Matokeo ya utafiti uliofanywa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini (DCC), umebaini kwamba wanafunzi wa vyuo vikuu hasa vya Dodoma pamoja na baadhi ya askari polisi wa mkoa huo, wamekuwa watumiaji wakubwa wa dawa hizo.
Mtaalamu kutoka DCC na mmoja wa watafiti wa mradi huo, Yovin Ivo Laurent, alieleza hayo hivi karibuni Dar es Salaam wakati akitoa matokeo ya utafiti kuhusu matumizi ya dawa za kulevya uliofanywa katika mikoa 12 nchini katika vipindi tofauti.
Kwa mujibu wa Laurent, polisi wa mkoa huo wamekuwa wakiwaruhusu watumiaji wa dawa hizo kwenda kupata huduma hizo za dawa za kulevya katika jengo lao wenyewe pia (askari polisi) wamekuwa watumiaji wa dawa hizo.
“Dodoma ni mkoa pekee ambao askari wake wamegundulika kuwaruhusu watumiaji wa dawa hizo za kulevya hasa heroin na bangi katika jengo lao wenyewe pia wao kutumia dawa hizo, uwepo wa vyuo vikuu mkoani humo umeongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya wanafunzi na walimu wake kutumia dawa hizo,” anasema Laurent.
Anasema kwamba wamepata habari za baadhi ya askari polisi wa Mkoa wa Dodoma kuwa miongoni mwa watumiaji wakubwa wa dawa hizo kutokana na kuelezwa wale wa kawaida ambao walidiriki kuwataja askari hao hata kwa majina.
Laurent anasema, kwa mujibu wa watumiaji wa kawaida askari hao wamekuwa pia wakishiriki kuwalinda watumiaji wa dawa hizo.
Ameongeza kwamba pamoja na wanafunzi wa vyuo hivyo kuwa watumiaji wa dawa hizo, utafiti wao umebaini kwamba katika Mkoa wa Mwanza mahakimu wamekuwa pia watumiaji wa dawa hizo pamoja na wananchi wengine wa kawaida.
Naye, Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Kenneth Kasseke, ameeleza kwamba utafiti wao ulijikita katika mikoa 12 ya Tanzania Bara, kati ya Julai na Septemba 2013 wakati wa Awamu ya Pili ulifanyika Mei na Agosti, 2014.
Kwa mujibu wa Kamishna Kasseke, utafiti wa kwanza ulifanywa katika mikoa mitano ya Mtwara, Morogoro, Pwani, Dodoma na Kilimanjaro wakati ule wa awamu ya pili ulifanyia katika mikoa saba ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Kigoma, Arusha, Tanga na Dodoma.
Pamoja na mambo mengine, katika utafiti huo wataalamu wamebaini kwamba Mkoa wa Tanga umebainika kuwa kinara kwa matumizi ya dawa hizo.
Mtafiti kutoka DCC, Moza Makumbuli, amesema katika utafiti wao walioufanya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha California-San Francisco (UCSF), sifa walizozitumia kuandaa ripoti yao ni kuwahoji watumiaji wenye kati ya miaka 15 na kuendelea ambao wametumia dawa hizo kwa mwezi mmoja na kuendelea.
Anasema lengo la utafiti huo ni kuangalia ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya nchini, na kwamba katika utafiti wao wamebaini kwamba watumiaji wengi wamekuwa wakitumia dawa hizo kwa kunusa, kujidunga na hata kumeza.
Naye Syangu Mwankemwa pia kutoka DCC anasema kwamba watumiaji wengi wanaojidunga hutumia sindano moja kwa watu zaidi ya watatu na kwa kutokuwa na ufahamu huo, kila atumiaye sindano hiyo huiosha kwa kudhani kwamba kufanya hivyo kunaweza kuwawezesha kuepuka kupata magonjwa kama vile virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine.
Kadhalika, Joel Ndayongeje kutoka Chuo Kikuu cha California-San Francisco, amesema katika utafiti huo wametembelea miji 47 iliyopo katika mikoa hiyo 12 kwa kuwahoji watumiaji 436 wa dawa za kulevya sawa na asilimia 75.
Amesema kati ya watumiaji hao waliofikiwa katika mikoa 12; Mkoa wa Tanga ulikuwa na watumiaji 60 wakati Geita ulikuwa na watumiaji wanane pekee.
“Kati ya watumiaji tuliowafikia asilimia 29 walikuwa na elimu ya shule ya msingi, 16 ya sekondari na asilimia 28 ya watumiaji wa dawa hizo waliacha shule,” anasema Ndayongeje.
Ametaja shughuli ambazo watumiaji wengi walikuwa wakizifanya kwamba ni shughuli haramu za ufanyaji ngono ili wapate pesa ya kujinunulia dawa za kulevya, uuzaji wa dawa za kulevya pamoja, upigaji debe na nyingine.
Naye Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar, Eliangu Khamisi, amesema njia pekee ya kudhibiti matumizi ya dawa hizo nchini ni kutoa elimu kwa jamii ikiwamo ya watumiaji wa dawa hizo ili waweze kufahamu madhara ya matumizi ya dawa hizo.
Pamoja na hilo, Kamisha Khamisi ameshauri tafiti hizo ziandaliwe kwa lugha nyepesi ili ziweze kueleweka kwa wananchi wa rika zote.