sisi tutakulipa mara mbili ya mshahara wako. Huyo nafunga virago nakwenda zangu kufundisha mahali pengine. Hapo nakuwa mwalimu wa fedha. Basi mwalimu nafuata fedha ni mamluki tu.”

Akaendelea kusema: wa pili askari mzalendo, naye lazima alipwe mshahara, ale, lazima avae, akae katika nyumba. Lakini huyu yuko pale analinda nchi yake, anaipenda nchi yake, yeye yuko pale tayari kuua kama hapana budi si kwa sababu ya fedha ila kwa sababu ya nchi yake. Huyo ni askari ‘MZALENDO’; ndiye tunayemtaka sisi.” (Taz. Ujamaa ni Imani Na. 1 uk. 69 – 70).

Sasa Mwalimu aliposema na wafanyakazi wengine (kama ule mfano wa mwalimu) wajijue wenyewe alitaka kuonesha kishawishi cha fedha kinavyoweza kuwahadaisha watu kuhama hama kutoka kazi moja na kwenda kwenye kazi nyingine. Si wito wa kuipenda kazi yenyewe, bali wenyewe siku hizi wanasema kutafuta unafuu wa maisha (in search for green pasture).

  Kumbe tamaa ya fedha inaondoa ule moyo wa uzalendo wa kuhudumia wengine kwa vile hakuna wito na kazi ile. Tabia ile ya kufuata fedha iwe kwa askari au kwa mfanyakazi yeyote mwingine inafananishwa na ule mvuto wa askari mamluki kutafuta fedha tu ndiyo unaojulikana kama UMAMLUKI – mercenary. Basi umamluki uko hata katika siasa.

  Hivyo, mamluki wanaweza kuwa walimu, madaktari, watawala na kadhalika. Hata wanasiasa wanaohamahama chama kimoja kwenda chama kingine cha siasa, wanavutwa na uchu au tamaa ya madaraka. Na madaraka jamani, bila kudanganyana yanaendana na heshima na kipato. Chairman wa chama anapata zaidi ya Katibu au Mtunza Fedha. Basi, chama kile kikishika dola hapo kiongozi wa chama “automatically” anakuwa mkuu wa nchi, na mshahara hapo unakuwa mkubwa. Madaraka ni heshima pamoja na mshiko pia.

Dokta mmoja wa Chuo Kikuu Huria aliandika hivi: “Mtu kuhama chama fulani na kuhamia chama kingine kuna sababu mbili ambazo ni a) kutafuta fursa ya kufanya ambacho mhusika alikokuweko awali asingeyafanya; na b) ni tamaa ya madaraka ambayo mwanachama husika alipokuwa kwenye chama kimoja alitamani kuyapata, lakini kutokana na sababu kadhaa ikiwamo kupanuka kwa demokrasia, hali inayotoa fursa kwa mwanachama mwingine kupewa madaraka hayo. Hapo mwanachama muhusika anakihama chama ‘A’ na kwenda chama ‘B’ ili kupata madaraka anayoyanuia kwenye hicho chama kingine. (Dk. Lazaro Swai katika Uhuru toleo No. 22195 la Jumatano Julai 29, 2015 Uk. 4).

  Hii tabia ya kutafuta madaraka imeonekana kihistoria duniani kote kuwa ni mojawapo ya vyanzo vya mitafaruku ulimwenguni. Historia ya wanasiasa wanaotamani madaraka kwa kutumia njia yoyote ile imekuja kuonekana kuwa ni ya viongozi wapenda ubabe na utawala wa kidikteta. Wakishapata hayo madaraka wanaandaa mfumo kandamizi unaowawezesha viongozi namna hiyo kubadili katiba za nchi kwa maslahi yao tu.

  Mifano hai imekuwapo kule Italia enzi za Benito Mussolini, Ujerumani enzi za Adolf Hitler, huku kwetu barani Afrika nchi kama Jamhuri ya Afrika ya Kati enzi za Jean Bédel Bokassa, jirani yetu nduli Idi Amin Dada wa Uganda, Mzee Kamuzu Banda wa Malawi na wengine chungu nzima. Hawa kwa kutamani madaraka wametawala kiimla tu na hata kutesa wapinzani wao alimradi waendelee kutawala. Ni uchu wa madaraka uliowafanya wawe hivyo. Athari zake zimeleta machafuko katika nchi zao na kuharibu uchumi pia.

  Wakati akiwa Dodoma Mei 25, 2015, Mheshimiwa Edward Lowassa alizungumza na vyombo vya habari alinukuliwa kusema wazi wazi: “Sitahama CCM, asiyenitaka ndiye aondoke kwenye chama. Mimi nina uhakika wa kupata nafasi ya kuwania urais” (Tazama Uhuru: Toleo No. 22195 la Jumatano tarehe 29/07/2015 ukurasa wa mbele kabisa).

  Kwa usemi huo tu inadhihirika wazi kuwa Mzee Lowassa ni kada wa CCM tangu ujana wake. Historia aliyowaelezea wana vyombo vile vya habari siku ile pale Dodoma inamwonesha Lowassa tangu ahitimu Chuo Kikuu Mlimani mwaka 1977 mpaka hivi sasa hajawahi kufanya kazi nje ya CCM.

  Kwa mazoea na makuzi aliyopata ndani ya CCM ndiyo maana alisema kwa kujiamini kabisa maneno kama: “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina plan ‘B’, mimi ni plan ‘A’ tu. Sisi ni chama dola, tumefanya mambo wengi mazuri.” Lakini akawaonya wenzake ndani ya CCM kwa kusema: “Meseji yangu kubwa kwa chama changu, tusifanye mchezo, tusibweteke badala yake tufanye kazi kubwa zaidi….” (Tazama Raia Mwema toleo No. 416 la Julai 29/07/2015 uk. 2).

  Mpaka hapo ameonesha kutumaini sasa kukamilisha ile safari yake yenye matumaini aliyoianza kule Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kabla ya vile vikao vya Dodoma.     Tunakubaliana sana na Mheshimiwa Edward Lowassa maana anakiri wazi wazi kuwa CCM ni chama dola, na anakishauri kisifanye masihara na uchaguzi ujao.

Tujiulize, nini kilichomfika kada huyu wa chama hata akaja kubadilika ghafla na tukamshtukia yuko kule Bahari Beach anajiunga na chama cha upinzani – CHADEMA? Kwanza CHADEMA ilikuwa hasimu wake mkubwa. Katibu Mkuu wa CHADEMA amediriki kumkashifu vibaya sana pale Mwembe Yanga eti Lowassa alikuwa ni mmoja wa mafisadi wakubwa hapa nchini. Jina lake likawa kati ya mafisadi katika orodha inayojulikana kama “ORODHA YA FEDHEHA”. Yeye alisema “hana plan B”.

  Sasa huko kuingia CHADEMA ni plan gani? Bado tunajiuliza ni DHARURA katika kuokoa jahazi? Maana hakuwa na “fallback” plan wakati ule anaongea pale Dodoma. Bado sijaelewa kilichomsukuma kada huyu hata ageuke ghafla, tunasema amegeuka (about turn) au amefanya “somersaulting” ya kisiasa.

  Tukashtukia ghafla tu yuko Bahari Beach kwenye mkutano wa CHADEMA. Mzee wa watu Julai 28, 2015 akapokewa kuwa mwanachama mpya wa CHADEMA. Ndipo alipofikia hatua ya kutamka mbele ya kadamnasi ya wana-CHADEMA na wana-UKAWA maneno haya: “NIMEKIHAMA CHAMA” kilichonilea tangu ujana wangu”.  

  Akaendelea hata kutumia yale maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, pale alipotamka kuwa CCM haikuwa baba wala mama yake. Basi, Mzee Edward Lowassa naye alikaririwa kutamka: “CCM siyo baba wala siyo mama yangu”.

  Ninashindwa kupambanua msingi wa ulinganisho wa matamshi ya viongozi wawili hawa. Baba wa Taifa kweli alitamka maneno namna ile LAKINI KAMWE HAKUKIHAMA chama chake. Wakati Mzee Lowassa ametamka maneno yale na kukihama chama chake! Sielewi kisawa (synonymity of their actions) cha matamshi ya viongozi hawa wawili maana hayafanani kamwe kimatendo. Nimetoka kapa kabisa hapa. “I am very baffled” ndiyo mshangao wangu!

  Aidha, nikitazama upande wa viongozi wakuu wa CHADEMA, waliompokea, napo sielewi kitu kabisa. Wananchi bado tunakumbuka tuhuma nzito sana Katibu Mkuu wa CHADEMA alizotoa pale Mwembe Yanga Septemba 15, 2008 katika mkutano wa hadhara. Pale Mzee Lowassa alikuwa mmoja wa viongozi wa CCM na Serikali waliotajwa kwa UFISADI.

  Ilitolewa ORODHA inayojulikana kama “List of Shame” au ORODHA YA FEDHEHA. Katibu Mkuu wa CHADEMA akasema wanao ushahidi wa kutosha. Lakini wao (CHADEMA) si Serikali ila walishangaa kwa nini Serikali isiwapeleke watuhumiwa wale wa orodha ya fedheha mbele ya sheria na CHADEMA wakaitwa kutoa ushahidi kuthibitisha zile tuhuma zao?

  Tunashtukia pale Bahari Beach Julai 28 Mwenyekiti akipiga “about turn” suala zima la ufisadi wa Mzee Lowassa. Tunaambiwa Mwenyekiti wa CHADEMA aliyeyusha (dilute) msimamo wake kwa kusema, “CHADEMA siyo Mahakama kwa kila kukicha kuendelea kuwatuhumu watu kwa kashfa mbalimbali pasipo kuwa na ushahidi (Tazama Uhuru Toleo No. 22193 la Jumatano tarehe 29/07/2015 uk. 2 ile ibara ya 3… “MBOWE AJIKANGANYA”).

  Kumbe CHADEMA mnajua kazi za Mahakama! Siyo mahali pa tuhuma, bali ni mahali pa kusikiliza kesi za watuhumiwa na pa kutolea uamuzi! Hivyo leo mnatuambia ile ORODHA YENU MLIYOTOA MWEMBE YANGA haikuwa ya kweli, bali zilikuwa ni tuhuma tupu. Itakuwa sahihi kwa watu sasa kusema kumbe yale yote yalikuwa ni “MAJUNGU MATUPU” maana hamna uthibitisho wa tuhuma zote mlizozitoa katika mkutano ule! Sasa tunaamini CHADEMA ni chama cha wapika majungu na wapangaji wa fujo tu hapa nchini.

Pili, Mwenyekiti wa CHADEMA amenukuliwa kusema: “Hata mimi niliwajibu kuwa hatuwezi kumpokea Lowassa, tena niliwajibu kwa Kiingereza, “OVER MY DEAD BODY” (sitampokea mpaka kufa” (Soma hayo kutoka SAUTI HURU toleo No. 346 la Alhamisi Julai 30, 2015 uk. 2 chini ya kichwa cha habari, “SLAA KUREJEA CCM”) Huku kumeza matapishi yake Mwenyekiti ndiko ninakuita “SOMERSAULTING” katika siasa. Nani ameidhinisha kumpokea Lowassa? Je, Mwenyekiti ulikuwa umekufa? Ni siasa gani chafu hizi mnazozileta katika nchi?

  Tuwaeleweje viongozi wetu wakuu wa CHADEMA? Mbowe alikwenda mbali zaidi katika kulamba matapishi yake yale alipotupeleka kwenye maandiko matakatifu ilimradi athibitishe CHADEMA haina watakatifu. Kumbe wapo wakosefu kama Lowassa pia. Ndiyo kusema ukosoaji wao wote ni blabla tu hamna chembe ya ukweli? Mbowe amenukuliwa kusema, “Ni nani aliye mtakatifu mpaka awe na uwezo wa kushika jiwe na kumpiga mwenzake”? Hii si CCM tu hata CHADEMA na Lowassa” (SUATI HURU toleo No. 346 la Alhamisi Julai 30, 2015 uk. 2 safu ya3 ibara ya juu mwanzo kabisa). Kwa kauli ile aliwazima wale wote waliojaribu kuhoji uhalali wake (Mbowe) kumkaribisha au kumpokea Mzee Lowassa katika CHADEMA wakubaliane mara moja na ule uamuzi wake. Je, utaratibu wa namna hiyo katika chama siyo dalili ya udikteta?

  Mtazamo wangu ni kwamba siasa ni mchezo mchafu. Leo unasema hivi na kesho wewe yule yule unang’aka na kusema tofauti kabisa na ulichokisema huko nyuma. Sasa basi mshangao wangu mimi juu ya Mbowe na Dk. Slaa ni kuwa wote hawa ni Wakristo, ndiyo maana Mbowe amerejea kwenye maneno ya Injili ya Mtume Yohana sura ile ya 8 aya au mistari ya 7-9).   Ningewashauri wanasiasa hawa waache kudanganya watu, uongo wa aina yoyote ile ni DHAMBI. Kama kweli wanaiamini Injili basi wasituhumu viongozi wa chama tawala kwa kujinufaisha tu. Kwa hili naomba viongozi wakuu wa CHADEMA wanaofurahia kutoa kashfa zisizo na ukweli wala hawawezi kuzithibitisha kama ilivyotokea kwa Mzee Lowassa kuwa fisadi kumbe hawakuwa na uthibitisho wowote, waache TABIA hii.

  Sasa wanasema “CHADEMA ni chama cha kujenga mshikamano na hakiwezi kuhukumu bila ushahidi”, ni maneno ya Mbowe pale Bahari Beach, Julai 28, 2015 wakati anampokea Mzee Lowassa. Basi wamrudie Mungu na watafakari vyema yale maneno ya Mtume Matayo katika sura ya 7. Maneno yenyewe yanasema hivi: “Nawakumbusha wasomaji wangu, Mahayo 7 tunasoma hivi “MSIHUKUMU, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa HUKUMU ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa (Mat. 7:1 – 2). Kadiri mlivyowahukumu mafisadi  akina Lowassa pale Mwembe Yanga, nasi sasa tunawahukumu kwa uongo wenu ule.

Mimi nimeona watu kama akina Dk. Slaa, akina John Mnyika, akina Tundu Lissu na Mbowe mwenyewe wamejijengea utamaduni wa kuwahukumu wengine serikalini kuwa ni mafisadi. Wasomaji, mtakumbuka ulitokea wakati Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, alitamka wazi hawako tayari sasa kupokea makapi yaliyoachwa katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi ndani ya vyama vingine. Swali, huyu Mzee Lowassa hakuwa “reject” kutoka kinyang’anyiro ndani ya CCM? Je, hastahili kuitwa kapi? CHADEMA hapo wanajiteteaje katika hili? Mtu huyu ametuhumiwa na CHADEMA kwa ufisadi, mtu huyo huyo amekataliwa uongozi katika chama chake kilichomlea, CHADEMA wamesema potelea mbali sisi ni huyu huyu sasa.

Basi kuweni wakweli na mkikataa kwa kusema siyo basi iwe ni siyo ya kweli (Yak. 5:12). Tusiendelee kudanganyana. Muwe na SERA SAFI na iwe wazi na siyo huo ubabaishaji mlioonesha Bahari Beach. Uamuzi wenu huo umetokana na UKAWA kukosa mtu wa kustahili kuwa rais ndiyo maana katika tapata (desperate situation) yenu mkaangukia kumpigia magoti mzee kada wa CCM Lowassa aje awatoe kwenye dimbwi la wasiwasi katika uteuzi wa mgombea kutoka vyama vya upinzani.

  Baba wa Taifa aliwahi kutamka kuwa upinzani bora au upinzani wa kweli utatokana na viongozi wa CCM. Haya, mmekubali maneno haya na kwa hiyari yenu mmekwenda kumkumbatia kada wa CCM aje awaopoe. Ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo, haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. (Nyerere: Tujisahihishe uk. 3 ibara ya I toleo la 1962). Ni ukweli usiopingika kuwa kiongozi mzuri ni yule aliyepikwa na CCM tu. Na mheshimiwa Lowassa amepikwa na kuiva.

  Lengo hasa la upinzani ni kuingo’a CCM kutoka madarakani. Hapo upinzani wanasema wako tayari kutumia kila njia halali au hata haramu (by hooks or crooks) ilimradi waing’oe CCM madarakani. Lakini upo usemi wa kale wa Kiingereza kwamba “The end does not justify the means” kwa tafsiri ya kwamba “LENGO HALIHALALISHI NJIA za kulifikia”. Tutumie njia safi na halali kuing’oa hiyo CCM kama kweli lengo lenu ni kutaka kuwakomboa Watanzania. Basi ni lengo zuri sana ila tutafute njia sahihi za kulifikia au za kulitekeleza.  

  Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, akihutubia umati wa wananchi kule Geita, katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyankumbu Jumatatu Julai 20, 2015 amenukuliwa kusema, “Ndugu wananchi, mgombea wa UKAWA nimtaje, nisimtaje? Tumeshampata mgombea urais wa UKAWA na mnampenda sana, mnamjua sana, ni mtu anayefahamika nchi nzima na duniani”.

  Basi kwa kupagawa kwake na furaha mbele ya umati wa wananchi wale, Lissu akajikuta akiropoka na kutaja jina la Dk. Slaa. Soma (Mwananchi toleo No. 5473 la Jumatano Julai 22, 2015 uk. 4).

  Wiki moja tu baada ya ropoka ile, CHADEMA hao hao wanakutana Bahari Beach, wanataja jina la Mzee Lowassa. Hapo kweli chama hiki kina mshikamano na chain of command moja? Yaani mtiririko wa kutoa uamuzi na nani anakisemea chama? Hapo wanajengeana uhasama miongoni mwao viongozi hawa. Lissu kutaja jina lake, Mbowe kutaja jina lake bado Dk. Slaa naye kama Katibu Mkuu atakuja kutaja jina lake. Hapo CHADEMA ina msimamo au ni vurugumechi tu?

  Je, wale viongozi wengine ndani ya UKAWA kama Mhe. Profesa Lipumba, Mhe. James Mbatia na Mhe. Dk. Emmanuel Makaidi wanabaki kuburuzwa tu na uongozi wa CHADEMA? Ama kweli, madaraka kitu kingine! Waswahili wana msemo huku pwani kuwa hewala si utumwa, au kubali yaishe! Ndivyo viongozi wale wengine katika UKAWA wanavyoelekea kutenda.

  Ninaamini CHADEMA kwa hili ndiyo UKAWA maana wanaonekana kuwa na kura ya turufu. Vinginevyo basi CHADEMA wameshika mpini na hao wengine wameshika kwenye bapa la kisu. Wakijaribu kufurukuta tu CHADEMA wakavuta hicho kisu, vyama vile vingine ndani ya UKAWA vitadhurika! UKAWA watasambaratika.

  Wanaona bora hali iwe hivyo ilimradi UKAWA waonekane ni wamoja kweli. Huko mimi naita ni kujidhalilisha kwa hao viongozi wa vyama vingine wasiokuwa na ushawishi wowote (no influence) katika uteuzi wa mgombea urais wa UKAWA. Hayo ni maoni yangu au mtazamo wangu kadiri ya mambo yalivyo sasa.

Kwa misemo namna hii, viongozi wetu hao ndani ya UKAWA wanakubali lolote litakaloamriwa na CHADEMA, wako tayari kulipokea ilimradi wakidhi lile lengo lao la umoja huo la kuing’oa CCM. Je, huo ni UZALENDO? Ni mapenzi kwa nchi yako au ndiyo uchu wa madaraka? Mbona tunadanganyana?

  Uzalendo ni zaidi ya kufikiria cheo na madaraka. Kumng’oa mwenzako ni uhusuda siyo uzalendo. UKAWA mpo? Tafakarini mivurugano ya ndani ya CHADEMA kisha tuelezeni chaguo lenu katika urais ni NANI? Tuachane na huo umamluki katika siasa za nchi hii. Kama ni Lowassa basi na iwe hivyo ikubalike kiutaratibu.

Ninajua mwanasheria mkuu wa CHADEMA kakazia kusema kuwa lengo la UKAWA eti wamefanya hivyo kwa sababu UKAWA wanataka OKTOBA 25 iwe ndiyo mwisho wa utawala wa zaidi ya nusu karne wa CCM, na mfumo wao wa utawala. Wamefanya  utafiti wa kina, mpaka kupata jina la Lowassa. Ahaa! Hapa wametua. (Mwananchi Toleo No. 5484 la Ijumaa Julai 31, 2015 Uk. 2)

  Lissu huyo huyo Geita alimtaja Dk. Slaa, wiki hii Dar anamkangamalia Mzee Lowassa, ndivyo dunia ilivyo bendera hufuata upepo tu. Lazima afyate mkia kwa bosi wa chama chake. Kwa Kilatini upo usemi unadhihirisha hali hiyo. Usemi ule uko hivi: “Qui mayor, minor chesat” Mkuu akitamka jambo, mdogo unafunga domo lako.

Wananchi tunabaki kujiuliza ukweli ni upi na uongo ni upi? Dk. Slaa hajatamka lolote na wala hajajitokeza katika vikao vya CHADEMA. Sasa kikatiba anayeitisha vikao vya chama ni nani? Hivi maji na mafuta vinachanganyika kweli?

  Mie nangojea kuona namna Mhe. Edward Lowassa na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa watakavyokaa katika meza moja kuishambulia CCM katika majukwaa wakati wa uchaguzi ujao! Hapo ndipo mtu utakapotambua siasa ni nini. Wanasiasa ni watu wa namna gani? Wananchi tuamini chama kipi cha kutuongoza huko tuelekeako? Tuchague CCM au tuchague UKAWA inayoburuzwa na CHADEMA?

  Mungu atuepushe na mivurugano ya ndani ya vyama vya upinzani. Tunaomba sana wakubaliane kiongozi mmoja wa kupeperusha ile bendera ya upinzani kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.  Basi sisi yetu macho na masikio. Tutaona mengi, tutasoma mengi na mwisho wa Oktoba UKWELI utajulikana. Wananchi peke yao watatoa UAMUZI wa kukabidhi nchi kwa chama kipi.

Mungu ibariki Tanzania.