Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeteketeza vifungashio tani 44.4 ambavyo vimepigwa marufuku kwa matumizi, ambapo uteketezaji huo umefanyika katika kiwanda cha Saruji cha Twiga Cement Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika zoezi hilo ambalo limefanyika leo Septemba 14,2022 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe amesema katika tani 44.4 za mifuko ambayo imekamatwa na kuteketezwa, mifuko tani 41 zimekamatwa katika Wilaya ya Kinondoni.
Amesema wataendelea kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu kuhakikisha mifuko ya plastiki inaondoka katika mazingira ili kuokoa viumbe hai ambavyo vingeweza kuathirika na mifuko hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka amesema uwepo wa vifungashio hivyo vinaathiri afya za binadamu na wanyama kwani kumekuwa na matumizi ambayo si sahihi hasa kufungashia chakula cha moto na kusababisha kumleta madhara ya kiafya kama saratani na magonjwa ya damu.
“Hivi vifungashio havitakiwi kuwa sokoni ndo maana tunachukua jukumu la kuteketeza ili kuwaonyesha wengine kwamba hivi vifungashio havipaswi kuwa kwenye mazingira kwasababu vikiingia kwenye mazingira vitaathiri ustawi wa jamii”. Amesema Dkt.Gwamaka.
Aidha Dkt.Gwamaka amesema zoezi hilo linaendelea kwa mikoa mingine kukamata vifungashio hivyo, na amewataka wananchi kuacha mara moja kutumia mifuko ya plastiki ili kulinda afya zao na wanyama.