Na Mwandishi wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imesema haina mpango wa kubadili utaratibu uliowekwa kwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa kukaa miaka sita bila kuoa ama kuolewa mara baada ya kujiunga na jeshi hilo.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Dkt. Stergomena Tax ameliambi Bunge kuwa kwa sasa utaratibu huo utabakia kama ulivyo kutokana na misingi iliyowekwa kwa ajili ya kuwaandaa askari hao kulinda nchi.
Dkt. Stergomena amesema askari wapya wanaojiunga na Jeshi wanahesabiwa kama wapiganaji ambao wapaswa kupewa ujuzi zaidi na kutumika kwenye vita hivyo miaka sita iliyowekwa ya kutokuoa ama kuolewa na inatoa nafasi kwa askari hao kutumika katika shughuli za medani.
Waziri huyo wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa jimbo la Bunda, Boniface Getere aliyetaka kupunguzwa kwa miaka sita iliyopo kwa kwa sasa kwa askari wapya wa Jeshi kuoa ama kuolewa na kuwa mwaka mmoja ama miaka miwili.