Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrsai ya Kongo(DR CONGO) zimetiliana saini ya makubaliano katika ushirikiano wa kuboresha sekta ya ulinzi ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mahusiano mema yaliyopo baina ya Mataifa hayo.
Akizungumza jana baada ya zoezi la kusaini hati ya makubaliano Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nchini Tanzania *Stergomena Tax* amesema kwamba zoezi la makubaliano limeanza baada mazungumzo ya kamati ya ushirikiano sekta ya ulinzi *JPC* ambapo kamati hiyo ikafikia makubaliano hayo.
Aidha amesema kwamba makubaliano hayo ni mwendelezo wa ushirikiano wa kuimarisha sekta ya ulinzi ya Tanzania na DR Congo ili kuwa na mwambata wa wanajeshi yaani Tanzania kupokea wanajeshi kutoka DR Congo huku DR Congo ikipokea wanajeshi kutoka Tanzania kwa ajili yakukabiliana na vitendo vya uhalifu.
“Makubaliano haya yamelenga kuboresha maeneo mbalimbali katika sekta ya ulinzi ikiwemo kubadilishana taarifa za kiintelejensia,kufanya kwa pamoja mafunzo na mazoezi ya kijeshi na kitaalamu, kutembeleana ‘ kushirikiana katika masuala ya maafa,pia kushirikiana katika tiba wakati wa oparesheni mbalimbali” amesema Waziri Stergomena.