Na Asila Twaha,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kuanisha maeneo ya kimkakati ili ujenzi wa vituo vya afya vijengwe katika maeneo hayo na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Mhe.Dkt.Festo Dugange wakati akijibu maswali bungeni leo kwa niaba ya Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Raia TAMISEMI wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu Kiswaga aliyetaka kujua lini Serikali itapeleka huduma ya vituo vya afya katika vijiji vya Lutale,Kwamanga na Igogo.
Mhe. Dugange ameongeza kuwa Serikali ilishatoa utaratibu na kuzielekeza Halmashauri zote nchini kuanisha Kata za kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.
Ameongezea kuwa ujenzi wa vituo vya afya utazingatia vigezo na si kila eneo litajengwa vituo hivyo.
Aidha, ametoa wito kwa Mhe. Mbunge na Mkurugenzi wa Halamshauri ya Wilaya Magu kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuangalia na kuanisha maeneo yenye vigezo hivyo ili hatua za haraka zichukuliwe ujenzi uanze na wananchi wapate huduma.
Mapema Naibu Waziri amewatoa hofu Waheshimiwa Wabunge kuwa, ujenzi wa vituo vya afya vitakavyojengwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa tiba amesema, bajeti ya mwaka 2022/23 Serikali imetenga sh. bilioni 69.95 ambapo vifaa hivyo vitaenda kwenye vituo vya afya 530 vinavyojengwa nchi nzima.
“Ninapokea shukrani za Mbunge wa Rungwe Antony Mwantona kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluh Hassan kwa kujenga vituo vya afya vitatu ndani ya mwaka mmoja ndato,kimwa, imenjora” amesema Dugange.
Aidha ameongeza kuwa, vituo vya afya vilivyokamilika vitapewa kipaumbele kwa kupatiwa vifaa tiba ili viweze kutoa huduma na wananchi waweze kupata huduma.
Dugange amesema, Serikali itaendelea kusimamia sekta ya afya na kuendelea kuweka mipango mizuri ili vituo vyote vinavyojengwa kuwekewa vifaatiba.